Iweje kuwe na wachezaji wengi wapenzi wa jinsia moja wanawake kuliko wanaume?

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya kupachika magoli mawili kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake, mshambuliaji machachari wa Marekani Megan Rapinoe aliulizwa juu ya hisisa zake kwa kucheza kwenye kiwango bora kwenye mwezi wa kupigia chapuo haki za wapenzi wa jinsia moja.
"Ndiyo wapenzi wa jinsia moja! Hauwezi kushinda michuano hii bila ya kuwa na wapenzi wa jinsia moja kwenye timu yako - haijawahi kutokea. Hiyo ni sayansi," mchezaji huyo alisema baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Ufaransa ambao ndio wenyeji wa michuano hiyo kwa mwaka huu.
Maneno ya mchezaji huyo yanaweza kuzua mjadala mkubwa kwenye jamii, lakini kuna jambo moja la msingi la kuliangalia, jinsi ambavyo yupo huru kusema kuwa yeye ni mpenzi wa jinsia moja na wapo wengi kama yeye kwenye mchezo huo.
Kujitaja kwa ufahari
Nyota huyo wa Narekani ni moja ya wachezaji 38 ambao wamejitokeza wazi tena kwa ufahari na kusema wao ni wapenzi wa jinsia moja katika michuano hiyo inayoelekea tamati, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mtandao wa Outsports, ambao umejikita kwenye habari za wapenzi wa jinsia moja.
Namba hiyo ya wachezaji ni sawa na asilimia 6.9 ya wachezaji 552 kutoka mataifa 24 waliyoshiriki mashindano hayo.

Chanzo cha picha, Kevin C. Cox
Outsports inadai kuwa namba hiyo ni rekodi mpya katika michuono yeyote ya Fifa - michuano iliyopita iliyofanyika nchini Canada mwaka 2015 ilikuwa na wapenzi wa jinsia moja 23.
Je, kulikuwa na wachezaji wangapi waliojintangaza hadharani katika Kombe la Dunia la wanaume mwaka 2018 nchini Urusi kuwa ni wapenzi wa jinsia moja?
Hakuna hata mmoja.
Kiuhalisia, hakuna hata mchezaji mmoja mwenye jina kubwa kwa upande wa wanaume ambaye ameshawahi kujitokeza mbele ya umma kuwa anajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Mchezaji anayefahamika zaidi ni Thomas Hitzlsperger, wa Ujerumani ambaye alijitangaza baada ya kustaafu mwaka 2014.

Chanzo cha picha, Getty Images
Uchokozi
"Kwenye vyumba vya kubadilisha nguo kuna maongezi mengi, uchokozi na kuoga kwa pamoja, ni mazingira magumu, na naelewa kwa nini ni vigumu kwa wachezaji wa kiume kujitangaza hadharani," anasema mshambuliaji wa Chelsea Olivier Giroud, ambaye alishinda Kombe la Dunia na timu ya taifa ya Ufaransa mwaka 2018, alipohojiwa na gazeti la Le Figaro.
"Ni kitu kigumu sana kufanya baada ya kutengeneza jina lako kwa muda mrefu," ameongeza Mfaransa huyo ambaye ameshiriki kampeni kadhaa za kukemea unyanyapaa kwa wapenzi wa jinsia moja.
Si kwamba kwenye michezo mingine hali ni tofauti na kuwa wapenzi wa jinsia moja wanajitokeza: mwaka 2016 katika Michezo ya Olimpiki jijini Rio Brazil, Outsport iliorodhesha wanariadha 56 ambao wamejitangaza kuwa wapenzi wa jinsia moja kati ya michezo 28 iliyoshindaniwa na wanamichezo 10,000.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kushambuliwa na mashabiki
Utofauti baina ya wanaume na wanawake kwenye mpira wa miguu, mchezo unaopendwa zaidi duniani ni mkubwa sana.
"Takwimu zinaonesha kuwa wachezaji wanawake wanawake wanapendwa na mashabiki na wanakubalika hata wakijitangaza kuwa ni wapenzi wa jinsia moja," anaeleza Profesa Stacey Pope kutoka kitengo Michezo na Sayansi ya Mazoezi, Chuo Kikuu cha Durham.
"Kwa upande wa wanaume, mpira wa miguu kihistoria umekuwa ukihusiswa na mabavu na wale waliojitangaza awali walipata mapokezi hasi," anaeleza.
Pope anatoa mfano wa Justin Fashanu, ambaye mwaka 1990 alikuwa mchezaji wa kwanza kujitangaza kuwa ni mpezi wa jinsia moja katika ligi za juu za England.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wachezaji wanawake hata hivyo wanakumbana na ubaguzi, ikiwemo watu kuamini kwamba kila mwanamke anayecheza ni mpenzi wa jinsia moja.
Lakini Profesa Pope anaamini kutokana na hisia hizo, inakuwa rahisi kwa wanawake kujitangaza.
'Kutokukubalika kwa wanaume'
"Kwa upande wa wanaume, mashabiki wanaamini wapenzi wa jinsia moja hawana nguvu za kutosha za kucheza mchezo huo," anasema Susan Cahn, Profesa wa masuala ya Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Buffalo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanaharakati hata hivyo wanadai kuwa bado wadau wa kandanda hawajajikita katika kuondosha unyanyapaa katika mchezo huo kama ipasavyo.
Kundi la wanaharakati la Kick It Out, limeripoti kuwa visa vya unynyapaa kwenye viwanja vya mpira nchini England vilizidi kwa 9% mwaka 2018 kulinganisha na 2017.
Japo Fifa huko nyuma imwshatoza faini vyama vya mpira vya nchi ambazo mashabiki wake wamekuwa wakitoa maneno ya kibaguzi kama Mexico, sheria za shirikisho hilo hata hivyo halitaji ubaguzi dhidi ya wachezaji ambao ni wapenzi wa jinsia moja kama ni kosa. Kapo ubaguzi wa rangi, dini na asili umetajwa.
Je, mashindano ya wanawake yanaweza kubadili mtazamo hasi?
"Ni jambo la kuvutia kuona wanawake ambao ni wapenzi wa jinsia moja wakiongoza katika eneo hili. Inaonesha kuwa watu wanapokubalika kuwa kama walivyo, inasaidia timu nzima," amesema Robbie De Santos, ambaye ni Mkurugenzi wa mtandao wa wanaharakati wa wapenzi wa jinsia moja wa Stonewall.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Lakini ni muhimu pia hatutakiwi kushangilia. Tunajua kuwa wachezaji wa michezo mbalimbali kwa ngazi tofauti wanashindwa kutoka hadharani na kusema wao ni wapenzi wa jinsia moja."
Mfano ni kuwa, nchi ya Ufaransa ambayo imeandaa Mombe la Dunia la wanawake, na timu ya wanaume ni mabingwa wa dunia haina mchezaji hata mmoja si mwanaume au mwanamke katika timu zao za taifa ambaye amejitangaza kuwa ni mpenzi wa jinsia moja.
Susan Cahn pia anasema licha ya wachezaji wanawake wanazidi kujitokeza na kusema wao ni wapenzi wa jinsia moja, idadi ya mashabiki inaongezeka, jambo ambalo anasema ni kubwa na la kufurahisha.












