Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mlanguzi wa mihadarati aliyejivalisha kama mwanawe wa kike ili kutoroka jela akamatwa
Mlanguzi wa mihadarati nchini Brazil alikamatwa akijaribu kutoroka jela ambayo alikuwa anazuiliwa kwa kujifanya kuwa mwanawe wa kike mwenye umri wa miaka 19.
Mamalaka ya gereza hilo mjini Rio de Jeneiro ilitoa kanda ya video ikimuonyesha mfungwa huyo akiwa amevalia nywele bandia , barakoa , sidiria na tishati iliokua ikim'bana.
Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 42 alivitoa vitu hivyo kimoja kimoja ili kuonyesha mwili wake wa kiume ambao haufanani na mwanawe wa kike.
Maafisa wamesema kwamba mwanawe huyo huenda akashtakiwa kwa kumsaidia mfungwa kutoroka jela.
Wanasema kwamba msichana huyo mwenye umri wa miaka 19 alikuwa ameenda katika jela hiyo kumtembelea babake Clauvino da Silva katika jela hiyo ya Rio de Janeiro kwa jina Bangu 3 ambapo alikuwa akihudumia kifungo cha miaka 73 na miezi 10.
Mamlaka ilisema kwamba Silva alikua akipanga kumuacha mwanawe wa kike nyuma huku akijaribu kujipatia uhuru kwa kujaribu kuwa kama yeye.
Lakini walinzi hao hawakufanywa wajinga na hatua yake na baada ya kumlazimu kupigwa picha mbele ya jela hiyo walizisambaza picha hizo kwa vyombo vya habari na mtuhumiwa huyo akarudishwa jela.
Sio mara ya kwanza kwa mfungwa kumwacha mtu wa famili jela ili kujaribu kutoroka.
Mwaka uliopita mfungwa mmoja raia wa Peru alimpatia dawa ya kulala nduguye pacha na kumwacha ndugu huyo kuhudumia kifungo chake.
Mamalaka haikugundua tukio hilo hadi pale mfungwa huyo alipokamatwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kutoroka.
Mwanawe wa kike na watu wengine saba ambao walikuwa wamemtembelea Silva kwa sasa wanahojiwa.
Maafisa wa jela wanaamini kwamba walipenyeza vifaa vilivyotumiwa na Silva kujifanya mwanawe.
Wanashuku kwamba mmoja wao , mwanamke mjamzito ambaye hakupekuliwa na walinzi alikuwa ameficha nywele hizo bandia na miwani iliotumiwa na Silva mwenyewe.
Hili sio jaribio la kwanza la kutaka kutoroka la Silva.
Mwaka 2013, alikuwa miongoni mwa kundi la wafungwa 31 waliotoroka taasisi ya Vicente Piragibe iliopo Gericino kupitia bomba la maji taka la jela hiyo.
Baadaye alikamatwa.
Maafisa wanasema kwamba atahamishwa hadi katika jela kuu ili kuzuia majaribio hayo ya kutaka kutoroka.