Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Mimi ni ushahidi wa kutosha kwamba babangu ni mbakaji'
Mwanamke aliyedaiwa kuzaliwa baada ya tendo la ubakaji anataka babake kushtakiwa katika kesi moja ya aina yake , BBC imegundua.
Vicky anasema kuwa mamake alikuwa chini ya umri wa miaka 30 wakati rafiki mmoja wa familia alipombaka.
Anasema kwamba uzawa wake ni thibitisho la uhalifu na anataka vinasaba vya DNA kufanyiwa vipimo ili kumpeleka jela babake kwa tendo la ubakaji.
Maafisa wa polisi wa West Midlands wanasema sheria haimtambui yeye kama mwathiriwa.
Vicky ambaye sio jina lake kutoka mji wa Birmingham aliasiwa miaka ya 70 akiwa na umri wa miaka saba.
Akiwa na umri wa miaka 18 alianza kumtafuta mama aliyemzaa na kugundua kutoka kwa mfanyakazi mmoja wa jamii na rekodi zake za huduma kwa jamii kwamba alizaliwa baada ya ubakaji.
''Mamangu mzazi alikua na umri wa miaka 13 -akiwa mwanafunzi wakati huo na babangu ni rafiki wa familia ambaye alikuwa na umri wa miaka 30'' , Vicky alielezea kipindi cha BBC Victoria huko Derbyshire.
Rekodi hizo zinasema kwamba mamake Vicky alikuwa ameenda katika nyumba yake kama mfanyikazi wa nyumbani wa kumuangalia mwanawe wakati alipobakwa.
Ubakaji huo umetajwa katika sehemu saba za faili hizo. Rekodi hizo zinaonyesha jina lake na anwani , kwamba wahudumu wa jamii, maafisa wa polisi , maafisa wa afya walijua lakini hakuna hatua iliochukuliwa.
Ilinifanya kuhisi hasira nyingi, na kumuonea huruma mamangu mzazi.
Ushahidi wa wazi
Vicky alifanikiwa kuonana tena na mamake mzazi, akitaja wakati huo kama kitu kisicho cha kawaida.
Miaka kadhaa baadaye, wakati kesi za unyanyasaji wa kihistoria zilipoanza kuangaziwa na vyombo vya habari kufuatia kashfa iliomkumba Jimmy Savile aliamua kuchukua hatua.
Wakati huo wote alidhania kwamba ni makosa kwamba babake hakuwa ameshtakiwa.
''Ni wakati huo ndiposa nilikumbuka kwamba kuna ushahidi wa DNA''. Mimi ni sawa na tukio la uhalifu linalotembea. Na kila kitu kimeandikwa katika faili. Kwa kweli watu watagundua kwamba mimi ni mkweli. Nilitaka awajibike, Nilitaka haki kwa mamangu, nilitaka haki yangu. Matokeo ya kitendo alichokifanya yameathiri maisha yangu yote''.
Mamake mzazi ambaye hakutaka kukumbuka kisa hicho na ambaye hakusaidiwa na maafisa wa polisi licha ya kisa hicho kujulikana hakutaka kuripoti kisa hicho tena lakini akamuunga mkono mwanawe ambaye amekuwa akiifuatilia kesi hiyo.
Vicky aliitaka idara ya polisi kukubali kesi isiokuwa na mwathiriwa wakati mwathiriwa anapokataa kutoa ushahidi; Licha ya kwamba ushahidi huo upo - hatua inayomlazimu mamake kuhusishwa.
''Nasema kwamba wanaweza kutumia ushahidi na vibali vya kuzaliwa ili kuthibitisha miaka''.
Kesi hizo ambazo zinafanyika kwa kutumia ushahidi pekee zinaweza kutumika katika kesi za ubakaji wakati ambapo mwathiriwa amejiondoa ama kukataa kuhusika kutoa taarifa lakini uma umeomba kufuatilia.
Lakini maafisa wa polsi ,huduma za jamii , mawakili na wabunge wamemwambia kwamba sio mwathiriwa na kwamba hakuna kesi inayoweza kuanzishwa , anasema.
''Kwasababu ya uhalifu huo mimi niko hai. Maisha yangu yote yanatokana na tendo hilo, lakini hakuna mtu anayeniona mimi kama mwathiriwa. Naishi, nikivuta pumzi kama mwana wa ubakaji na hakuna anayejali. Ni vipi hilo linaweza kuwa sawa?'', anasema.
Mbunge wa leba wa eneo la Birmingham Yardley Jess Phillips anasema kwamba watoto waliozaliwa kutokana na ubakaji wanafaa kuchukuliwa kama waathiriwa.
''Madhara ambayo yatamkabili mtu, uhusiano wake, maisha yake kuhusu vile wanavyohisi, bila shaka wataathiriwa''.
''Nilidhani kwamba tumeshinda hoja hii , wazo ni kwamba sio lazima uwe mwathiriwa wa moja kwa moja - hatuwezi kusema katika muktadha wa hali ya mgogoro wa nyumbani kwamba mtoto ambaye hajaathirika na swala hilo hakuwa mwathiriwa wa uhalifu uliokuwa ukifanyika''.
Vicky alimsaka babake , akiwa amevalia kamera ya siri ili kurekodi mazungumzo yao.
Anasema kwamba hakukataa ama kuthibitisha kwamba alishiriki ngono na mamake.
''Hii ni mojawapo ya kesi za kihistoria ambazo kuna ushahidi wa kutosha. Nawataka maafisa wa polisi kuitisha vipimo vya DNA . Nawataka maafisa wa polisi na wale wa huduma za jamii kuomba msamaha na kujifunza. Vilevile nataka ufafanuzi wa neno mwathiriwa kuelezewa''.