Maelfu ya raia wa Uganda ni wahanga wa 'ulanguzi wa binadamu' Oman

Uganda imelezea hofu yake kuhusu hali ya raia wa nchi hiyo wanaofanya kazi Oman ikidai kuwa huenda ni wahanga ''ulanguzi'' wa binadamu.

Suala hilo limeangaziwa katika ripoti iliyowasilishwa bungeni leo Ijumaa.

Zaidi ya Waganda 40,000 wanafanya kazi Oman - taifa ambalo halina makubaliano yoyote ya kibiashara.

Serikali ya Uganda imekuwa ikijaribu kuwafikia raia wake ambao ni wahamiaji wanaofanya kazi Mashariki ya Kati baada ya kupokea simu za kutafuta usaidizi kutoka kwa raia hao wanaofanya kazi za ndani.

Wengi wao ni wanawake ambao wamekosa nafasi ya ajira chini mwao na kuamua kutafuta kazi katika mataifa ya Uarabuni.

Lakini mpango wa ajira kwa wahamiaji umekumbwa na madai ya unyanyasaji wa kingono pamoja na dhulma wanazopitia wafanyikazi wa ndani kutoka kwa waajiri wao.

Wengi wao wamekuwa wakinasa kanda za video na kuzisambazwa katika mitandao ya kijamii wakiomba jamaa na marafiki wawasaidie kurudi nyumbani.

Katika kisa cha hivi karibuni mwanamke wa umri wa makamo waliyekuwa akifanya kazi Jordan, alidai kuuzwa kama mtumwa kwa dola 3000.

Alimpigia simu mbunge mmoja nchini Uganda ambaye baadae aliwasilisha kisa chake katika bunge la nchi hiyo.

Licha ya changamoto zinazowakabili raia wake ugenini, serikali ya Uganda imesema kuwa haitasitisha mpango wa kuwapeleka watu wake kufanya kazi nje ya nchi.

Serikali inasema hatua yakuweka marufuku ya muda kwa mpango huo mwezi Januari mwaka 2016, ilichangia ongezeko lavisa vya ulanguzi wa binadamu.

''Kuondoa marufuku hiyo kulituwezesha kujadiliana na mataifa husika na kufikia mkataba wa kibiashara, pia ilituwezesha kuzuru mataifa hayo kubainisha kama watu wanaolalamikia visa vya unyanyasaji ni raia halisi wa Uganda.

Ukweli ni kwamba tulipochunguza walikotoka watu hao nchini Oman tulibaini kuwa ni raia wa Uganda.'' aliongeza waziri huyo wa leba.

Pia ameongeza kuwa wamefingua mfisi za kushughulikia amslahi ya wafanyikazi wa uganda waliopo Ughaibuni.

Waziri wa leba amesema serikali inajaribu kufanya rasmi mkataba wa ajira na Oman, ili kuhakikisha haki ya Waganda wanaofanya kazi nchini humo zinalindwa.

Mkataba kama huo tayari umeumetiwa saini kati ya Uganda na mataifa ya Saudi Arabia, Jordan na Falme za Kiarabu, UAE.

Karibu kampuni 200 zipepewa leseni ya kuwa mawakala wa kuwatafutia kazi ng'ambo raia wa Uganda.

Kampuni sita tayari zimefutiwa leseni kufuatia madai hayo ya unyanyasaja.