Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mshindi wa taji la urembo la wanawake 'wanene' azungumza
Tracy Nduati ni mshindi wa taji kwa Jina Miss Kenya plus Size World ,ni shindano ambalo liliwaleta pamoja warembo wanene wapatao 22, wengi wao wakiwa na uzito wa zaidi ya kilo 100 na kuendelea.Mzito zaidi akiwa na uzito wa kilo 145.
Bi Tracy amezungumza na mwandishi wa BBC, Ann Ngugi, akisema kuwa kwa kupata taji hili , imempa ujasiri wa kujiamini zaidi , kwani kutokana na unene wake amekuwa na changamoto katika kutangamana na jamii kwa ujumla .
" Sikujua kwamba siku mmoja unene wangu huu ungenipa taji lolote , kwa sababu nimekejeliwa na kuchekwa hadharani kuhusu muonekano wangu , taji hili limenitia moyo sana na nadhani kuwa ni ujumbe kwa wanawake wanene kuwa wa pia ni warembo ".
Ni mwanamke ambaye amepitia amepita kwenye milima na mabonde kutokana na ukubwa wake wa mwili.
Tukio ambalo hawezi kamwe kulisahau ni wakati mpenzi wake wa wakati huo, alikuwa anamkejeli mno kutokana na uzito wake , kwa mfano aliwahi kumuambia kuwa hawezi kutembea naye mahali palipo na watu wengi ,Tracy alipotaka kujua ni kwanini Tracy anasema mpenziwe alimjibu: "wanawake wanene kama wewe ni wa kukaa nyumbani, na sio wa kutoka nao" na ndio moja ya sababu zilizomfanya yeye kuingia kwenye shindano hili.
Anasema alichoka kuchekwa na kubeba kejeli za watu kila alipokua kutokana na unene wake.Tracy mwenye umri wa miaka 30, anasema kuwa aliona ni kheri atumie kile ambacho baadhi ya watu wanakiona kuwa kibovu kumfurahisha yeye .
Ile dhana iliyopo kwenye jamii ni kuwa mwanamke mrembo ni yule ambaye ana kiuno chembamba , na pia mrefu kama twiga, inafanya mabinti wengi kuamua kufuata mitindo ya kuhatarisha maisha yao ili wasionekane wanene . Kwa mfano mabinti wengine hujinyima chakula mchana kutwa, huku miili yao ikitetemeka kila wakati , wengine nao wanatumia dawa za kupunguza miili.
Kwa mfano mmoja wa walimbwende hawa waliokuwa wanashindania taji hili anasema kuwa anakumbuka alipokuwa msichana alitamani sana kuwa mwanamitindo wa mavazi lakini alihisi kwamba alikuwa ni mnene mno .
Wenzake wakati huo walimshauri kuwa akitumia madawa ya kulevya kwa mfano heroine na cocaine ataonekana mwembamba na atakubalika kama mwanamitindo, na hapo ndio safari yake ya uraibu wa madawa ya kulevya ilipoanzia , alikonda lakini hakuweza kuwa mwanamitindo kwa kuwa alianza kuwa mraibu.
" Imekuwa ni safari kwangu nilikuwa mwanamke asiyejielewa kwa kuwa nilipotoshwa na marafiki zangu nitumie madawa ya kulevya ili nikonde , lakini hali hii ilinifanya kuanza kulala mitaani nisijielewe hivyo taji hili japo sikushinda, limenipa ujasiri wa kuwa naweza kuwa mwanamitindo nikiwa bado mnene nilivyo"
Shindano hili limetoa mwanya kwa wanawake wanene wa kuwa chochote wanachotamani maishani.
Walioandaa shindano hili wanasema kuwa wanataka kutumia vyema tasnia ya urembo wa wanawake wanene kutoa mabalozi wazuri kusaidia la kuhamasisha jamii kuwa unene hauna kasoro yoyote na kwa hiyo unyanyapaa na dhana iliyopo kuhusu wanawake wanene utupiliwe mbali.