Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Umoja wa Mataifa wasema shambulio dhidi ya wahamiaji Libya huenda ni uhalifu wa kivita
Shambulio lililofanywa kutoka angani dhidi ya kituo cha kuwahifadhi wahamiaji nje ya mji wa Libya na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 44 linaweza kuwa uhalifu wa kivita, afisa wa UN amesema.
Karibu watu At 130 walijeruhiwa katika shambulio hilo ambalo serikali ya Libya inadai lilitekelezwa na vikosi tiifu kwa mbabe wa kivita, Jenerali Khalifa Haftar.
Vikosi vya Jenerali Haftar vinailaumu serikali kwa kushambulia kituo hicho.
Wengi wa waliouawa wanaaminiwa kuwa watu wa asili ya Kiafrika kutoka eneo la jangwa la Sahara ambao wamekuwa wakijaribu kuingia Ulaya kupitia Libya.
Maelfu ya wahamiaji wanazuiliwa na serikali katika vituo vya kuwahifadhi wahamiaji vinavyosimamiwa na serikali ya Libya.
Taarifa kuhusu mahali kilipo kituo kilichoshambuliwa siku ya Jumanne na maelezo ya raia waliokuwa wakihifadhiwa hapo yamewasilishwa kwa pande zote zinazozozana katika mgogoro wa Libya, alisema Kamishena mkuu wa kutetea haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet.
"Shambulio hili limefanywa katika mazingira ambayo yanaashiria huenda ni uhalifu wa kivita ,"alisema.
Aliongeza kuwa hii ni mara ya pili kituo hicho kinashambuliwa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea "kusikitishwa" kwake na ropoti hizo na kuomba kufanywe uchunguzi huru"kuhakikisha wahasiriwa wanapata haki".
Kwa upande wake, Baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa, limebadilisha ajenda yake, na litajadili faraghani hali nchini Libya.
Libya imetumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baada ya kiongozi wake wa muda mrefu Muammar Gaddafi kung'olewa madarakani na kuuawa mwaka 2011.
Tunafahamu nini kuhusu shambulio hilo?
Kituo cha kuwahifadhi wahamiaji cha Tajoura, ambacho kilikuwa na watu 600, kimeripotiwa kulengwa katika shambulio hilo.
Wanawake na watoto ni miongoni mwa waathiriwa, Guma El-Gamaty, mwanachama wa kundi la kisiasa linaloungwa mkono na UN, aliiambia BBC.
Afisa wa wa Wizara ya Afya nchini Libya, Dkt Khalid Bin Attia, aliionesha kiwango cha uharibifu uliosababishwa na shambulio hilo BBC ilipofika katika eneo la tukio:
"Watu walikua kila mahali, kituo kiliharibiwa kabisa, watu walikuwa wakilia hapa na wengi wao wamepata usumbufu wa kiakili, baada ya umeme kukatizwa.
"Hatukuweza kuona vizuri kilichokuwa kinafanyika japo ambulensi zilikuwa zikija na kuondoka, hali ilikua mbaya sana, kulikuwa na damu kila mahali."
Mwezi Mei Umoja wa Mataifa uliomba watu wanaoishi katika kituo cha Tajoura kuhamishwa mara moja kwa kuhofia huenda wakavamiwa.
Nani wa kulaumiwa?
Serikali ya muungano wa kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, inaongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj, inailaumu jeshi la Libya National Army (LNA) kwa kutekeleza shambulio dhidi ya kituo hicho.
Shamulio hilo la ''kikatili'' lilifanywa ''kimakusudi ''na lilitekelezwa kama ''ilivyopangwa'', ilisema serikali.
Jeshi la LNA -linaloongozwa na Jenerali Haftar - limekuwa likikabiliana na vikosi vya serikali katika eneo lilishambuliwa
Lilikuwa limetangaza siku ya Jumatatu kwamba litaanza mashambulizi makali katika maeneo maalum mjini Tripoli baada ya mbinu zote za "kukomesha" mapigano kumalizika .
LNA linasema ndege zake za kivita zililipua kambi zinazoshirikiana na serikali karibu na kituo cha cha kuwahifadhi wakimbizi.
Generali Haftar amehusika na siasa za Libya kwa zaidi ya miongo minne na alikuwa mshirika wa karibu wa Gadaffi hadi mzozo ulipoibuka kati ya mwishoni mwa miaka ya 1980 hali iliyomfanya kukimbilia mafichoni nchini Marekani.
Alirejea Libya maandamano ya kupinga utawala wa Gadaffi yalipoanza mwaka 2011, ambapo alijenga kambi katika eneo la Mashariki mwa nchi hiyo kwa usaidiza waUfaransa, Misri na UAE.
Watu wa Libya wanahisia tofauti kumhusu kutokana na ushirikiano wake wa zamani na Gadaffi pamoja na uhusiano wake na Marekani lakini wanamsifu kwa kuwafurusha wanamgambo wa kiislam katika mji wa Benghazi na viunga vyake.
Uchambuzi wa mwandishi wa BBC Sebastian Usher,
Mhariri wa masuala ya Uarabuni
Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine ya kutoa misaada ya kibinadamu yameonya kuwa mikasa kama hii haiwezi kuepukika mapigano yakizuka upya katika mji wa Tripoli ambako wahamiaji wanazuiliwa katika vituo vilivyo karibu na maeno mapigano yanaendelea.
Hali ya wahamiaji kutokea mwanzoni ilikuwa mbaya na badhi yao wamekuwa wakidhulumiwa na watekaji nyara na wanamgambo.
Umoja wa Mataifa unasema mashambulio ya anagani dhidi ya Tajoura yanaonesha kuwa sera ya Umoja wa Ulaya ya kuwaregesha Libya watu wanaojaribu kuvuka bahari Mediterrania kuingia Ulaya lazima ikomeshwe .
Sera hiyo imesaida kupunguza idadi ya watu wanaoingia barani ulaya kupitia njia hiyo japo zingine zimefunguliwa.
Lakini mshirika ya kutoa misaada ya kiutu yansema gharama ya kutekeleza sera hiyo ni ghali mno.
Baada ya oparesheni ya Jenerali Khalifa Haftar katika mji wa Tripoli kutibuka, kuna uwezekano wa vikosi vyake kushambulia watu kiholela hali ambayo itahatarisha zaidi maisha ya raia.
Lakini wanamgambio wanaowazuilia wahamiaji katika mazingira hatari karibu na eneo la vita, sharti walaumiwe chochote kikitokea