Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kenya: Rais Kenyatta amemwandikia Rais Magufuli alivyokerwa na kauli ya Jaguar
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemwandikia waraka maalum Rais wa Tanzania, John Magufuli kuelezea jinsi Serikali yake ilivyoghadhabishwa na matamshi yaliyotolewa na Mbunge wa Starehe, Charles Kanyi maarufu Jaguar.
Ujumbe huo wa maandishi umewasilishwa na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli.
Kwa mujibu wa Gazeti la Mwananchi, Bw. Majaaliwa alisema: "Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu kwani kuna baadhi ya makabila yanapatikana katika nchi hizi mbili hivyo ushirikiano katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kibiashara na ya kijamii hayawezi kukwepeka."
Aliongezea kuwa siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana Serikali husika zilikaa mezani na kumaliza tofauti hizo.
''Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.'' alisema
Wiki iliyopita, Jaguar alitoa matamshi yenye utata akiwataka raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Kenya wakiwemo Watanzania waondoke ndani ya muda wa saa 24 kauli iliyozua mjadala mkubwa.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za EAC na duniani kwa ujumla ambao wapo nchini wakifanya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi.
"Mambo yetu yote katika nchi za Afrika Mashariki hasa ya biashara na ya kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa kushirikiana," alisema Bw. Majaliwa.
Waziri Mkuu ameahidi kuwa Serikali ya Tanzania haitafumbia macho kauli iliyo na viashiria vya uchochezi dhidi ya nchi jirani ili kuunga mkono juhudi mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na viongozi wakuu wa Mataifa ya Afrika.
Kwa upande wake, Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuwatuliza Watanzania kupitia kauli yake aliyotowa Bungeni wiki iliyopita na kuwaomba wasitilie maanani matamshi ya Jaguar kwani sio msimamo Serikali ya Kenya au Wakenya wenyewe.
Balozi Dan Kazungu, aliongeza kuwa siku zote msimamo wa Rais Kenyatta umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.
Mbunge huyo ailikamatwa na kufikishwa mahakamani na kesi dhidi yake inaendelea.