Mtuhumiwa mauaji ya kimbari Rwanda ahukumiwa Marekani kwa kudanganya

Jean Leonard Teganya was convicted for immigration fraud

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Jean Leonard Teganya amehukumiwa kwa kusema uongoa katika uhamiaji

Raia mmoja wa Rwanda amehukumiwa miaka minane gerezani nchini Marekani kwa kusema uongo katika uhamiaji na kuapa urongo baada ya kuficha ukweli kwamba alihusika katika mauaji ya kimbari nchini Rwanda mnamo 1994

Jean Leonard Teganya, mwenye umri wa miaka 47, "alishtakiwa na kuhukumiwa kwa uhlaifu mkubwa wa udanganyifu katika uhamiaji: kwa kutoa taarifa za uongo kumhusu kama mhalifu wa kivita ili kupata hifadhi nchini Marekani,"amesema wakili nchini Marekani Andrew E Lelling, katika taarifa iliyotolewa na idara ya sheria.

Katika siku 100 mnamo 1994, takriban watu 800,000 waliuawa nchini Rwanda katika mauaji hayo ya kimbari.

Teganya anakana kuhusika katika mauaji hayo.

Lakini waendesha mashtaka nchini Marekani wanasema Teganya ambaye alikuwa mwanafunzi anayesomea masuala ya afya wakati wa mauaji hayo ya kimbari, alishiriki katika mauaji ya takriban watu saba na ubakaji wa watu watano wakati huo.

Licha ya kwamba mashtaka na hukumu dhidi ya Teganya yanatokana na udanganyifu huo, na sio mambo aliyoyafanya wakati wa mauaji hayo, kesi hiyo ilikuwa changamoto kubwa kwa jaji.

"Nimemhukumu kama muongo au kama muuaji au mbakaji au mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari?" Jaji F Dennis Saylor IV inaarifiwa na shirika la habari la AP aliuliza.

Maelezo ya video, Anne-Marie alipoteza watoto wake wanne na mumewe wakati wa mauaji ya kimbari

Waendesha mashtaka wa serikali huko Boston wamesema huenda wangeomba ahukumiwe maisha gerezani, iwapo hukumu ingekuwa ni kwa makosa ya mauaji na ubakaji Reuters linaripoti.

Mwandishi habari na muangalizi wa uchaguzi Elizabeth Blunt anasema kesi hiyo ina uwiano na kesi dhidi ya Tom Woewiyu, aliyekuwa msemaji wa mbabe wa kivita Liberia Charles Taylor aliyepatikana na hatia ya kusema uongo ili kuruhusiwa kuishi Marekani kwa kudanganya kuhusu alivyohusika katika vita vya kiraia nchini humo.

French forces in Rwanda were accused of not doing enough to stop the killing

Chanzo cha picha, AFP

'Mauaji katika vyumba vya kuwazalisha akina mama waja wazito'

Teganya, aliye na umri wa miaka 47, alikuwa mwanafunzi anayesomea masuala ya afya nchini Rwanda wakati mauaji hayo ya kimbari yalipotokea na alituhumiwa kwa kuongoza kikosi cha wanajeshi na kuwatambua wagonjwa wa kabila la Kitutsi hospitalini, taarifa ya Marekani imeeleza.

"Baada ya kutambuliwa wagonjwa hao wa walichukuliwa na kuuawa nyuma ya wodi ya akina mama kujifungua," imeongeza.

Teganya alitoroka Rwanda mnamo 1994 na kuishia nchini Canada ambako aliomba hifadhi. Lakini maafisa walimnyima ombi lake kutokana na kutuhumiwa kuhusika katika mauaji hayo ya kimbari.

Aliponea kurudishwa Rwanda na kuingia Marekani ambako aliwekwa kizuizini. Katika ombi lake la kutaka hifadhi Marekani, hakifichua taarifa kuhusu kuhusika kwake katika mauji hayo, serikali ya Marekani inasema.

About 800,000 people were killed in the 1994 genocide

Chanzo cha picha, AFP

Teganya anatarajiwa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo, shirika la habari la Reuters linaarifu.

Wakili wake anasema alitoroka Rwanda kutokana na kuhofia kutuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kimbari chini ya utawala uliopo.

Alieleza kuwa Teganya ni baba mzazi wa watoto wawili aliyeshika dini "aliyeishi maisha ya ukimya" kwa miaka 25 iliyopita.

Wakati hukumu yake itakapokamilika huenda Teganya akatimuliwa kutoka Marekani.