Simulizi ya mtoto aliyezaliwa baada ya mauji ya kimbari nchini Rwanda

Kijana mwenye miaka 24, raia wa Rwanda ambaye mama yake alibakwa wakati wa mauaji ya kimbari anaiambia BBC jinsi gani aliweza kubaini mazingira ya kuzaliwa kwake.Majina yao yalibadilishwa kwa sababu ya aibu iliyokuwepo baada ya mazingira ya ubakaji, ambayo mpaka sasa ipo.
Jean-Pierre anasema fomu iliyokuwa ikiuliza majina ya wazazi alipomaliza shule ya msingi ilimfanya aulize baba yake ni nani.
''Simfahamu-sikujua jina lake,'' alisema.
Tahadhari:baadhi ya watu wanaweza kukwazwa na maudhui ya makala haya
Kutokuwa na baba nyumbani halikua jambo la ajabu: watoto wengi wengine wanaweza kuwa hawana baba -zaidi ya watu 800,000 waliuawa wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.Lakini walijua majina ya baba zao.
Alisikia kwa wanakijiji wakinong'ona, na majina watu waliokuwa wakimuita- lakini ilimchukua miaka kadhaa kubaini ukweli wote.

Chanzo cha picha, Reuters
Mama yake aitwae Carine alisema akiwa imara, ''si jambo la kulipokea mara moja.''
''Alisikia habari tofauti, alisikia tetesi.Kila mtu kwenye jumuia anajua kuwa nilibakwa.Sikua na jambo la kufanya,'' alieleza.
''Mtoto wangu aliendelea kuniuliza baba yake ni nani.Lakini miongoni mwa wanaume 100 au zaidi walionibaka, sikuweza kumgundua baba.''
'Sikuweza kukimbia'
Idadi kamili ya watoto waliozaliwa kutokana na vitendo vya ubakaji wakati wa mauaji ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa siku 100 mwaka 1994 haijulikani.
Jitihada zinafanywa na Umoja wa mataifa kumaliza mzozo unaohusu unyanyasaji wa kingono-ubakaji kama silaha ya vita iliyotumika nchini Syria mpaka Colombia na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo mpaka Myanmar mwaka jana.
Walionusurika wanaeleza simulizi zao kwenye mitandao ya kijamii kwa kutumia #EndRapeinWar kuadhimiha siku ya Umoja wa mataifa ya kukomesha unyanyasaji wa kingono vitani

Chanzo cha picha, AFP
Lakini si rahisi kwa wale waliohusika kukumbuka matukio hayo-hata robo ya karne baadae.Kusikia simulizi ya Carine, ni wazi alisubiri mpaka mtoto wake alipokua vya kutosha ili kuweza kuambiwa ukweli.
Alikua karibu na umri sawa na mtoto wake alipobakwa kwa mara ya kwanza, maelfu ya wasichana na wanawake , wengi jamii ya Tutsi waliamini kuwa walifanyiwa vitendo hivyo na majirani zao wa jamii ya Hutu, wanamgambo na wanajeshi.
Mauaji ya kimbari ndio yalikua yameanza, na alikua akivuja damu kutokana na majeraha ya panga usoni-majeraha ambayo mpaka sasa yamefanya iwe vigumu kwake kula na kuzungumza.
Wauwaji-ambao kabla walikua sehemu ya jamii hiyo hiyo-walimburuza mpaka kando ya shimo ambalo walikua wakitupa miili ya wanaume,wanawake na watoto waliouawa shuleni.
Lakini pamoja na majeraha, pamoja na maumivu, Carine alijua kuwa hakutaka kufa.Alijua pia hakutaka kufa wakati kundi la wanajeshi lilipomdhalilisha kingono kwa kutumia miti na fimbo saa chache baadae, na kumsababishia majeraha makubwa.
Kundi jingine lilimshambulia, kwa kumpiga mwili mzima, akaamua kuwa hataki tena kuishi.
''Sasa ninataka kufa.Nilitaka kufa kila saa.''
Lakini shida ndio ilikua imeanza:hospitali iliyokuwa ikiokoa maisha yake haraka ilivamiwa na wanamgambo wa kihutu.
''Sikuweza kukimbia.sikuweza kuondoka kwa sababu kila kitu kilikua kimevunjika,'' alieleza.
''Mtu yeyote aliyetaka kunidhalilisha kingono aliweza kufanya hivyo.Kama wauaji wakitaka kujisaidia waliweza kujisaidia haja ndogo mwilini mwangu.''

Chanzo cha picha, Reuters
Pale hospitali ile ilipodhibitiwa na waasi wa Rwanda Patriotic Front ndipo Carine hatimaye alipata matibabu aliyoyahitaji, na aliruhusiwa kurudi nyumbani kijijini kwake-akiwa mdhoofu, aliye na majeraha ya kuvunjika, kuvuja damu lakini akiwa hai.
Madaktari walipobaini kuwa mjamzito walipatwa na mshangao.
''Niliuliza ni nini cha kufanya wakati mwili wangu haukua vizuri.Sikuweza kufikiria nini kitakachotokea.
''Mtoto alipozaliwa sikuelewa kwa nini.Sikuamini kama mtoto wa kiume ametoka kwangu.Nilikua nikijiuliza mara zote nini kilitokea.Baada ya kujifungua, nikamlea mtoto-ingawa sikuhisi mapenzi yeyote.''

Chanzo cha picha, Reuters
'Watoto waliotelekezwa'
Hadithi hii -au simulizi tofauti - imekua ikitolewa mara mia kwa watoto nchini Rwanda katika kipindi cha miaka 25 iliyopita, ingawa mara chache huelezwa kwa uwazi.
''Ubakaji ni mwiko, mara nyingi aibu hii huwapata wanawake badala ya wanaume,'' anasema Sam Munderere, Mkurugenzi wa mfuko wa Rwanda, ambao hutoa msaada wa elimu na saikolojia kwa wakina mama na watoto wao wanaozaliwa kutokana na vitendo vya ubakaji.
Wakati mwingine unyanyapaa huwafanya wakina mama kuwatelekeza watoto, hata kuvunjika kwa ndoa zao.
Ikiwezekana,wanawake hufanya siri.Matokeo yake,watoto wengi hugundua walipatikanaje, kama Jean Pierre,wakati walipokua wakijaza fomu.
''Changamoto ni kwa wakina mama kuwaambia watoto wao namna walivyozaliwa baada ya mauaji ya kimbari.Ilikua rahisi kusema baba yako aliuawa wakati wa mauaji ya kimbari.
Katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, mfuko wa Rwanda uliwasaidia wakina mama kupata maneno ya kusimulia madhila yaliyowakumba miaka iliyopita lakini ukweli mtupu,Sam anaeleza.
''Madhara yanaweza kuwa ya muda mrefu;madhara yanaweza kuwa kuanzia kizazi hadi kizazi,''anasema, akitoa mfano wa simulizi ya mwanamke mmoja ambaye alificha ukweli kuhusu baba yake kwa mumewe mpya.
Ingeathiri ndoa yake kama angefahamu.

Kuna mama mmoja ambaye alikiri alimnyanyasa binti yake kwa sababu aliamini kuwa na tabia mbaya kutokana na ''mazingira aliyozaliwa''.
Na kuna mama wengine kama Carine, ambao walijisikia kutokuwa na mapenzi na watoto wao, athari ambayo haiwezi kubainika.
''Kuna madhara ambayo hatuwezi kufikiri, anasema Munderere.''vijana wana changamoto zao na tunafanya kila tunachoweza kuwasaidia kuweza kumudu kuishi ndani ya jamii zao, kujisikia wao ni wazuri kama walivyo vijana wengine wa Rwanda.
Maumivu
Hatimaye Carine alimwambia Jean-Pierre hadithi yote, na hata uzazi wake, kijana wake alipotimiza miaka 19 au 20.
Amesema, amekubali.Lakini bado, anajisikia kuna tundu kwenye maisha yake, baba yake anaweza kuwa wapi.Amejawa chuki kwa mwanaume aliyemshambulia mama yake-lakini Carine ameamua kusamehe.
''Vitu vilivyokuwa vikinipa msongo ni kuwakumbuka walionifanyia.Unaposamehe unajisikia vizuri,'' alisema Carine.

Chanzo cha picha, Reuters
''Sikuwahi kuwa na hasira kuhusu yeye,''Jean-Pierre anaongeza.''Wakati mwingine namfikiria:Ninapokutana na changamoto za maisha huwa nawaza kuwa ningependa baba yangu angekuwepo ili anisaidie kutatua matatizo''.
Ana mpango wa kusomea ufundi na siku moja awe na familia yake.
''Nina mpango wa kuisaidia familia yangu pia,'' anasema, ingawa hivi vyote vinahitaji fedha.''
Kwa Carine, alipata huduma ya ushauri nasaha mapema, ikamsaidia kuwa na mapenzi na Jean-Pierre kadiri alipoendelea kukua:''Ninajisikia kuwa huyu sasa ni mwanangu.''
Jean-Pierre, sasa anajivunia mama yake na alivyonufaika mpaka sasa: ''ni vigumu kuona lakini nilikua na furaha sana na maendeleo yake.
''Namna alivyochukulia kwa mtazamo chanya alichokipitia.Namna anavyofikiria kuhusu wakati ujao''.













