Rashid Charles Mberesero: Mfahamu Mtanzania aliyehusika katika shambulio la kigaidi katika chuo kikuu cha Garissa Kenya

Habari kwamba raia mmoja wa Tanzania ni miongoni mwa washukiwa watatu waliopatikana na hatia ya kupanga na kutekeleza shambulio katika chuo kikuu cha Garissa nchini Kenya 2015 zimewawacha wengi na mshangao

Rashid Charles Mberesero ambaye alikamatwa na watu wengine wanne muda mfupi baada ya mkasa huo wa Garissa uliosababisha vifo vya wanafunzi 148, alipatikana na hatia hiyo wakati mahakama moja nchini Kenya ilipotoa uamuzi wake baada ya takriban miaka minne.

Katika uamuzi huo raia huyo wa Tanzania pamoja na Hassan Edin na Mohammed Abdi jina jingine Mohamned Ali Abikar walipatikana na hatia ya kupanga shambulio hilo chini ya ushirikiano wa wanachama wa kundi la Al-Shabab.

Pia walipatikana na hatia ya kuwa wanachama wa kundi la al-shabab kutoka Somalia.

Mtu wa nne Sahal Diriye Hussein aliondolewa mashtaka.

Lakini Rashid Charles Mberesero ni nani haswa?

Rashid Mberesero, aligundulika katika eneo la tukio akiwa sio mwanafunzi wala mfanyakazi wa chuo hicho.

Kulingana na gazeti la The Citizen toleo la tarehe 10 mwezi Aprili 2016, Rashid aliyesoma shule ya upili ya Bihawana mjini Dodoma alidaiwa kutoroka shule baada ya kukatazwa kuvaa kofia kichwani.

Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo wakati huo, mwanafunzi huyo alijiunga na shule hiyo mwaka 2015 baada ya kutoka shule ya upili ya Bahi Kagwe.

Chakushangaza ni kwamba licha ya kutoweka katika shule, hakuna aliyefuatilia alikokwenda

Kwa takriban miezi minne wazazi wa kijana huyo walidhani kwamba mwana wao yupo shule swala ambalo halikuwa la kweli.

Haijulikani ni nini haswa kilichomfanya kuingia katika ugaidi

Wazazi wa Rashid walishangaa kugundua kwamba mwana wao alikuwa miongoni mwa watu waliopanga na kutekeleza shambulio la Garissa.

Kwa takriban miezi minne wazazi wa kijana huyo walidhani kwamba mwana wao yupo shule swala ambalo halikuwa la kweli.

Siku za nyuma wakati ambapo kesi ya washukiwa hao ilipokuwa ikiendelea raia huyo alipatikana na ugonjwa wa kiakili akiwa jela.

Kulingana na gazeti la Daily Nation nchini Kenya, Rashid Charles Mberesero aligunduliwa kuwa hawezi kuendelea na kesi baada ya ripoti ya daktari wa maswala ya kiakili kusema kuwa alikuwa akitibiwa tatizo la kuwa na ''mienendo isiyo eleweka'' katika jela ya kamiti.

Kulingana na Daily Nation, upande wa mashtaka ulitaka kupewa muda kujadiliana jinsi ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya wenzake kutoka Kenya.

Alikuwa akikabiliwa na matatizo yasio ya kawaida, ambapo aliamini watu wote karibu naye walikuwa na nia za kishetani'', daktari Mucheru Wang'ombe aliandika katika ripoti yake.