Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mahakama kutoa uamuzi kuhusu wapenzi wa jinsia moja Kenya: Je ni changamoto gani wanazopitia?
''Siku niliwaambia wazazi wangu kwamba mimi ni mpenzi wa jinsia moja, walinitenga, walinifukuza katika nyumba yetu na kuamua kutowasiliana na mimi'' , anasema Alex ambaye sio jina lake kamili, na ambaye anaishi jijini Nairobi. Huo ulikuwa mwanzo wa matatizo yangu''.
Nilitafuta mahali pa kuishi
"Sikuwa na mahali pa kwenda. Nilihisi maumivu moyoni mwangu''.
''Baadhi ya marafiki zangu walitaka kunisaidia lakini hawakuweza baada ya familia zao kukataa. Wengine wachache walitaka kunisaidia lakini kwa lengo la kujamiana nami''.
Lakini Alex ambaye anajitambulisha kuwa mwanamke mwanamume alisaidiwa na mpenzi wake wa kiume ambaye alikuwa na uhusiano naye wakati huo.
Mimi hubaguliwa katika maeneo ya umma .
''Wengi hawataki kunihudumia katika migahawa. Watu wananitenga katika maeneo ya umma''.
Lakini kama wanachama wengine wa wapenzi wa jinsia moja, Alex anasubiri kwa mahakama kuu kutoa uamuzi kuhusu sheria ya kikoloni inayowakandamiza wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya.
Uonevu
Mitazamo ya unyanyasaji ipo nchini Kenya. Ni vigumu kwa watu kama Alex kuendelea na maisha yao ya kawaida.
Alinyanyaswa akiwa shule na anaendelea kutengwa na jamii.
"Mimi na mpenzi wangu tulifurushwa na mwenye nyumba wetu wakati alipogundua kuhusu mwelekeo wetu wa kijinsia''.
Huku wanaharakati wakishinikiza kuhalalisha mapenzi ya jinsia moja, makundi ya kidini ikiwemo yale ya Kikristo na Kiislamu yamekuwa yakipinga mabadiliko hayo.
Baadhi ya wapinzani hao wanadai kwamba ni kinyume na utamaduni wa Kiafrika. Wanasema kuwa makabila mengi ya Afrika hayana neno la kutaja wapenzi wa jinsia moja.
Wamekataa kukubali
Alex sasa analifanyia kazi kundi moja la kampeni. Anasema kuwa tabia zimeanza kubadilika.
"Nina dada zungu wawili na ndugu mmmoja wa kiume. Wanazungumza na mimi mara kwa mara. Dada zangu walitaka kuleta amani kati yangu na wazazi wangu , lakini wakihofia chuki kutoka kwa majirani na watu wa familia , wazazi wangu walikataa kunikubali''.
''Siwachukii nawataka wanikubali siku moja''.
Familia imenikataa
Anatamani kujiunga na familia yake ili kusherehekea siku kuu kama ile ya Krisimasi. Tunaishi nje ya familia yetu. Tunataka kuishi ndani ya familia. Natumai kwamba uamuzi mzuri utatolewa ili kubadili tabia miongoni mwetu.
Mwanaharakati wa kupigania haki za kibinaadamu Kawira Mwirishia hajawai kunyanyaswa . Yeye anasema kuwa wazazi wake walikubali hali yake na kumtia moyo.
''Sidhani kwamba jamii kwa jumla wanapinga wapenzi wa jinsia moja. Rais wetu anasema hili sio tatizo. lakini mara kwa mara viongozi wanaowakilisha wahafidhina wanajitokeza na kutoa vitisho''.
Hofu ya Ubakaji
Lakini amepata hadithi nyingi za kuumiza kutoka kwa marafiki zake
''Ninawajua watu ambao wamebakwa''
Ni tukio ambalo wapenzi wa jinsia moja wa kike hubakwa na wanaume ili 'kuwatibu' ,mwelekeo wao wa kijinsia.
Neno "corrective rape" liligonga vichwa vya habari duniani 2008 wakati Eudy Simelane, mchezaji wa soka wa zamnai nchini Afrika Kusini alibakwa na genege la watu , kupigwa na kudungwa kisu hadi kufariki.
Wanawake waliobakwa huteseka kimya kimya kwa kuwa iwapo watakwenda kwa maafisa wa polisi wanahofia kukamatwa.
Iwapo watabadili sheria hiyo dhidi ya wapenzi wa jinsia moja hali itaimarika
Hukumu jela
Chini ya sheria, mtu atakayepatikana na hatia ya kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja atahukumiwa kifungo cha miaka 14 jela .
Lakini kama wanaharakati wa kibinaadamu wanavyosema sheria hiyo haijawahi kutumika.
''Ni watu wawili pekee walioshtakiwa katika kipindi cha miaka 10'', alisema Neela Ghoshal kutoka kundi moja la wanaharakati.
Lakini makundi ya LGBT hukumbwa na unayanyasaji kutoka kwa maafisa wa polisi na makundi mengine. Unayanyasaji dhidi ya wapenzi wa jinsia moja hufanyika sana mjini badala ya vijijini.
Tume ya wapenzi wa jinsia moja pekee imetoa usaidizi kwa takriban watu 1500 tangu 2014.
Hofu dhidi ya ghasia imewashinikiza wapenzi wengi wa jinsia moja kutoroka taifa hilo na kutafuta uhifadhi katika mataifa ya magharibi , kama vile Kenneth Macharia ambaye ametafuta hifadhi nchini Uingereza.
Kwa sasa anaichezea klabu ya raga inayowakumbatia wapenzi wa jinsia moja Bristol Bisons.
Hukumu ya kifo
Katika maeneo ya taifa la Somalia , taifa linalogawana mpaka na Kenya , wapenzi wa jinsia moja huuwawa.
Nigeria, Sudan na Mauritania pia hutoa hukumu kama hiyo. Mataifa 34 kati ya 54 ya bara Afrika hutoa hukumu ya jela kwa wapenzi wa jinsia moja.
Duniani mataifa 70 nusu yao yale yaliotawaliwa na Uingereza yanamiliki sheria dhidi ya wapenzi wa jinsia moja.
Nchini Kenya wapenzi wa jinsia moja wameamua kuwa wazi kuhusu mwelekeko wao wa kijinsia .
Lakini tishio la kupigwa bado wanaendelea kuwa nalo.
Vijana
''Mimi hufikiria jinsi ninavyovaa na kile ninachofanya. Kile ambacho mtu angefikiria kunihusu. Sijui ni nani nitakutana naye'', alisema Tumaini ambaye hakutaka kutumia jina lake sahihi.
'' Watu hunong'ona nyuma yangu . Na iwapo ni rafiki yangu tutajadiliana. Iwapo ni mtu nisiyemjua nitaondoka haraka iwezekanavyo''.
Anasema kuwa baadhi ya marafiki na watu wa familia yake walimtenga walipogundua kwamba anashiriki mapenzi ya jinsia moja.