Uchaguzi Afrika Kusini: Mtihani mkubwa kwa ANC miaka 25 baada ya utawala wa ubaguzi

Chanzo cha picha, RAJESH JANTILAL
Hasira kuhusu rushwa, kutetereka kwa uchumi na mageuzi kuhusu sera za umiliki wa ardhi ni masuala muhimu wakati raia Afrika kusini wanapiga kura katika uchaguzi wa sita mkuu kuwahi kufanyika tangu kumalizika kwa utawala wa ubaguzi wa rangi miaka 25 iliyopita.
Vijana waliounga mistari kupiga kura wamekuwa wakizungumzia matatizo ya kupata ajira, huku takwimu zikionyesha kwamba ukosefu wa ajira umefika 27%.
Chama tawala cha African National Congress (ANC), kilichoongoza vita hivyo dhidi ya ubaguzi wa rangi, kimekiongoza nchi tangu 1994.
Lakini ufuasi wake umefifia kutokana na kuendelea kuwepo ukosefu wa usawa.
Chama kikuu cha upinzani chenye msimamo wa kati Democratic Alliance (DA) na cha mrengo wa shoto Economic Freedom Fighters (EFF) ndio wapinzani wakuu.
Nasherehekea kwamba nchi yetu sasa inaongozwa na mtu mweusi "
"Mimi ni mfuasi wa chama cha ANC lakini sikuwapigia kura mara hii," mjenzi Thabo Makhene ameliambia shirika la habari la Reuters. "Wanastahili kuzinduka. Namna wanavyoliendesha taifa, kutumia vibaya fedha za umma, wamepotea maadili yao."
Esau Zwane, 90, anayesubiri kupiga kura Soweto, Johannesburg, aliishi katika utawala wa ubaguzi wa rangi. Alikuwa anasherehekea "kwamba nchi yetu sasa intawaliwa na mtu mweusi," ameiambia BBC.
Kukabiliana na ukosefu wa usawa
Utawala wa ubaguzi wa rangi, uliokuwepo tangu 1948 hadi 1994, ulihalalisha ubaguzi wa rangi na kuwapendelea watu weupe au wazungu na suala la ardhi limesalia kuwa tete.
Idadi ndogo ya wazungu wanaendelea kumiliki ardhi zaidi kuliko idadi kubwa ya raia weusi nchini. Chama cha EFF kimeongoza katika kujaribu kulibadili hili.

Chanzo cha picha, Reuters
Mwandishi wa BBC Andrew Harding mjini Johannesburg anasema msimamo wa chama umelazimu ANC kufikiria kuchukua hatua kali kukabidhi ardhi zaidi kwa haraka mikononi mwa raia weusi, jambo lililochangia chama hicho kutoa ahadi ya kuichukua ardhi kutoka kwa watu weupe pasi kuwapa fidia.

Viongozi wa chama:

Chanzo cha picha, EPA

Wakati huo huo chama kikuu cha upinzani, DA, kinasema hakiamini kwamba mageuzi katika suala la ardhi linahitaji "kutekelezwa katika namna ya kumpokonya mmoja ili kumpa mwingine", na badala yake ni kuahidi kutilia uzito mageuzi ya ardhi katika bajeti na kuitoa ardhi ambayo haijatumika ya serikali.
Masula mengine katika uchaguzi huu ni pamoja na kutoridhishwa na huduma muhimu zilizo duni kama maji, nyumba na umeme na hasira kutokana na kuongezeka kwa uhalifu wa mabavu.

Masuala muhimu:

Chanzo cha picha, EPA

Masuala matatu makuu wakati ANC kiking'ang'ania kubakia madarakani ni:
- Rushwa
- Kutetereka kwa uchumi
- Mageuzi ya sera ya ardhi
Zaidi ya watu milioni 26 wamejisajili kupiga kura - lakini utafiti wa kutafuta maoni unaashiria kwamba vijana milioni 6 hawako kwenye daftari ya wapiga kura.
Kura hiyo ya kutafuta maoni pia inaashiria kwamba ANC kitapata zaidi kidogo ya 50% ya kura huku DA kikitabiriwa kupata 20%, linaripoti shirika la habari la AFP.
Iwapo hayo yatakuwa ya kweli ina maana kwamba ugavi wa kura ya ANC umepungua. Kilijizolea 62% katika uchaguzi wa mnamo 2014.
Uchaguzi Mkuu 2019
26.76 Milioni Idadi ya wapiga kura
28,757Vituo vya kupigia kura
220,000Maafisa wanaosimamia uchaguzi

Takwimu katika uchaguzi mkuu Afrika kusini:
- Watu milioni 26.76 wamesajiliwa kupiga kura
- 55% kati yao ni wanawake
- Vyama 48 vipo kwenye debe
- Kuna vituo 28,757 vya kupiga kura
- Wafanyakazi 220,000 wa tume ya uchaguzi
- Vijana milioni 6 hawakujisajili kupiga kura


Chanzo cha picha, Reuters
Kando na kuendelea kutokuwepo usawa, inadhaniwa kwamba kushindwa kukabiliana na rushwa kumeathiri sifa ya ANC.
Rais Cyril Ramaphosa aliingia madakarakani mwaka jana akiahidi kukabiliana na suala hilo. Lakini kwa baadhi kukipigia kura ANC huku Ramaphosa akiwa kiongozi wa chama hicho ni kushinikiza enzi ya ufisadi katika chama hicho.
Vituo vya kupiga kura vitafungwa mwendo wa saa tatu usiku saa za huko sawa na 19:00 GMT lakini kwa watakaokuwa ndani ya vituo kabla ya muda wa kufungwa, wataruhusiwa kupiga kura yao.
Wapiga kura watawachagua wabunge kutoka orodha ya chama alafu wabunge wateuliwa watamchangua rais punde bunge litakapoanza vikao.
















