Mt Kilimanjaro: Tanzania kuanzisha usafiri wa angani katika mlima huo - Ni usafiri gani huo?

Tanzania inataka kuongeza idadi yake ya watalii kupitia magari ya kutumia nyaya katika mlima Kilimanjaro , ambao ndio mrefu zaidi barani Afrika na tayari imeanza mazungumzo na kampuni moja ya China na nyengine ya magharibi.
Takriban watalii 50,000 hupanda mlima Kilimanjaro kila mwaka.
''Gari la kutumia nyaya linaweza kuongeza idadi ya watalii kwa asilimia 50 kupitia kuwawezesha wale wasioweza kupanda mlima huo kwa miguu'' , alisema Constantine kanyasu , naibu waziri wa Utalii nchini humo.
''Kwa sasa taifa hilo linafanya utafiti kuhusu njia salama zitakazotumiwa na magari hayo'', Kanyasu aliambia chombo cha habari cha Reuters.
''Kwa sasa tunafanya utafiti ili kuona iwapo mradi huu tafanya kazi'' , alisema.

Kuna kampuni mbili moja kutoka China na nynegine kutoka mataifa ya magharibi ambazo zimeonyesha hamu.
''Hii haitakuwa mara ya kwanza duniani, magari ya kutumia nyaya yapo Sweden, Itali na Himalayas'', alisema.
Kanyasu aliongezea kuwa serikali ilikuwa inatazama mipango ya kibiashara , wawekezaji na faida yake.
Urefu wa njia hizo haujajulikana , huku kukiwa na mapendekezo kulingana na gharama na maswala ya kiuhandisi, alisema waziri huyo. Tathmini ya athari za mazingira itafanywa , alisema.
Pingamizi
Wachukuzi wa mizigo na wale wanaowaelekeza watalii katika mlima huo hatahivyo wanaupinga mradi huo kwa kuwa wanahofia utapunguza idadi ya watalii wanaopanda mlima huo.

Loishiye Mollel, ambaye ni kiongozi wa shirika la wachukuzi wa mizigo, amesema kuwa wageni hutumia wiki moja kupanda mlima huo.
''Mgeni mmoja kutoka Marekani anaweza kuandamana na takriban watu 15 nyuma yake , huku watu 13 wakiwa wachukuzi, mpishi na mwelekezi . Kazi zote hizo zitaathiriwa na magari ya nyaya'', alisema.
'Tunapendekeza kwamba mlima huu uwachwe vile ulivyo''.
Kuna takriban wachukuzi 20,000 wanaofanya kazi kati ya mlima Kilimajaro na ule wa Meru , ambao ni mlima mwengine uliopo karibu, alisema.
Mapato ya Tanzania kupitia Utalii

Mapato ya Tanzania kutokana na utalii yaliongezeka kutoka asilimia 7.13 mwaka uliopita, ukisaidiwa na kuwasili kwa wageni kutoka ng'ambo.
Mpato ya Utalii yaliongezeka hadi $2.43b mwaka uliopita kutoka $2.19b mwaka 2017.
Utalii ndio chanzo kikuu cha fedha za kigeni nchini Tanzania, kutokana na fukwe nzuri za bahari, safari za kutazama wanyama pori na Mlima Kilimanjaro ambao una urefu wa mita 5000 kutoka shina lake.
Mombasa Kenya
Hatua hiyo inajiri baada ya taifa jirani la Kenya pia kupendekeza kuanzisha huduma kama hiyo katika kivuko cha likoni kaunti ya Mombasa.
Mwaka uliopita Mkurugenzi mkuu wa shirika la feri nchini kenya Bakari Gowa alielezea kwamba tayari magari hayo yameanza kutengenezwa.
``Itachukua kama mwaka mmoja hivi magari hayo kutengenezwa kisha yataletwa Kenya mwaka ujao yaanze kazi ya kubeba watu angani kuwavukisha katika kivuko cha Likoni,'' anasema Gowa.
Je, magari haya ya nyaya yatasafirisha watu vipi?
Magari haya yatakuwa juu ya hewa yakitumia umeme. Nyaya hutumiwa kuyavuta au kuyashusha kwa utulivu.
'Cable cars' - kama yanavyofahamika hayatumii injini na badala yake huvutwa kwa nyaya inayozungushwa kwa mota.













