Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mfahamu kiongozi wa upinzani Afrika Kusini anayeandamwa na kivuli cha Mandela
Mmusi Maimane ndiye kiongozi wa kambi ya upinzani nchini Afrika Kusini.
Yeye ndiye kinara katika wa upinzani katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo ambao wachambuzi wanauita ni harakati ngumu za kutaka kumng'oa rais Cyrill Ramaphosa madarakani.
Japo utawala wa kibaguzi ulikomeshwa rasmi Afrika ya Kusini mwaka 1994, mfumo wa vyama vya siasa kwa kiasi kikubwa, mifumo ya vyama vya siasa nchini humo imejengeka kulingana na rangi za raia wake.
Chama tawala nchini humo, Africa National Congress (ANC) ndicho kilipambana dhidi ya utawala wa kibaguzi chini ya uongozi wa Nelson Madela. Kutokana na hilo, kinaungwa mkono zaidi na watu weusi.
Chama Kikuu cha upinzani, Democratic Alliance (DA) kinaungwa mkono kwa kiasi kikubwa na wazungu ambao ni raia wa nchi hiyo.
DA hata hivyo kipo chini ya kiongozi kijana mwenye miaka 38, tena kwa rangi ni mweusi. Si mwengine, ni Bw Maimane.
'Kibaraka wa Wazungu'
Maimane alijiunga na siasa kupitia chama cha DA mwaka 2011, na baada ya miaka minne, akaukwaa uongozi mkuu wa chama hicho.
Mafanikia hayo hayakuja pasi na purukushani, nje na ndani ya chama.
Ndani ya DA, wapo waliokosoa kuwa, kijana huyo (wa miaka 34 kipindi hicho) hakuwa na uzoefu ama weledi wa kutosha kukiongoza chama.
Nje ya DA, hasa machoni mwa wanavhama na viongozi wa ANC, hatua hiyo ilionekana kama kumsimika 'kibaraka wa wazungu' kwenye uongozi wa chama chao.
Dhana ya 'vibaraka wa wazungu' si ya leo. Iliasisiwa na Mandela mwenyewe. Miaka 19 iliyopita, mzee Mandela alikibeza chama cha DA kuwa: "nyumba ya mabwana wa kizungu na vibaraka wao weusi."
Toka wakati huo mpaka hii leo, chama cha DA kimekuwa kikihangaika kujinasua kutoka kwenye kitanzi hicho walichovikwa na Mandela.
Maimane ndiye kiongozi wa kwanza mweusi wa chama hicho ambacho kiliasisiwa na wwazungu waliberali katika kipindi cha utawala wa kibaguzi.
Ni dhahiri kuwa, kuchaguliwa kwa Maimane kukiongoza DA imekuwa ni moja ya mbinu za chama hicho kuonekana ni cha wote na si kundi fulani ama rangi fulani.
"Uweledi wa kiuongozi si jambo la uzoefu tu," ameiambia BBC na kuongeza, "Je, nimekuwa kisiasa toka nilipopata cheo hicho? Jawabu ni ndio."
Na hivi karibuni aliwaambia wapinzani wake ndani na nje ya chama hicho 'wafunge midomo yao' kwa kumkosoa kuwa yeye ni kibaraka ama hana uzoefu wa kutosha.
Mambo saba kuhusu Mmusi Maimane
- Alizaliwa mwaka 1980 kitongoji cha Soweto, Johannesburg ambapo Nelson Mandela aliishi kwa miaka mingi.
- Amesoma vyuo vikuu nchini Afrika Kusini na Wales, ana Shahada ya Uzamivu katika masomo ya Teolojia na Saikolojia.
- Ameoa mwanamke wa kizungu Natalie, ambaye walikutana kanisani, na kukiri kuwa ilimchukua muda kukubaliana na jamii inavyochukulia tofauti yao.
- Anaongea lugha sita.
- Amekuwa akihubiri kanisani jijini Johannesburg mwishoni mwa wiki kwa miaka kadhaa sasa.
- Alikuwa mshauri wa kibiashara kabla ya kuingia kwenye siasa, na kuwa msemaji wa DA mwaka 2011.
- Alichaguliwa kuwa kiongozi wa kwanza mweusi wa DA mwaka 2015 akiwa na miaka 34.
'Mapambano ya kihistoria'
"Usipoteze kura yako tena kwa mtu mweupe," katibu mkuu wa ANC hivi karibuni amewaambia wapiga kura kwenye kampeni, akikilenga chama cha DA.
Maafisa wa ANC, na wale wa chama kidogo lakini chenye msimamo mkali cha Economic Freedom Fighters (EFF), kinachoongozwa na Julius Malema, wanakishambulia wazi wazi chama cha DA kuwa si upinzani bali watumishi wa "mabepari weupe," na Bw Maimane kuwa ni "mfanyakazi wa bustani" anayelinda maslahi ya wazungu wachache.
Mwaka 2005, Maimane alifunga ndoa na mwanamke wa Kizungu ambaye alikutana naye kanisani miaka kadhaa nyuma. Wana watoto wawili, wakike na wakiume.
Kwa sasa Maimane anasema harakati dhidi ya ubaguzi nchini humo ni "mapambano yake ya kihistoria."
"Bizo ndizo harakati zinazotawala Maisha yangu na nitazipambania mpaka siku nakufa," ameiambia BBC.
Lakini mapambano hayo ya Maimane si kwa vyama pinzani tu, bali hata ndani ya DA.
"Chama cha DA kililazimika kubadilika. Inabidi tuendelee kukibadilisha chama," amesema Maimane.
Je anafanikiwa katika hilo?
Wakosoaji wake wanasema uthabiti wa chama hicho umejengeka katika misingi yake ya kupambana kisera na utawala bora. Na kwakuwa Maimane aliingia uongozini akiwa hana uzoefu wowote, hivyo hana mchango mkubwa katika kukiimbarisha chama.
Lakini kwa Maimane na wafuasi wake, wanasisitiza kuwa chini ya uongozi wake, chama hicho kimetanuka na kupenya katika maeneo na "jamii ambazo isingeweza kuzifikia hapo kabla."
Kujikita katika siasa za uchumi
Siku chache zijazo zitaamua mustakabali wa Maimane kisiasa.
Mapambano makali zaidi yapo kwenye jimbo Tajiri zaidi nchini humo la Gauteng.
Chama cha DA ambacho tayari kinalishikilia jimbo la Western Cape, endapo kitaweza kuwashusha ANC mapaka chini ya 50% jimboni Gauteng, basi wataweza kuingia kwenye serikali ya mpito ya jimbo hilo.
Ingawa kwa mwaka huu kura zote za maoni zinaonesha kuwa ANC watashinda uchaguzi, mchuoano wa Gauteng unatazamiwa kuamua uchaguzi wa kitaifa wa mwaka 2024.
Katika miaka ya mwisho ya utawala wa rais aliyejiuzulu Jacob Zuma, chama cha ANC kilipoteza Imani miongoni mwa raia wengi wa nchi hiyo kutokana na kushamiri kwa kashfa za rushwa na ufisadi.
Japo kwa sasa chama hicho kimeanza kurejesha Imani polepole chini ya rais Ramaphosa.
Hata hivyo, Muimane anaamini ANC haiwezi kubadilika na imevunjika vipande vipande ambavyo haviwezi kuungika tena na kuwa kitu kimoja.
Lakini pia nafahamu fika kuwa ni mapambano makli zaidi kuwaaminisha waliowengi nchini Afrika Kusini kuwa yeye na chama chake cha DA ndiyo mbadala na jibu kwa matatizo ya nchi.
"Ninawaasa na kuwaomba Waafrika Kusini kuwezesha siasa za mrengo wa kati (chama cha DA) kushinda. Mabadiliko huwa hayapendezi sana mwanzoni, lakini tunayahitaji," amesema Maimane.