Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Koffi Olomidé: Nyota wa muziki Congo ahukumiwa Ufaransa kwa kupatikana na hatia ya ubakaji wa mtoto wa miaka 15
Koffi Olomidé, mojawapo ya nyota wa muziki Afrika , amepatikana na hatia kwa ubakaji wa mojawapo ya wanengeuaji wake alipokuwa miaka 15.
Amehukumiwa miaka miwili gerezani na mahakama ya Ufaransa akiwa hayupo, baada ya kukosa kufika mahakamani.
Uamuzi huo una maana kwamba nyota huyo wa Congo atakamatwa iwapo atatekeleza uhalifu mwingine, anasema mwandishi wa BBC Nadir Djennad.
Olomidé, mwenye umri wa miaka 62, aliagizwa alipe Euro 5,000 kwa madhara aliyomsababishia mnenguaje wake huyo wa zamani.
Mahakama ya Nanterre, nje ya mji mkuu Paris, pia ilimuagiza alipe faini ya kiwango sawa kwa kuwasaidia wanawake watatu wengine kuingia nchini Ufaransa kwa njia haramu.
Wakili wa Olomidé amepongeza uamuzi huo na kuutaja kuwa ushindi, akiwarifu waandishi habari kwamba uamuzi huo utachangia kuondolewa waranti wa kimataifa wa kumkamata.
Koffi Olomidé ni nyota wa muziki wa mtindo wa rumba na soukous ambao ni maarufu sana barani Afrika.
Olomidé alishtakiwa mara ya kwanza mnamo 2012 kwa ubakaji wa kimabavu lakini mashtaka yakapunguzwa.
Wanenguaji wanne waliokuwa wakimfanyia kazi wameiambia mahakama kwamba aliwanyanyasa kingono mara kadhaa kati ya mwaka 2002 na mwaka 2006. Wameeleza kuwa unyanyasaji huo ulifanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Ufaransa.
Wanawake hao pia walieleza kwamba walizuia kwa lazima katika nyumba moja nje ya mji wa Paris na walifanikiwa kutoroka usiku wa Juni 2006, lakini hawakurudi DR Congo kutokana na kuogopa kutafutwa na kulipizwa kisasi.
Waendesha mashtaka walikuwa wakishinikiza ahukumiwe miaka 7 gerezani lakini mahakama imetupilia mbali mashtaka ya unyanyasaji na madai ya utekaji nyara.
Olomidé alikimbilia Congo mnamo 2009 akiahidi kujitetea lakini alikosa kufika mahakamani Ufaransa katika kesi hiyo ambayo kutokana na ombi la walalamishi ilifanyika faraghani.
Muimbaji huyo ambaye jina lake halisi ni Antoine Agbepa Mumba, amejipata mashakani na sheria kwa mara kadhaa:
- 2018 Zambia iliagiza akamatwe baada ya kutuhumiwa kumshambulia mpiga picha
- 2016 alikamatwa na kutimuliwa baada ya kumshambulia mojawapo ya wanenguaji wake Kenya
- 2012 alishtakiwa DR Congo kwa kumshambulia produza wake na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitatu ambacho angefungwa iwapo angetekeleza uhalifu mwingine
- 2008 alishutumiwa kumpiga teke mpiga picha katika kituo cha Televisheni DR Congo RTGA na kuivunja kamera yake katika tamasha , lakini walipatanishwa baadaye.