Rufaa ya Mkurugenzi wa mashitaka dhidi ya Mbowe, Matiko yatupiliwa mbali

Chanzo cha picha, chadema
Mahakama ya Rufani Tanzania, imetupilia mbali rufaa iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.
Aidha, mahakama hiyo imeelekeza jalada la kesi hiyo kurudishwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusikiliza rufaa iliyokatwa na wawili hao kupinga kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Novemba 23, mwaka jana.
Uamuzi huo uliandaliwa na jopo la Majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti wao, Jaji Stella Mgasha, Mwanaisha Kwariko na Gerald Ndika baada ya kusikiliza hoja za upande wa mashitaka na upande wa utetezi zilizowasilishwa Februari 18, mwaka huu.
Katika rufaa hiyo, upande wa mashitaka uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Paul Kadushi na Mawakili wa Serikali, Samon, Salum Msemo ambao waliwasilisha hoja tatu za kupinga uwepo wa rufaa Mahakama Kuu ikiwemo Jaji kukosea kupanga kusikilizwa kwa rufaa kinyume na kifungu cha 362 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Tanzania: Viongozi wa Chadema wasomewa mashtaka Pia walidai kuwa mahakama haikuwapa haki ya kusikilizwa waomba rufaa na kwamba Jaji alisukumwa na hali ya upendeleo hoja ambayo waliiondoa wakati wa usikilizaji wa rufaa. Akisoma hukumu hiyo, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Sylvester Kainda alisema kuwa rufaa ya DPP haina mashiko kuwepo mahakamani hapo kwa sababu haikuwa sahihi kwake kupeleka mapingamizi huku ikijua alichokuwa anakipinga mahakama kuu ilipewa mamlaka. ''Haikuwa sahihi kwa DPP kuleta mapingamizi haya wakati wanajua mamlaka ambayo Mahakama Kuu imepewa na hiki sio kitendo kizuri hivyo, rufaa hii haina msingi na jalada liendelee na usikilizaji Mahakama Kuu,'' alieleza Kainda.
Alisema ni kweli rufaa iliyokatwa na Mbowe na Matiko, ilikuwa chini ya hati ya dharura na kwamba kumbukumbu za mwenendo wa shauri hilo kutoka mahakama ya chini (Kisutu) hazikuwa zimeambatanishwa.

Chanzo cha picha, CHADEMA
Sababu ya rufaa ya DPP
Sababu za DPP kukata rufaa hiyo ilitokana na Novemba 23, 2018 wajibu maombi (Mbowe na Matiko) kupinga uamuzi wa kufutiwa dhamana mahakama ya Kisutu na siku iliyofuata upande wa utetezi ukiongozwa na Kibatala walikata rufaa kupinga maamuzi hayo.Novemba 27, mwaka jana, Jaji Rumanyika aliona kuwa rufaa hiyo imepelekwa chini ya hati ya dharura hivyo aliagiza mwenendo wa shauri upelekwe mahakamani hapo pamoja na wahusika wapande zote wafike.
Pia walidai mahakama imekosea kuwafutia dhamana kwa sababu Novemba 12, mwaka huu Mbowe na Matiko walifika mahakamani bila kukamatwa na kuwa chini ya ulinzi.

Chanzo cha picha, CHADEMA
Hata hivyo, Novemba 28, upande wa mashitaka na wa utetezi walifika mahakamani hapo na mapingamizi ya pande zote yalisikilizwa ikiwemo sababu nne za Mbowe na Matiko za kupinga uamuzi huo kwamba mahakama haijawapa nafasi wadhamini ya kujieleza kwa mujibu wa sheria.Alidai masharti ya dhamana waliyopewa washitakiwa ni kinyume na sheria. Hata hivyo, upande wa mashitaka uliomba mahakama hiyo itupilie mbali rufaa hiyo kwa sababu tatu ikiwemo warufani kushindwa kukata rufaa kupinga dhamana iliyotolewa na mahakama ya Kisutu na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza rufaa kwani taarifa ya kusudio la kukata rufaa imekosekana. Kainda alisema Jaji Sam Rumanyika wa Mahakama Kuu alitimiza matakwa ya kisheria na si vinginevyo kwa kuelekeza mwenendo wa kesi ulioandikwa kwa mkono pande zote zipewe na kwa pamoja walikubaliana zitumike.
Alisisitiza kuwa inaelekeza kwamba mwenendo wa kesi uambatanishwe na rufaa husika lakini kama sivyo, Jaji amepewa mamlaka ya kuelekeza vinginenvyo. ''Hatuwezi kupingana na Jaji kwa uamuzi aliochukua wa kujulisha pande zote tarehe ya kusikilizwa kwa kesi hiyo na baada ya kubaini kuwa pande zote hazikuwa na mwenendo wa kesi hiyo aliagiza mwenendo huo wapewe pande zote,'' alisema Kainda.












