Ukeketaji ni nini, na kwanini unaendelea licha ya kukatazwa katika mataifa mengi duniani?

Mmoja kati ya wasichana 20 wamefanyiwa ukeketaji wa sehemu zao za siri kulingana na takwimu kutoka kwa Umoja wa mataifa UN.

Hiyo inamaanisha kwamba jumla ya wanawake milioni 200 kutoka duniani walio hai leo, wote au baadhi yao wamekatwa, kubadilishwa ama hata kuondolewa sehemu zao za siri.

Umoja wa mataifa umetoa wito wa kusitishwa kwa kitendo hicho katika siku ya kimataifa tarehe 6 mwezi Februari. Wanawake na wasichana hukeketwa wakiwa wadogo- mara nyengine hata watoto ama baadaye katika maisha yao wanapo baleghe.

Ukeketaji unasababisha matatizo ya kimaungo pamoja na yale ya kiakili ambayo baadaye humuathiri mwanamke katika kipindi cha maisha yake yote kilichosalia.

'Nilifanyiwa ukeketaji wakati nilipokuwa na miaka 11' anasema Bishara Sheikh Hamo kutoka Afrika. 'Niliambiwa na nyanyangu kwamba ukeketaji ni mojawapo ya mahitaji ya kila msichana'.

Lakini kile ambacho Bishara hakuambiwa ni kwamba kitendo hicho kitamuacha kuwa na hedhi zisizo za kawaida pamoja na matatizo ya kibofu cha mkojo katika maisha yake yote, maambukizi ya mara kwa mara na wakati ulipojiri, ingebidi ajifungue kupitia njia ya upasuaji.

Kwa sasa yeye ni mwanaharakati dhidi ya ukeketaji.

Je Ukeketaji ni nini?

Ukeketaji ni ukataji wa sehemu za siri za mwanamke.

Ukataji huo unahusisha maeneo nyeti, na shirikisho la afya duniani linauelezea kuwa ''kitendo chochote kinachojeruhi uke kutokana na sababu ambazo sio za kimatibabu''.

Ukeketaji unaumiza wanawake na wasichana kimaungo na kiakili na hakuna faida yoyote ya kitabibu wakati wa kitendo hicho.

Inachangia huzuni na inaharibu uhusiano wa wanawake na vile wanavyojihisi. Hufanyika kinyume na matakwa ya wanawake ama hufanywa kwa lazima.

Bishara ameambia BBC vile alivyokeketwa pamoja na wasichana wengine wanne: 'Nilifunikwa uso. halafu akanifunga mikono yangu nyuma. Miguu yangu ilitawanywa wazi na baadaye kunikata sehemu yangu ya uke. Baada ya dakika chache, nilihisi uchungu mkali. nilipiga kelele lakini hakuna mtu angenisikia'.

'Nilijaribu kupigania uhuru wangu, lakini kuna kitu kilinizuia mguu wangu'.

Anasema kilikuwa kitendo kibaya. 'Ni mojawapo ya kitendo kibaya na kichafu. Walitumia kisu hicho hicho kwetu sote. Dawa iliokuwepo ya kuondoa uchungu huo ilikuwa ile ya kienyeji ya miti shamba'.

'Kulikuwa na shimo ardhini na dawa ya miti shamba katika shimo hilo. Baadaye walinifunga miguu kama mbuzi na kunipaka dawa hiyo'.

'Baadaye walimuita msichana mwengine'.

Ijapokuwa ukeketaji ni haramu katika mataifa mengi, bado hufanyika katika baadhi ya sehemu Afrika, Asia na eneo la Mashariki ya kati - na kwengineko duniani katika jamii kutoka nchi ambako ukeketaji ni kawaida.

Kuna aina nne za ukeketaji

1: Clitoridectomy. Hii inahusisha kukatwa kwa kiasi fulani au kikamilifu kwa sehemu nyeti ya kisimi na ngozi inayoizunguka sehemu hiyo.

2: Excision . Kukatwa kwa kiasi fulani kisimi, pamoja na kuondoshwa kwa mdomo wa ndani wa uke au labia minora.

3: Infibulation. Kukatwa na kwa mdomo wa ndani na wa nje wa uke na kuushona upya na badala yake kuacha tundu ndogo tu.

Utamaduni huu unasababisha maumivu makubwa na kumfanya mkeketwa kutaabika pakubwa, lakini pia kuna hatari kubwa ya kupata maambukizi ya kuendelea: Kufungwa kwa uke na tundu ya mkojo, inawaacha wanawake na tundu ndogo ya kupitisha mkojo na damu ya hedhi.

Kwa hakika, mara nyingine tundu inayoachwa huwa ndogo mno kiasi cha kuhitaji kukatwa upya ili mwanamke aweze kushiriki tendo la ndoa , au wakati wa mama kujifunguwa mtoto.

Na mara nyingi husababisha matatizo yanayomdhuru mama na mwana.

4: Hii huangazia mbinu nyingine zote kama kudunga, kutoboa, kunyofoa kabisa na pia kuchoma kabisa kisimi au sehemu nyeti.

Kwanini linafanyika?

sababu kubwa zinazotajwa kwa ukeketaji ni , kukubalika katika jamii, dini, imani potofu kuhusu usafi wa mwili, mbinu ya kuhifadhi ubikira, kumfanya mwanamke aweze kuolewa, na kushinikiza hamu ya tendo la ndoa kwa wanaume.

katika baadih ya tamaduni, ukeketaji huonekana kama njia ya kuingia katika utu uzima na sharti la kuweza kuolewa.

Licha ya kwamba hakuna faida kwa usafi na afya ya mwili, jamii zinazokeketa zinaamini wanawake wanahitaji kukeketwa, na kwa ambao hawajaliptia hilo, wao huonekana kama wachafu, wasi na afya wala thamani.

Mara nyingi wanawake hukeketwa kwa lazima, na maafisa wa fya kote duniani wanamini ni aina ya unyanyasaji dhidi ya wanawake na ukiukaji w ahaki z abinaadamu na iwapo litatekelezwa kwa watoto basi huwa ni aina ya unyanyasaji wa watoto.

Ukeketaji unafanyika wapi?

Inakadiriwa kwamba ukeketaji unafanyika kotea Afrika, sehemu za eneo la Mashariki ya kati na pia Asia - lakni pia ndai ya baadhi ya jamii za wahamiaji Ulaya, Amerika kaskazin ina kusini na Australia.

Kwa mujibu wa ripoti ya Unicef iliyotokana na utafiti katika mataifa 29 barani Afrika na mashariki ya kati, ukeketaji bado unafanyika pakubwa, licha ya kwamba mataifa 24 kati yayaliojumuishwa yana sheria au sera dhidi ya ukeketaji.

katika baadih ya tamaduni ambako ukeketaji unafanyika, ni mwiko hata kulijadili suala hilo. kwa mara nyingine kutokana na hofu ya kushutumiwa na watu wa nje.

Au kwa mara nyingine - katika maeneo ambako ukeketaji ni marufuku - kwa hofu ya kushtakiwa kwa familia au watu katika jamii.