'Mashujaa' wa vita vya ukeketaji Tanzania

Mabinti wadogo wa umri mpaka miaka minane, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania wanaongoza operesheni dhidi ya ukeketaji kwenye jamii zao.

Sheria ya Tanzania ilieleza mwaka 1998 kuwa shughuli za ukeketaji ni uhalifu, hata hivyo vitendo hivyo bado vinafanyika kwa kiasi kikubwa nchini Tanzania.Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia idadi ya watu, mwanamke mmoja kati ya kumi wenye umri kati ya miaka 15-49 wamekeketwa.

Vitendo hivi ambavyo vinatishia maisha hufanyika kipindi cha mapumziko ya mwishoni mwa mwaka ambapo mamia ya wasichana hukeketwa na mara nyingi hufuatiwa na ndoa.

Vitendo hivi vinafanyika hasa kutokana na imani kuwa wasichana ni lazima kukatwa sehemu zao ili kupunguza vitendo vya uzinzi.Pia wasichana waliokeketwa hutolewa gharama ya mahari mara mbili zaidi ya wasiokeketwa.

Lakini jitihada za kumaliza ukeketaji nchini Tanzania zimeongezeka, waathirika wa ukeketaji wanaongoza vita dhidi ya vitendo hivi vilivyopitwa na wakati.

Wakitambua kuwa wazazi wao au walezi wanajiandaa kuwapeleka kukeketwa,wasichana hukimbia makazi yao kuepuka kuuzwa na kuingia kwenye ndoa za utotoni.

''Nilikimbia nyumbani kwasababu nilishapata elimu kuhusu ukeketaji lakini pia nilifahamu kuwa ukeketaji una madhara makubwa.Hivyo walipotaka kuipeleka kukatwa sikupenda.Nilijaribu kuwaeleza ni insi gani vitendo hivi vilivyo vibaya, hawakunisikiliza ndio maana nilikimbilia sehemu iliyo salama ambapo nitaweza kulindwa''Anaeleza Neema mwenye miaka 12.

Nyumba salama, tumaini kwa wasichana na wanawake', ambapo Neema na maelfu ya wasichana wengine waliokimbia nyumba zao na kuelekea hapo, inasimamiwa na mwanamke aitwaye Rhobi Samwelly. Wakati wa msimu wa kukatwa, Rhobi, akishirikiana na polisi na timu yake wanapambana na ukeketaji na wakati mwingine, huwaokoa wasichana na kuwakamata wazazi na mangariba.

''Kilichinivutia na kuanzisha nyumba hii ni kwa sababu nilitaka wasichana kulindwa.Wakati wa msimu wa kukatwa ambapo kunakuwa na harakati nyingi kwenye jamii, wasichana wanalazimishwa kukeketwa na hakuna wa kuwasaidia.Tumewaokoa wasichana wengi.Nilianza kufanya kazi kwenye nyumba salama moja iliyokuwa chini ya kanisa,na sasa tuna nyumba mbili na tumewaokoa wasichana zaidi ya 600, ambao walilindwa wasikeketwe''.Alisema Rhobi

Nyumba hizi zinatoa eliu bure kuhusu mafunzo ya ufundi, kama vile ushonaji na Kompyuta.Wasichana wanaweza kutumia ujuzi wao mpya kupata kipato na kusaidia familia zao, pia wakijiimarisha uwezo wao wa kujitegemea.

Baada ya msimu wa kukata kuisha hufanyika mkutano wa mapatano ambapo wazazi huamua kama watawachukua mabinti zao na kuhakikisha kuwa hawakeketwi, huku wasichana nao wakipata nafasi ya kueleza kama wanajisikia kuwa salama endapo watarejea nyumbani kwa wazazi wao

UNFPA imekuwa ikimsaidi Rhobi na timu yake kuwapatia washauri nasaha ambao wanaongeza uwezekano wa kuwashawishi wazazi kuachana na vitendo vya ukeketaji.

Baada ya uzoefu huu, wasichana wengi wataweza kuwaelimisha wazazi na walezi kuhusu madhara ya Ukeketaji, lakini pia wataweza kutembelea shule mbalimbali na jamii kutoa elimu na kufanya kampeni kumaliza vitendo vya ukeketaji.