Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wasichana 800 wakeketwa kaskazini mwa Tanzania
Wasichana zaidi ya 800 walikeketwa kaskazini mwa Tanzania mwezi uliopita, mkuu wa wilaya ya Tarime Glorious Luoga amesema.
Hilo lilifanyika ingawa polisi wamekuwa wakikabiliana na utamaduni huo.
Wanawake 12 wanaotuhumiwa kuhusika katika kuwakeketa wasichana hao wamekamatwa na maafisa wa polisi, mkuu huyo wa wilaya amesema.
"Operesheni ya polisi bado inaendelea. Hatutatulia hadi wote waliohusika wakamatwe na kushtakiwa," Luoga aliambia wanahabari.
Eneo la Tarime, wasichana hukeketwa wakiwa na umri wa kati ya miaka 12 na 17.
Inakadiriwa kwamba nchini Tanzania, wasichana na wanawake 7.9 milioni wamekeketwa.
Novemba, kabla ya kuanza kwa msimu wa ukeketaji Tarime, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Tarime, Thomas Mapuli alikuwa ametangaza kwamba polisi wamejiandaa kuwakamata mangariba wote ambao wangejaribu kukeketa watoto wa kike.
"Tumejipanga vizuri na hatutakuwa na huruma kwa atakayekutwa anatenda kosa la ukeketaji," alisema Bw Mapuli.
Wasichana takriban 140 milioni wamekeketwa maeneo ya Afrika, Mashariki ya Kati na Bara Asia.
Jamii zinazotekeleza utamaduni huu huutazama kama njia ya kuwatakasa wasichana na kuwaandaa kwa maisha ya ndoa.
Lakini utamaduni huo husababisha matatizo mengi ya kiafya.
Wengi hufariki wakikeketwa na baadaye wengi hukabiliwa na matatizo sana wanapojifungua.