Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
DR Congo: Watu 900 wameuawa katika vita vya kikabila mwezi uliopita UN unasema
Vita vya kikabila magharibi mwa Jmahuri ya Kidmeokrasi ya Congo vimesababisha vifo vya takriban watu 890 katika muda wa siku tatu mwezi uliopita, Umoja wa mataifa unasema.
"Duru za kuaminika" zinaeleza mapigano kati ya jamii za Banunu na Batende yalizuka katika vijiji vinne huko Yumbi, ofisi ya Umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadamu inasema.
Idadi kubwa ya wakaazi wa eneo hilo inaarifiwa wameachwa bila ya makaazi.
Uchaguzi mkuu wa Desemba 30 uliahirishwa huko Yumbi kutokana na ghasia.
Mashambulio hayo yanaarifiwa kutokea kuanzia Desemba 16 hadi 18.
Umoja wa mataifa unasema nini?
Nyumba 465 na majengo yaliteketezwa au kuharibiwa, zikiwemo shule mbili za msingi, kituo cha afya, soko na ofisi ya tume huru ya uchaguzi katika eneo hilo, Umoja huo umesema.
Raia walioachwa bila ya makaazi ni pamoja na watu 16,000 waliotafuta hifadhi kwa kuvuka mto Congo hadi katika nchi jirani ya Congo-Brazzaville, umeongeza.
"Ni muhimu kwamba ghasia hizi za kushtusha zichunguzwe kwa haraka na kwa kina na watuhumiwa wachukuliwe hatua za kisheria," amesema kamishna wa haki za binaadamu katika Umoja wa mataifa, Michelle Bachelet.
Takriban watu 82 walijeruhiwa katika shambulio hilo, kwa mujibu wa ripoti, lakini Umoja wa mataifa umesema unatarajia idadi ya walioathirika kuongezeka.
Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja huo imesema imeanzisha uchunguzi.
Yumbi, katika jimbo la Mai-Ndombe kwa kawaida ni eneo lenye amani, waandishi wanasema.
Ripoti zinaashiria mapigano yalizuka wakati watu wa kabila la Banunu walipojaribu kumzika mojawapo ya viongozi wao wa kitamaduni katika ardhi ya kabila la Batende.
Uchaguzi wa urais katika eneo hilo pamoja na katika maeneo ya Beni na Butembo mashariki mwa jimbo la Kivu kaskazini, uliahirishwa hadi Machi huku tume ya uchaguzi ikieleza ni kutokana na ukosefu wa usalama na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Taarifa za sasa ni zipi kuhusu uchaguzi huo uliokumbwa na mzozo?
Mgombea wa upinzani Felix Tshisekedi alitangazwa mshindi lakini mpinzani mwingine wa utawala wa sasa, Martin Fayulu, anasisitiza yeye ameshinda, na kutuhumu Tshisekedi wameingia katika makubaliano na rais anayeondoka Joseph Kabila.
Fayulu alikata rufaa katika mahakama ya katiba Jumamosi akitaka kura zihesabiwe upya kwa mkono.
Suala hilo litajadiliwa katika mikutano ya Umoja wa Afrika na SADC katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, leo Alhamisi, AFP linaripoti.
Kabila amehudumu kwa miaka 18 na matokeo, iwapo yatathibitishwa, yataidhinisha ukabidhi wa kwanza wa uongozi kwa mpangilio tangu taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji mnamo 1960.