Al-Shabab Somalia: Mashambulizi ya anga yaua wanamgambo 62, Marekani imeeleza

Al-Shabab mwaka 2012 (picha ya maktaba)

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Marekani imesema ina nia ya kuwadhibiti al-Shabab nchini Somalia

Jeshi la Marekani limesema limewaua wapiganaji 62 wa kundi la kiislamu la al-Shabab kwa mashambulizi sita ya anga nchini Somalia.

Mashambulizi manne yaliyotekelezwa siku ya Jumamosi yalisababisha vifo vya wanamgambo 32 na wengine 28 waliuawa wakati wa mashambulizi mawili ya anga, ilieleza taarifa hiyo

Haya ni mashambulizi makubwa kuwahi kutokea tangu mwezi Novemba mwaka 2017, pale Marekani ilipowaua wanamgambo 100

Kumekuwa na ongezeko la mashambulizi ya anga tangu Rais wa Marekani Donald Trump aingie madarakani mwezi Januari mwaka 2017

Mashambulizi ya hivi karibuni yaliyotekelezwa nchini Somalia yamefikia 40 mwaka huu, ukilinganisha na 35 yaliyorekodiwa mwaka 2017

Marekani ina kambi yake kubwa ya kijeshi katika nchi jirani ya Djibouti,ambako mashambulizi ya anga yanapotokea

Rais Trump alilipa mamlaka jeshi la Marekani mwezi Machi mwaka 2017 kushambulia wanamgambo nchini Somalia.

Hakuna raia waliopoteza maisha katika mashambulizi hayo ya anga yaliyotekelezwa kwa ushirikiano na serikali ya Somalia, jeshi la Marekani limeeleza.

Wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Al-Shabab

''Sambamba na washirika wetu Somalia na washirika wa kimataifa, tumejikita katika kuzuia al-Shabab kutumia fursa ya usalama uliopo kujenga uwezo na kushambulia raia wa Somalia'', uongozi wa jeshi hilo umeeleza

Al-Shabab, yenye uhusiano na al-Qaeda, hawajazungumza lolote kuhusu mashambulizi hayo ya karibuni.

Taasisi ya usalama ya Think tank imesema katika ripoti yake ya mwezi Novemba kuwa al-Shabab wamelazimika kubadili mbinu kutokana na mashambulizi ya anga yanayotekelezwa dhidi yao.

Taasisi hiyo imesema kundi hilo sasa inafanya mashambulizi kwenye maeneo ya kambi za kijeshi, lakini mashambulizi dhidi ya Ofisi za serikali na biashara yamekuwa yakiongezeka.

Marekani imesema wanamgambo hao wameendelea kuwa tishio, pamoja na kukabiliwa na majeshi ya Marekani na washirika wake

Bado wanamgambo hao wanashikilia maeneo makubwa ya Somalia, na bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi makubwa kwa kutumia watu wanaojitoa muhanga, vilipuzi,silaha nzito na ndogondogo, ripoti imeeleza.