Jeshi Tanzania laanza rasmi 'operesheni korosho'

JWTZ

Jeshi la Tanzania (JWTZ) hii leo limeanza rasmi operesheni ya kuratibu ununuzi, uhifadhi na usafirishaji wa zao la korosho kwa mikoa ya kusini mwa Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi aliwakabidhi JWTZ kiwanda cha kubangua korosho cha Bucco ambacho serikali ilikirudisha mikononi mwake wiki iliyopita baada ya mwekezaji kushindwa kukiendeleza kama ilivyotakiwa wakati wa ubinafsishwaji wake.

Kuanzia leo maghala yanayohifadhi zao hilo kwenye mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma yapo chini ya ulinzi wa wanajeshi. Na tayari malori ya usafirishaji ya jeshi hilo yapo njiani kutoka jijini Dar es Salaam kuelekea mikoa hiyo ili kuratibu uchukuzi.

Rais John Magufuli juzi Jumatatu aliwakabidhi rasmi wanajeshi shughuli hiyo baada ya kuwafungia nje wafanyabiashara amabao walionekana kusuasua kununua zao hilo kwa bei elekezi ya isiyopungua Shilingi 3,000 za Tanzania kwa kilo.

Awali bei ya zao hilo iliporomoka kutoka wastani wa Sh4,000 kwa kilo kwa mwaka jana mpaka wastani wa Sh1,500 na Sh2,700 kwa msimu huu. Wakulima waligomea bei hiyo na hatua hiyo iliungwa mkono na serikali.

JWTZ

Katika kikao cha pamoja cha serikali na wafanyabiashara kilichofanyika Oktoba 28 na kuongozwa na rais Magufuli ilikubalika bei ya Sh3,300 lakini hatahivyo minada haikuendeshwa kwa kasi ambayo serikali iliitarajia. Hatua hiyo ilitafsiriwa na serikali kama mgomo baridi. Kwanza serikali iliwapa wafanyabiashara siku nne za kutaja kiwango watakachonunua lakini baadaye Magufuli alibadili maamuzi na kuipa shughuli hiyo Benki ya Maendeleo ya Kilimo na JWTZ.

Leo hii mkuu wa 'operesheni korosho' Luteni Benjamin Kisinda ameimbia BBC kuwa wapo tayari kufanikisha oparesheni hiyo kwa ufanisi mkubwa.

Jana waziri mpya wa kilimo nchini Tanzania Japhet Hasunga aliiambia BBC kuwa serikali itafikiria hatima ya wafanyabiashara wa korosho mara baada ya kumaliza ununuzi wa zao hilo.

Korosho

Chanzo cha picha, Issouf Sanogo

Hasunga aliwasili mkoani Mtwara jana mara baada ya kuapishwa na rais Magufuli juzi Ikulu jijini Dar es Salaam kuchukua nafasi ya Charles Tizeba aliyefutwa kazi kutokana na kadhia ya korosho.

"Hatima ya wafanyabiashara wa korosho labda wasuburi tukishanunua hizi korosho ndio tutakaa nao tuamue. Tulishakaa nao vikao vingi, tukakubaliana na bei elekezi, wao hawakutaka kuzingatia. Wanadhani serikali labda hatuwezi ndio maana tunanua wenyewe sasa, halafu ndio tufikirie sasa namna ya kushirikiana nao," amesema Hasunga na kuongeza: "Tunajua kuwa wanaumuhimu, lakini si umuhimu wa kuringa ama kutaka kununua kwa shilingi 1,500 au 2,000..."

Sakata la korosho pia limesababisha aliyekuwa waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji Charles Mwijage kufutwa kazi na nafasi yake kuchukuliwa na Josephat Kakunda.