Benki ya Dunia yathibitisha kuinyima Tanzania mkopo wa dola milioni 300

Rais Magufuli

Chanzo cha picha, IKULU

Taarifa za Tanzania kunyimwa mkopo wa dola milioni 300 na Benki ya Dunia ni sahihi, BBC imethibitisha.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Benki hiyo kimeambia BBC kuwa mkopo huo ambao ulikuwa unalenga kuboresha elimu nchini Tanzania hautatolewa tena.

Fedha hizo zilitarajiwa kufika Tanzania mwezi uliopita, Oktoba 2018. Taarifa za kuzuiwa kwa mkopo huo awali ziliripotiwa na Shirika la Habari la CNN lenye maskani yake nchini Marekani.

Chanzo hicho pia kimethibitisha kuwa moja ya sababu kuu za kuzuiliwa kwa mkopo huo ni uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuzuia wanafunzi wanaopata ujauzito kuendelea na masomo mara baada ya kujifungua.

Katika taarifa rasmi iliyotumwa kwa barua pepe na moja ya wasemaji wakuu wa benki hiyo aliyopo jijini London, Benki hiyo imesema inaendelea na majadiliano na serikali ya Tanzania juu ya suala hilo.

"Benki ya Dunia inaunga mkono sera ambazo zinawatia moyo wasichana na kuwawezesha kubaki shule mpaka mwisho wa uwezo wao. Matokeo ya kiuchumi na kijamii kwa wasichana kumaliza elimu yao ni makubwa kwa kila jamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo," sehemu ya barua pepe hiyo inasomeka na kuongeza: "Tukishirikiana na wadau wengine tutaendelea kupigania haki ya wasichana kupata elimu kwa kujadiliana na serikali ya Tanzania."

Magufuli na Bird

Chanzo cha picha, IKULU

Maelezo ya picha, Rais John Magufuli alikutana na Mwakilishi Mkaazi wa Benki ya Dunia Tanzania Bi Bella Bird mwezi uliopita Ikulu ya Magogoni

Mwezi Juni mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza rasmi kuwa wanafunzi watakaopata ujauzito hawataruhusiwa kuendelea na masomo katika shule za serikali. Wakati Magufuli akitoa kauli hiyo, kulikuwa na vuguvugu la wanaharakati na wanasiasa wakiwemo kutoka chama tawala cha CCM ambao walikuwa wanataka kufanyike maboresho ya sheria ili kuwaruhusu mabinti hao kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Kwa sasa hakuna takwimu rasmi inayoonyesha idadi ya wanafunzi ambao wamefukuzwa shule nchini Tanzania kutokana na ujauzito.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, sababu nyengine ya kuzuiliwa kwa mkopo huo ni maboresho ya Sheria ya Takwimu yaliyopitishwa na Bunge la Tanzania Septemba 10 ambapo pamoja na mengine, inakataza usambazaji wa takwimu zinazolenga kupinga, kupotosha au kukinzana na takwimu rasmi za serikali.

Adhabu ya kufanya hivyo ni faini ya Dola 6,000 au kwenda jela miaka mitatu.

Mwezo Oktoba Benki ya Dunia ilitoa taarifa rasmi ya kuonesha masikitiko yake juu ya uamuzi huo. "Tumeifahamisha serikali ya Tanzania kwamba marekebisho hayo, iwapo yatatekelezwa, huenda yakaathiri sana kuandaliwa kwa takwimu rasmi na zisizo rasmi, ambazo huwa muhimu sana kwa ustawi wa taifa lolote lile.

Ni muhimu sana kwa Tanzania, sawa na taifa jingine lolote, kutumia sheria za takwimu kuhakikisha takwimu rasmi ni za kiwango cha juu zaidi na za kuaminika na pia kulinda uwazi na uwajibikaji katika matumizi yake, kuendeleza mjadala kwa manufaa ya raia," ilisema taarifa hiyo.

Afisa huyo wa Benki hiyo amethibitisha kuwa safari zote rasmi za wafanyakazi wa Benki ya Dunia zimesitishwa kutokana na hofu ya kukamatwa na kushtakiwa watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni alitangaza operesheni ya kuwakamata wapenzi wa jinsia moja lakini baadaye serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje 'ilimruka' kwa kusema uamuzi huo ni wake binafsi na si sera ya nchi.

Awali BBC iliwasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Tanzania Leonard Akwilapo ambaye alisema taarifa za kuzuiwa kwa mkopo huo amezisoma mtandaoni na ofisi yake haikuwa inategemea kupokea pesa yoyote kutoka Benki ya Dunia.

"...hatuna taarifa rasmi na serikali haifanyi kazi kwa kusikia kwenye mitandao ya kijamii," Akwilapo ameiambia BBC.

Msemaji wa serikali Dkt Hassan Abbas pia ameiambia BBC kuwa hawezi kuliongelea suala hilo sababu hana taarifa rasmi mpaka sasa.

Wakati huo huo, wanaharakati kutoka kituo cha utetezi wa haki ya uzazi kijulikanacho kama Equity Now wanasema ni wakati muafaka sasa kwa serikali ya Tanzania kuangalia upya sera yake kwasababu wasichana wanaoacha masomo kutokana na mimba ni wengi.

Kwa mujibu wa kituo hicho, kwa mwaka 2013, wasichana zaidi ya 8,000 walifukuzwa au kuacha shule.

"Benki ya Dunia inajaribu kuishutumu serikali kwa sababu haitendi haki kwa watoto na jukumu la Tanzania ni kuhakikisha haki za kila mtu zimetiliwa maanani," Juddy Gitau mratibu wa kituo hicho ameiambia BBC na kuongeza: "Jambo la muhimu ni kuelimisha wasichana na vijana pia ili waelewe namna ya kujikinga kuingia katika huo mtego na jamii ielewe kwa sababu mimba sio ugonjwa. Kwa mujibu wa utafiti ambao tumeufanya nchini Tanzania ,wasichana wengi wamedhulumiwa na watu wao wa karibu hivyo kuna mambo mengi ya kuangalia katika kutatua tatizo hili na sio kuwaachisha wasichana peke yao."