Uchaguzi Marekani 2018: Republicans wapoteza wingi bunge la Congress wabanwa kwenye Ugavana

Rais Trump

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais Trump akiwa katika mkutano wa kampeini jimbo la Indiana siku moja kabla ya kura ya katikati ya muhula

Chama cha Rais Donald Trump, Republicans kimepoteza wingi katika bunge la Congress hali ambayo itafanya urais wa Trump kupitia katika wakati mgumu zaidi.

Republicans pia wamepoteza viti saba vya Ugavana mpaka sasa. Chama hicho kimefanikiwa kubaki na wingi katika bunge la Seneti.

Kwenye uchaguzi wa bunge la Congress, mpaka sasa majimbo 412 yametangaza matokeo. Democrats wanaongoza kwa viti 219 huku Republicans wakifuatia na viti 193. Bado kuna majimbo ya uchaguzi 33 hayajatangaza matokeo na Democrats wanatarajia kushinda zaidi. Katika uchaguzi kama huu mwaka 2014 Republicans walizoa viti 247 na huku Democrats wakiambulia viti 188.

Ushindi wa Democrats katika bunge la Congress, si jambo zuri hata kidogo kwa Rais Trump ambapo sasa atakabiliwa na upinzania maradufu katika kutekeleza sera zake kwa miaka miwili iliyobaki kwenye muhula wake wa uongozi.

Upande wa bunge la Seneti mpaka sasa kati ya majimbo 96 yaliyotangaza matokeo, Republican wameshinda 51 na Democrats 43. Bado majimbo manne hayajatangaza matokeo. Katika uchaguzi kama huu uliofanyika mwaka 2014, Republicans walishinda viti 54 huku Democrats wakipata viti 46.

matokeo

Katika upande wa Magavana, tayari majimbo 47 yameshatangaza matokeo huku Republican wakiongoza kwa kuwa na viti 25 na Democrats 20. Bado kuna majimbo matano hayajatangaza matokeo. Mwaka 2014 Republicans walishinda majimbo 37 na Democrats 17.

Uchaguzi huu wa katikati ya muhula unakuja wakati rais Trump amefikia nusu ya muda wa uongozi wake madarakani.

Uchaguzi huu pia unatarajiwa kubaini ikiwa Trump ana uwezo wa kuongoza Marekani katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Shauku ya upigaji kura hususani kwa vijana ulikuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 2014.

wapiga kura Marekani

Chanzo cha picha, Getty Images

Siku za hivi karibuni rais Trump amekuwa akitumia mbinu tofauti kuwasilisha hoja ambazo zinaonekana kuzua hisia mseto katika juhudi ya kuimarisha uungwaji mkono wake.

Aliyekuwa mtangulizi wake, Barack Obama - amekuwa mstari wa mbele kuendesha kampeni za chama cha Democratic - amesema "hulka ya taifaletu iko katika sanduku la upigaji kura".

Ni masuala gani muhimu katika uchaguzi huu?

Wakati wa kampeini zake za mwisho katika majimbo ya Ohio, Indiana na Missouri, bwana Trump alirejelea masuala muhimu yaliyomsaidia kushinda uchaguzi wa mwaka 2016 akisisitiza kuwa Democrats watasambaratisha uchumi na kwa kuruhusu uhuamiaji haramu.

Aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Aliyekuwa rais wa Marekani Barack Obama

Wagombea wa Democratic kwa upande wao wameamua kujiepusha na makabiliano ya moja kwa moja na wapinzani wao na badala yake kuangazia masuala ibuka kama vile ya afya na ukosefu wa usawa katika mambo ya uchumi.

Chama hicho kinatumai kuwa wapiga kura vijana na wale wanaotokea katika makundi ya wachache waliyotengwa watavutiwa na kura hiyo kama hatua ya kupinga msimamo wa rais Trump dhidi ya masuala yanayowagusa wao na wenzao moja kwa moja.

Trump amekabiliwa na ukosoaji mkubwa kutokana na lugha yake ambayo inadaiwa kuwagawanya watu.

Upigaji kura wa mapema ulianza Novemba 4 katika majimbo ya Los Angeles na California

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, Upigaji kura wa mapema ulianza Novemba 4 katika majimbo ya Los Angeles na California

Watafiti wa kura ya maoni wanabashiri kuwa Democrats huenda wakashinda viti 23 wanavyohitaji kuongoza bunge la waalikilishi , na viti vingine zaidi kama 15 za ziada.

Uchaguzi huu unamaanisha nini?

Uchaguzi wa katikati ya muhula utaamua ni nani atakayechukua udhibiti wa mabunge yote mawili ambayo yanatunga sheria ya nchi.

Ikiwa Republicans watafanikiwa kuendelea kuongoza mabunge ya seneti na ya uwakilishi, huenda wakaimarisha ajenda ya chama na ile ya rais Trump.

Lakini Democrats wakiwapokonya jukumu hilo huenda wakabadilisha mipango ya bwana Trump.

Katika mahojiano na runinga ya ABC siku ya Jumatatu, rais Trump alisema anataka kupunguza makali ya matamshi yake katika kipindi kilichosalia cha uongozi wake.

"Nahisi kwa kiwango fulani, sina chaguo, nadhani nilitakiwa kupunguza makali ya matamshi yangu kuanzia mwanzo."