Picha ya nyani wawili waliopigwa na bumbuazi yashinda tuzo ya mwaka 2018

Chanzo cha picha, Marsel van Oosten / WPY
Ni picha ya nyani wawili wenye pua mchongoko wakiwa juu ya mawe wakiwa wanaangalia kitu kwa mbali kwa umakini mkubwa.
Ni kitu gani hicho wanachokiangalia, na wanafikra gani vichwani mwao? Jibu ni, wanaangalia ugomvi mkubwa wa baadhi ya nyani kwenye kundi lao kubwa.
Picha hii yenye mchanganyiko wa uzuri wa kuvutia na sokomoko la kuogofya ndiyo mshindi wa jumla wa Tuzo za Mpiga Picha Bora wa Wanyama kwa mwaka 2018. Marsel van Oosten alipiga picha hiyo katika milima ya Qinling nchini Uchina.
Mpiga picha huyo raia wa Uholanzi ilimpasa afuatilie kundi hilo la nyani kwa siku kadhaa ili aweze kufahamu mienendo na tabia zao. Lengo lake kuu lilikuwa ni kuonesha kwa picha moja uzuri wa nywele za mgongoni na nyuso za rangi ya samawati ya madume.
Ustahmilivu wake ukamuwezesha si kupata picha nzuri ya dume bali na jike katika hali ya kustaajabisha na kupendeza.
Van Oosten ameambia BBC kuwa "alishtuka na kujiona aliyeheshimiwa" kupata tuzo hiyo. "Nina furaha hususan kwa picha hii maana hawa ni wanyama waliopo hatarini kutoweka. Watu wachache tu ndio wanaojuwa uwepo wao, na ni jambo muhimu kwetu kutambua kwamba kuna wanyama wengi duniani ambao wapo kwenye hatari ya kutoweka."
"Si faru, chui na dubu pekee (walio hatarini); hata aina hii ya wanyama pia wanahitaji uangalizi na ulinzi wetu wote."

Duma aliyejipumzisha

Chanzo cha picha, Skye Meaker / WPY
Tuzo ya mpiga picha anayechipukia imeenda kwa Skye Meaker kutoka Afrika Kusini kwa picha yake maridhawa ya duma aliyetandawaa kwenye gogo.
Mpiga picha huyo mwenye umri wa miaka 16 alichukua picha hiyo katika Hifadhi ya Akiba ya Mashatu iliyopo nchini Botswana.
Mnyama huyo ni maarufu katika hifadhi hiyo akijulikana kwa jina la Mathoja, lenye maana ya "mwenye kutembea kwa kuchechemea". Duma huyo alivunjika mguu utoyoni.
Kutokana na ulemavu alionao, hawezi kupandisha mawindo yake juu ya miti na humpasa ayale akiwa chini na kupambana na fisi ambao hujaribu kumpora chakula chake, amesema Skye.
"Tulisubiri kwa saa kadhaa kupata picha hii. Nilitaka Mathoja afumbue macho, na kwa dakika kadhaa tuliyapata macho yake yakiwa kodo. Mathoja alituangalia moja kwa moja."
Licha ya tuzo hiyo kubwa, Skye pia amenyakua tuzo ya kipengele cha wapiga picha wa umri wa miaka 15 mpaka 17.
Baadhi ya washindi wa makundi mengine:

Bundi ndani ya bomba

Chanzo cha picha, Arshdeep Singh / WPY
Kundi la wapiga picha chini ya miaka 10- Picha hii imepigwa na kijana mwengine mwenye umri mdogo, Arshdeep Singh. Amenyakua tuzo kwa picha hii aliyoipiga nje kidogo ya mji wa Kapurthala, katika jimbo la Punjab nchini India. "Niliona bundi wakiruka na kuingia ndani ya bomba na kumuarifu baba yangu. Mwanzo alinibishia , akasema haiwezekani, lakini akasimamisha gari. Tulisubiri kwa wastani wa dakika 20 mpaka 30 mpaka walipotoka nje na hapo nikwapiga picha."

Kitanda cha sili

Chanzo cha picha, Cristobal Serrano / WPY
Kundi ka wanyama katika mazingira yao - Cristobal Serrano kutoka Uhispania ameibuka na ushindi katika kundi hali kwa picha yake inawaonesha wanyama wa baharini wajulikanao kama sili ama seals kwa lugha ya kingereza wakiwa wamejipumzisha katika donge kubwa la barafu mithili wapo kitandani katika rasi ya Antarctic.

Dondora wabeba udongo

Chanzo cha picha, Georgina Steytler / WPY
Kundi la tabia kwa wanyama wasio na uti wa mgongo- Georgina Steytler ameshinda kwenye kundi hili kwa picha ya dondora wanaobeba udongo katika mbuga ya Walyormouring magharibi mwa Australia. Ilimpasa alale kwenye matope ili kuwapata vyema katika kimo chao. "Ilinipasa nijilaze chini kwenye tope na kupiga picha moja baada ya nyengine. Nilitaka kumpata vizuri walau dondora mmoja akibeba udongo, kuwapata wawili ilikuwa jambo la kupendeza sana." Dondora hao hutumia tope hilo kujengea nyumba zao.

Kupaa usiku

Chanzo cha picha, Michael Patrick O'Neill / WPY
Kundi la chini ya maji - Huyu ni samaki anayepaa ndani ya maji kwa kutumia mapezi yake yaliyo kama mbawa. Picha hii ya ushindi ilipigwa na mpiga picha na mpiga mbizi kutoka Marekani Michael Patrick O'Neill katika fukwe ya Florida's Palm Beach.

Nyani mwenye huzuni

Chanzo cha picha, Joan de la Malla / WPY
Kundi la wapigapicha za habari - Picha hii ya kushtusha ya nyani aliyekizuizini mtaani ilipigwa na Joan de la Malla katika kisiwa cha Java, Indonesia. Ni nyani aliyelazimishwa kuvalia kama jokeli. "Ni vazi linalomuumiza, na anaonekana akinyanyua mkono wake akijaribu kuvua." Mpiga picha huyo anafanya kazi na taasisi inayotetea haki za wanyama, na nyani huyo tayari ameshaokolewa, na anatarajiwa kurudishwa mwituni.

Vita ya majini

Chanzo cha picha, David Herasimtschuk / WPY
Kipengele cha tabia za mijusi na nyoka- Hii ni vita ya mjusi mkubwa aishie majini afahamikaye kama salamanda na nyoka mkubwa. Picha hii imepigwa katika mto Tellico, jimboni Tennessee nchini Marekani na David Herasimtschuk. Nyoka huyo alifanikiwa kujiokoa kutoka kwenye mdomo wa mjusi huyo mkubwa.

Upepo mkali

Chanzo cha picha, Orlando Fernandez Miranda / WPY
Kundi la Mazingira ya Dunia- Picha hii ya kuvutia inaonesha jinsi upepo mkali unavyopeperusha mchanga katika jangwa na mafuvu nchini Namibia kwenye fukwe ya bahari ya Atlantiki.

Tuzo hizo za picha za wanyama na mazingira zilianzishwa mwaka 1964 na ndio kubwa zaidi katika eneo hilo. Tuzo hizo zinaendeshwa Makumbusho ya Historia ya Asili ya London.
Maonesho makubwa ya picha hizo bora yatafanyika jijini humo kuanzia Ijumaa ya wiki hii. Wahindani wa mwaka ujao wanaanza kuwasilisha picha zao Jumatatu wiki ijayo.












