Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mukhtaar Roobow: Mkuu wa zamani wa Alshabaab awania uongozi serikalini Somalia
Aliyekuwa kiongozi wa kundi la wanamgambo wa kiislamu nchini Somalia, Alshababaab ametangaza kuwa anawania uongozi serikalini.
Mukhtaar Roobow anayefahamika pia kama Abu Mansur, alijitoa katika kundi la Alshabaab mnamo 2012 lakini alijisalimisha kwa serikali ya Somalia mnamo Agosti mwaka jana.
Atawania urais wa jimbo la ksuini magharibi mwa Somalia katika uchaguzi wa kieneo mwezi ujao.
Mukhtar Robow amesema uamuzi huo kuingia katika siasa ni kufuatia wito wa wananchi, wafuasi wake katika jimbo hilo la kusini magharibi.
Amedhihirisha kwamba yupo tayari iwapo atashinda, kuidhinisha uhusiano thabiti na serikali ya shirikisho katika mji mkuu Mogadishu, ambayo imekuwa katika mzozo na tawala za baadhi ya majimbo.
Mukhtaar Roobow ni kiongozi wa juu zaidi katika kundi la al-Shabab kuwahi kujitoa kutoka kundi hilo na kujisalimisha, licha ya kuwa mojawapo ya waasisi wa kundi hilo.
Je Roobow ana nafasi gani ya kupata uongozi serikalini?
Mwandishi wa BBC Bashkas Jugosdaay anasema kuna mgawanyiko.
Kuna kundi linalomtazama na sura ya uovu unaotekelezwa na Alshabaab uliochangia vifo vya maelfu ya watu.
Hilo ni donda ambalo daima kovu yake itasalia na kwa hivyo huenda ikawa vigumu kwake kupata uungwaji mkono kikamilifu.
Na kuna upande wa pili ambao wanatazama faida inayotokana na kujisalimisha kwake na kutoa ushirikiano kwa serikali kuu ya Somalia katika kusaidia kupambana na kundi hilo la wapiganaji wa kiislamu.
Hivyobasi matumiani ni kwamba huenda faida ikaongezeka na pengine ndio anastahili kupata uongozi huo. Na kama anavyoeleza mwenyewe Roobow, wapo watu waliomshinikiza kuwania uongozi, pengine ndio hakikisho la uungwaji mkono wake.
Robow ni nani?
- Bwana Robo alikuwa naibu kiongozi wa al-Shabaab na msemaji wa kundi hilo la wapiganaji wa kiislamu.
- Mnamo mwaka 2000 alipata mafunzo katika kundi la kijihadi la al-Qaeda nchini Afghanistan.
- Alijitoa katika al-Shabab mnamo 2012, kutokana na alichokitaja kuwa ni tofuati za mawazo na fikra.
- Alijisalimisha pamoja na wapiganaji wake katika mji ulio kusini magharibu wa Hudur.
- Baadaye aliliunda kundi lake la wanamgambo waliopigana vita dhidi ya Alshabaab.
Mnamo Juni mwaka jana , kufuatia taarifa kwamba Robow anashirikiana na serikali ya Somalia, Wizara ya mambo ya nje ilimuondoa katika orodha ya magaidi na kufutilia mbali kitita cha dola milioni 5 iliyokuwa imeahidi kwa yoyote atakayesaidia katika kukamatwa kwa Robow.
Usalama bado ni mtihani mkuu kwa utawala wa Somalia
Miezi michache baada ya kutwaa urais wa Somalia kutoka uwanja wa ndege kwa kuhofia mashambulio ya Al Shabaab, Mohamed Abdullahi alitoa ahadi yake kwa wananchi wa Somalia.
Alisema, 'Lengo langu ni kuwashinda Al Shabaab kwa miaka miwili ijayo. Natumai kwamba tukifanya kazi pamoja, tutaleta Amani na utulivu nchini Somalia'.
Lakini uongozi wake umeshuhudia mashambulio, na Mogadishu ingali mojawapo wa miji hatari zaidi duniani.
Hassan Sheikh, mchambuzi wa masuala ya usalama anasema, 'Kwa sababu ni wapiganaji, wanaweza kupenya kirahisi katika maeneo ya umma na ya kibinafsi, na wana athari kubwa katika mfumo wa jamii kisiasa, kiuchumi na kijamii.
'Muhimu zaidi ni kuwa walisababisha uoga, na uoga huu huwasaidia kwani ni vigumu sana kuwakamata au kuwashinda'.
Wachanganuzi wanaamiini kuwa jinamizi la Al Shabab ni gumu kuliangamiza.