Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanariadha wa Kenya Gladys Cherono apata makaribisho ya kipekee nyumbani kwao
Mamia ya wenyeji wa kijiji cha Irimis kaunti ya Nandi eneo la bunde la ufa nchini Kenya walisherehekea kwa nderemo na vifijo ushindi wa Gladys Cherono katika mbio za Berlin Marathon nchini Ujerumani.
Hafla hiyo ilifanyika Jumamosi ya tarehe 22 mwezi Septemba mwaka huu.
Cherono, akiandamana na mumewe Joseph Bwambok na wasichana wao wawili, Lynn Jebet mwenye umri wa miaka 10 na Stacy Jelagat aliye na umri wa miaka 7, alilakiwa kwa shangwe na hoi hoi alipowasili nyumbani katika kijiji cha Irimis kilichoko kilomita 40 kutoka mji wa Eldoret anakoishi Cherono na familia yake.
Wanawake na wanaume pamoja na watoto wakiongozwa na mama yake Cherono, Salina Siror, walipiga vigegelele kwa furaha Cherono alipotoka kwenye gari lao kila mmoja wao akisubiri fursa ya kumkumbatia kwa furaha huku mama yake akimnywesha maziwa yaliyoganda yajulikanayo kama mursik kwa lugha ya jamii ya Kalenjin.
``Tumefurahia sana kumuona msichana yangu Gladys amerudi nyumbani kujiunga nasi kwa karamu hii kubwa,'' alisema mama yake Gladys akiwa mchangamfu.
``Ushindi wake huko Ujerumani ni furaha kubwa kwetu sisi sote, na ndio kwa sababu tumemuandalia karamu hii. Tumechinja ng'ombe na kuku, yeye atakula ule mguu mnono kwa heshima yetu kwake namimi nitampa maziwa yetuy ya mursik Mungu azidi kumuongezea nguvu ashinde tena.''
Baba yake Gladys, Samuel Kogo, anasema tangu aanze kushinda mbio kubwa huko Ulaya msichana wake amebadilisha maisha yao kwani siku hizi wanapata kila kitu watakacho.
``Tena msichana wangu amefanya sisi tunajulikana zaidi kwa kijiji hiki, kila mtu tunaye kutana anatusalimia na kutupongeza. Ni furaka sana, tunashukuru Mungu.''
Gilbert Tarus alikua miongoni mwa wana kijiji hicho aliyehudhuria karamu hiyo na kumlimbikizia Cherono sifa tele kwa ushindi wake huo maridhawa ambao anasema umewapa vijana wengi hapo morali wa kuendeleza vipaji vyao vya kukimbia.
``Unajua kaunti yetu ya Nandi imetoa wanariadha wengi mashuhuri akiwemo baba wa riadha nchini Kenya Kipchoge Keino,'' anasema Tarus, na kuongezea:``Nahimiza wanariadha chipukizi wa kaunti yetu ya Nandi waige mfano wa Gladys pamoja na bingwa wa wanaume Eliud Kipchoge ambaye alivunja rekodi ya dunia. Sisi tumefurahia sana hiyo.''
Cherono, ambaye Novemba tarehe 5 mwaka huu atasherehekea mwaka wake wa 34 wa kuzaliwa, alishinda mbio za Berlin Marathon kwa mara ya tatu na kuweka rekodi mpya ya Berlin ya saa 2,dakika 18 na sekunde 11, na hapo akaondoa sekunde 61 za muda wa zamani uliokua unashikiliwa na Mizuki Noguchi wa Japan aliposhinda mwaka wa 2015 kwa saa 2, dakika 19 na sekunde 12.
Jambo lililomfurahisha zaidi ni kumshinda nyota wa Ethiopia Tirunesh Dibaba na mwenzake Ruti Aga aliyemaliza wa pili na Dibaba akawa wa tatu.
``Nilikua na raha kubwa nilipomaliza mbio hizo nikijua nimeshinda wapinzani wangu wakali kutoka Ethiopia, sasa nitazidi kufanya mazoezi zaidi nishinde Berlin tena mwaka ujao kwa mara ya nne na nivunje rekodi nyingine,'' anasema Cherono. Kwa mara ya kwanza kwa historia ya Berlin Marathon wanariadha wa kwanza watatu walikimbia chini ya saa 2 na dakika 19.
``Tulifanya mazoezi ya kutosha Eldoret na wenzangu, kwa hivyo nilikua na uhakika wa kukimbia vizuri, wasiwasi wangu mkubwa ulikua kwa wenzetu wa Ethiopia,'' anasema Cherono.
Anaungwa mkono na mumewe Joseph Bwambok anayetueleza kama kocha wa mke wake alihakikisha yuko sawa kabisa kwa mbio hizo.
`` Mazoezi yaliendelea vizuri sana bila tatizo lolote, tulijua atapata upinzani mkali kutoka kwa Dibaba na mwenzetu hapa Edna Kiplagat ndio kwa maana tukajikakamua kabisa. Ni siku kubwa leo kuandaliwa karamu kama hii, nitakula nyama hapa vilivyo,'' anasema mumewe Cherono.
Je, wasichana wao wawili Lynn na Tracy wanapenda riadha?, namuuliza Bwambok.
``Ni ajabu wasichana wetu hawashuguliki na riadha na hatuwezi kuwalazimisha, wote wanataka kuwa madaktari,'' anatueleza baba ya watoto hao Bwambok.