Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mafunzo maalum kwa wahudumu wa chumba cha kuhifadhia maiti Tanzania
Wafanyakazi wa chumba cha kuhifadhi maiti katika hosptali nyingi nchini Tanzania wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu bila ujuzi wowote.
Wafanyazi hao huonekana ni watu wa tofauti kwenye jamii, huku wakikabiliwa na changamoto mbalimbali na wengine kufikia hatua ya kutengwa na jamii wakiwaogopa.
Katika kukabiliana na changamoto hizo sasa baadhi ya hosptali nchini humo zimeanza kutoa mafunzo maalumu kwa wafanyakazi hao ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Ukosefu wa mafunzo ya awali umewasababisha wafanyakazi hao kuchukuliwa tofauti na jamii, huku changamoto mbalimbali zikiwaandama na hata kuonekana kuwa si watu wa kawaida na wengine kutengwa.
Lakini sasa mtazamo umebadilika, haswa baada ya kuanza kutolewa mafunzo hayo na kazi yao kuonekana kuwa ni rasmi.
Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza, imeanzisha mafunzo maalumu kwa wafanyakazi wa chumba cha kuhifadhia maiti.
Dokta Kahima Jackson, Mkuu wa Idara ya Maabara katika hospitali ya Buganda na Mkufunzi wa mafunzo hayo, ana sema lengo la kuanzishwa ni kutokana na watumishi wengi waliokuwepo kutokuwa na taaluma hiyo.
'Tuliamua kuanzisha baada ya kubaini kwamba watumishi wengi wa chumba cha maiti walikuwa wakitolewa mitaani na kwamba watu hawa hawana elimu inayohusiana na utunzaji wa maiti.' Amesema Dakta Kahima.
Licha ya kuhusika na utunzaji wa maiti, moja ya kazi yao pia ni kushirikiana na Daktari, pale uchunguzi unapohitajika kujua kiini ama sababu za kifo.
Dokta Kahima anasema uchunguzi unafanywa kwa lengo la kusaidia masuala ya kisheria, pale penye utata.
Kusaidia madaktari na uchunguzi wa kitaalamu na pia kuna baadhi ya watu hutaka kujua sababu zilizosababisha kifo cha ndugu yao.
Mafunzo haya yanatarajia kusaidia kwa kiasi kikubwa wafanyakazi kama Shija kutoka katika hospital ya Nyamagana jijini Mwanza.
Kabla ya kupokea mafunzo hayo, Mhoja alikuwa akifanya kazi yake bila ya utaalamu, hali ambayo ilimsababisdhia madhara.
'' Nilichojifunza ni ule uchanganyaji wa dawa inayotumiwa kuhifadhi mwili, kule nilikokuwa nilikuwa nikiitumia bila ya kuchanganya, ni kali sana ilikuwa ikinichoma kwenye macho, inaniingia puani....'' Amesema Mhoja.
Kwa upande wake mwanamke pekee katika mafunzo hayo Theophilda Ngojani anasema watu walikuwa wakimchukulia kama mtu aliyechanganyikiwa kutokana na kufanya kazi hiyo.
'Hii kazi ndio iliyotuweka mjini utakuta wote tunapanga foleni kutafuta mkate'. Amesema Theophilda.