Tanzania yawafungulia kesi kijiji kizima kwa kosa la kuharibu miundombinu

mbinu

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kijiji kizima kuwajibishwa kwa uharibifu wa miundo mbinu

Polisi mkoani Mbeya nyanda za juu kusini mwa Tanzania wameanza kamatakamata ya watu katika kijiji cha Ngola kwa tuhuma za kuharibu miundombinu ya maji.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila aliamuru polisi mkoani humo wakamate wakazi wote wa kijiji hicho siku ya Jumatano, Agosti 15.

Wakaazi wa kijiji hicho wanashutumiwa kuharibu miundombinu ya maji yenye thamani ya dola elfu ishirini katika kijiji jirani cha Masheye ambacho kipo katika mkoa huohuo wa Mbeya.

Kijiji cha Ngola kipo katika mlima na hakijaunganishwa na huduma za maji safi na salama, hali ambayo inatajwa kuwatia hasira watu 1,600 wa kijji hicho.

Mkuu wa mkoa Chalamila ameiambia BBC kuwa kijiji chote lazima kiwajibike kwa ubadhirifu huo.

Tayari diwani wa eneo hilo ni miongoni mwa wale waliokamatwa.

"Kule kuna watu wenye akili timamu, lakini walishindwa kuzuia uharibifu…baada ya wao kushindwa nikaona ni muhimu kutuma polisi wawakamate wote. Naamini kuanzia sasa wataheshimu na kulinda miundombinu ya umma."

Wakuu wa mikoa na wilaya nchini Tanzania wana ruhusa ya kisheria ya kuamuru polisi kukamata mtu na kumuweka rumande mpaka kwa saa 48 kabla ya kumpeleka mahakamani.