Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sheria ya kikomo cha umri wa kugombea urais yaidhinishwa na mahakama Uganda
Mahakama ya katiba nchini Uganda imeidhinisha mageuzi ya katiba yaliondoa kikomo kwa umri wa kugombea urais.
Majaji wanne kati ya watano wa jopo la majaji wamesema mageuzi hayo hayakiuki katiba, na pia hayendi kinyume na hsri aya muongozo wa bunge nchini.
Awali umri wa mwisho kwa kugombea ilikuwa miaka 75.
Hii ina maana Rais wa nchi hiyo Yoweri Kaguta Museveni atakua huru kugombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021.
Kikao cha kutoa uamuzi huo uliowasilishwa katika mahakama kuu huko Mbale kilianza kwa naibu jaji mkuu, Alfonse Owiny-Dollo, kuanza kwa kuomba radhi kwa mahakama kuchelewa kuanza kwa muda uliopangwa awali.
Masuala matatu makuu ambayo mahakama ilitakiwa kuyatolewa maamuzi ni:
Hata hivyo mahakama imekataa kuongeza miaka ya wabunge waliotaka kusalia madarakani kwa miaka 7 badala ya mitano ya sasa.
Katika uamuzi wake Jaji Cheborion Barishaki ameeleza kwamba kuongezwa kwa muhula wa kuhudumu bunge kutoka miaka mitano hadi miaka saba itakuwani hatua ya kibinfasi na inakwenda kinyume na maadili ya uongozi bora:
Ameeleza kwamba kwa kutowashauri raia kuhusu kuongeza muhula wa kuhudumu, wabunge wamejilimbikizia uongozi ambao unatolewa kikatiba kwa watu kuamua ni nani wanaemtaka awaongoze.
Na kwa kuongeza muda wa wabunge kuhudumu kwa miaka miwili zaidi, viongozi hao wamewanyima raia nafasi za uchaguzi mwaka 2021, uliopangiwa uchaguzi mkuu nchini.
"Katiba ni ya kuwatumikia watu na sio kwa namna nyingine yoyote," alisema.
Kesi hii imewasilishwa baada ya watu kutoridhia hatua ya mageuzi hayo ya katiba yaliokumbwa na mzozo mwaka jana, yaliochangia kuondolewa kwa kikomo cha umri wa kugombea urais, na kuongezwa muda wa kuhudumu nyadhifa za kisiasa kutoka miaka mitano hadi misaba.
Je uamuzi huo umefuatiliwaje?
Raia nchini Uganda Alhamisi walifuatilia kwa makini uamuzi huo ukipitishwa kutoka mahakama ya katiba Mable kupitia vyombo vya habari na hata pia mitandao ya kijamii.
Na wakati uamuzi ukiendelea kusomwa kuhusu kuidhinishwa kwa kikomo cha umir wa kugombea urais - hatua inayoonekana ambayo huenda ikamruhusu Rais Yoweri Museveni kuendelea kuhudumu madarakani kwa zaidi ya utawla wake wa miongo mitatu, haya ndio baadhi ya yaliozungumzwa mitandaoni:
Kumekuwa na pingamizi kwa pendekezo la kuibadili katiba mwaka jana sio tu miongoni mwa raia nchini, lakini pia upinzani, viongozi wa kidini na hata baadhi ya wafuasi katika chama tawala Uganda.
Kulishuhudiwa maandamano makubwa kupinga hatua hiyo katika sehemu tofauti nchini na kusababisha Polisi kuingilia kati na kujaribu kuzima ghasia zilizozuka.