Mlipuko umetokea katika mkutano wa waziri mkuu Abiy Ahmed Ethiopia

Mlipuko mkubwa umetokea katika mkutano wa waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Inaarifiwa kwamba watu 83 wamejeruhiwa huku 6 wakiwa katika hali mahututi.

Imebidi kiongozi huyo mkuu aondoshwe kwa haraka muda mfupi baada ya kutoa hotuba yake wakati mlipuko huo unaodhaniwa kuwa wa guruneti, ulipotokea.

Maelfu walikuwa wamekusanyika katika bustani kuu ya Meskel mjini Addis Ababa katika mkutano ulioandaliwa kuiunga mkono serikali yake Abiy.

Abiy amelitaja shambulio hilo kama "Jaribio ambalo halikufanikiwa la vikosi visivyotaka kuiona Ethiopia imeungana".

Vyombo vya habari nchini vinaripoti kuwa watu kadhaa wamejeruhiwa na wamepelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu na bustani hiyo kupokea matibabu.

Mwandishi wa BBC nchini Ethiopia Emmanuel Igunza aliyekuwa katika eneo hilo anasema kulikuwa na kelele nzito na kubwa iliyosikika karibu na jukwaa walipokaa watumashuhuri muda mfupi baada ya waziri mkuu Abiy Mahmed kumaliza kuuhotubia umati.

Abhiy hakujeruhiwa na aliondolewa kwa haraka na maafisa wa usalama kutoka eneo hilo.

Abebaw Bekele, mkuu wa shirika la msalaba mwekundu mjini Addis, amesema wametuma ambulensi 13 kutoa usaidizi.

''Ambulensi 5 zilikuwa karibu kutoka eneo la mkasa. Maafisa wetu wamefika haraka na kusaidia kuwaondoa majeruhi kuwafikisha katika hospitali tofuati''.

Hali ya utulivu sasa imerejea na duru za polisi zinasema wanachunguza tukio hilo.

Umati mkubwa wa watu ulikusanyika katika mkutano huo ulioandaliwa kuiunga mkono serikali ya kiongozi huyo mpya anayeidhinisha mageuzi ambayo hayajawahi kushuhudiwa nchini.

Abiy Ahmed ni nani?

Abiy aliichukua nafasi ya waziri mkuu Ethiopia baada ya kiongozi aliyekuwepo Hailemariam Desalegn aliopjiuzulu ghafla mnamo Februari

Yeye ni kiongozi wa kwanza kutoka jamii ya Wa Oromo ambayo imekuwa ikiandamana dhidi ya serikali kwa takriban miaka mitatu ambapo mamia ya watu walifariki.

Inaaminika Abiy anaungwa mkono pakubwa miongoni mwa vijana wa Oromo pamojana makabila mengine.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 42alizaliwa katika mji wa Agaro huko Oromia na anatoka katika familia iliyochanganyika waislamu na wakristo.

Amelitumikia jeshi, ameidhibisha shirika la habari na usalam nchini, linalohusika na masuala ya usalama mtandaoni katika nchi ambayo serikali imedhibiti vikali mtandao.

Aliwahi pia kuwa waziri wa sayansi na teknolojia.