Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Unaweza kukaa muda gani bila kuishika simu?
Unaweza kukaa muda gani bila kuwa na simu yako, kabla ya kuanza kuhangaika?
Mfano uwe umeisahau pahali, imeisha chaji au labda umelazimishwa kuizima na kuiweka mbali?
Wanasaikolojia wamegundua kwamba jibu lake litakuwa dakika chache sana - hasa iwapo umri wako ni kati ya miaka 18 na 26.
Baada ya kufanya utafiti, waligundua kwamba watu ambao walipokonywa simu walikuwa na uwezekano wa juu wa kuonyesha tabia ya "mfadhaiko" wakilinganishwa na watu walioachwa kukaa na simu zao.
Washiriki, baada ya kupokonywa simu zao, walipopewa simu - hata kama hazikuwa zao - walionesha kuwa na kiwango cha chini kidogo cha mfadhaiko.
Watafiti wanasema siku hizi watu wameanza kutumia simu kama mbadala badala ya kutangamana na watu.
Wanalinganisha na jinsi mtoto anavyotuliwa hata kwa blanketi wazazi wake wanapokuwa mbali.
Utafiti huo ulianywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Eotvos Lorand nchini Hungary.
Veronika Konok, mmoja wa watafiti, anasema: "Binadamu anaweza kuunga uhusiano mzito sana na vifaa, na vitu kama vile picha za watu muhimu kwake, au wanasesere.
"Simu ni muhimu sana kwa sababu bali na kuwa kifaa muhimu, pia ni hutusaidia kujumuika na wengine kupitia teknolojia."
Utafiti huo ulifanywa miongoni mwa kundi la vijana wa miaka 18 hadi 26, ambao tabia zao zilinakiliwa kupitia video na mapigo yao ya moyo kupimwa.
Walipokonywa simu walionyesha dalili za mfadhaiko.
Veronika anasema anafikiri vijana wamekuwa na uhusiano mkubwa na simu zao.
"Watoto wanaotumia simu kuanzia utotoni, nafikiri uhusiano wao na simu utakuwa hata zaidi."
Matokeo yake si ya kushangaza, kwani simu yako ikiishiwa na chaji au uipoteze kwa muda, mwenyewe unfahamu kwamba unaweza kutatizika si haba.
Wasiwasi wa kuwa mbali na simu yako hata umepewa jina - unaitwanomophobia, ambao ni ufupisho wa "no-mobile-phone phobia".
Tatizo hilo huathiri vijana wanne kati ya watano kwa mujibu wa baadhi ya utafiti.