Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Viongozi wa madaktari Kenya waachiliwa huru, wapewa muda kumaliza mgomo
Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imeamua viongozi wa chama cha wahudumu wa afya waliokuwa wamefungwa jela mwezi mmoja waachiliwe huru mara moja.
Viongozi hao saba walifungwa Jumatatu baada ya kupatikana na hatia ya kutofuata uamuzi wa mahakama wa kumaliza mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa miezi miwili unusu sasa.
Viongozi hao wametakiwa kuhakikisha suluhu ya mgomo huo inapatikana katika kipindi cha siku saba.
Mazungumzo ya kutafuta suluhu yataongozwa na Chama cha Wanasheria Kenya (LSK) na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNHCR).
Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara na kuboresha mazingira ya utendaji kazi hospitalini
Wanataka pia serikali iwekeze zaidi katika dawa, vifaa na mitambo hospitalini pamoja na kutoa pesa zaidi za kufadhili utafiti wa kimatibabu.
Wamekataa mshahara walioongezewa na serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule walioafikiana mwaka 2013.
Karibu madaktari na wauguzi 5000 kutoka hospitali 2000 za umma, walianza mgomo wiki ya kwanza ya mwezi Desemba na wagonjwa wamekuwa wakikosa matibabu.