Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Viongozi wa madaktari Kenya wafungwa jela mwezi mmoja
Mahakama ya masuala ya wafanyakazi nchini Kenya imewahukumu viongozi saba wa chama cha wahudumu wa afya (KMPDU) kufungwa jela mwezi mmoja kwa kukaidi agizo la kumaliza mgomo ambao umedumu kwa zaidi ya miezi miwili.
Jaji Hellen Wasilwa amesema viongozi hao hawajatoa sababu ya kutosha kuonesha ni kwa nini hawajamaliza mgomo huo.
Ameamuru mazungumzo ya kumaliza mgomo huo yaendelee.
Jaji Wasilwa alikuwa awali amewapa viongozi hao muda wa wiki mbili kumaliza mgomo huo, na baadaye akawaongezea siku tano.
Mazungumzo ya kumaliza mgomo huo hata hivyo hayakuzaa matunda kipindi hicho.
Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara.
Wamekataa mshahara walioongezewa na serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule walioafikiana mwaka 2013.
Karibu madaktari na wauguzi 5000 kutoka hospitali 2000 za umma, walianza mgomo wiki ya kwanza ya mwezi Desemba na wagonjwa wamekuwa wakikosa matibabu.