Mafuriko nchini India 'yavunja rekodi za awali'

Mafuriko ambayo yamesababishwa na mvua itokanayo na pepo za msimu mto Ganges, India yamevunja rekodi zilizowekwa awali katika maeneo manne kaskazini mwa India, maafisa wameambia BBC.

Maafisa wamesema maji yamefikia viwango vya juu sana kuliko ilivyotarajiwa.

Viwango vya juu zaidi vilishuhudiwa Patna, jiji kuu la jimbo la Bihar ambapo kina cha maji ya mafuriko kilifikia 50.52m (166ft) mnamo 26 Agosti. Rekodi ya awali ilikuwa 50.27m mwaka 1994.

Mafuriko nchini India yameua zaidi ya watu 150 msimu huu na kuacha maelfu wengine wakiwa bila makao.

Majimbo ya Bihar na Uttar Pradesh yameathiriwa zaidi na mafuriko katika mto Ganges ambao ndio wa tatu kwa ukubwa duniani.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa India, hata hivyo, inasema kiwango cha mvua ambayo imenyesha maeneo hayo wiki za karibuni kimepungua.

Wataalamu wanasema mafuriko ya sasa huenda sana yamezidishwa na mchangatope ambao hubebwa na maji ya mto Ganges.

Mchangatope huo unadaiwa kupunguza kina cha maji mtoni na hivyo maji kuvunja kingo wakati wa mvua kubwa.

Baadhi ya wanajiolojia wanasema ongezeko la visa vya maporomoko ya ardhi eneo la Himalaya limeongeza kiasi cha mchangatope unaobebwa na maji ya mto huo.

Serikali inapanga kujenga mabwawa zaidi kukabiliana na mafuriko hayo. Mabwawa mawili yatajengwa eneo la Nepal na moja Arunachal Pradesh.