Mahali pekee ambapo nyangumi huja kutazama binadamu

    • Author, Kathleen Rellihan
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kuna wakati waliwindwa karibu kutoweka, nyangumi wa kijivu katika bahari ya Pasifiki katika eneo la Laguna San Ignacio huko Mexico sasa wanaonekana kutaka kuwajua binadamu kama vile tunavyotaka kuwajua wao.

"Anakuja tena!" mwongozaji wetu, José Sanchez, anasema wakati nyangumi mkubwa anapotukaribia kwa mara ya tano ndani ya dakika 45. Kila wakati anapokuja kwenye mashua yetu iliyozimwa, huinua kichwa akitutazama tunapomtazama.

Mashua yetu inapokaa kimya na injini ikiwa imezimwa, nyangumi huyu wa tani 40 anasugua kingo za mashua na kuinua sehemu ya juu ya mwili wake wenye madoadoa meupe na kutuangalia sote sita. Tuko ndani ya jicho la nyangumi - ambalo lina ukubwa wa kama mpira wa besiboli.

Hapa ni pwani ya magharibi ya peninsula ya Baja California Sur, Laguna San Ignacio – linaelezwa kuwa ndilo eneo la kuzaliana la nyangumi wa kijivu wa Pasifiki. Hii ni hifadhi inayolindwa ya nyangumi, pia sehemu ya matukio yasiyo ya kawaida. Hapa nyangumi hutafuta mawasiliano na wanadamu.

Kila mwaka kuanzia Januari hadi katikati ya Aprili, maelfu ya nyangumi wa kijivu hufika eneo hili wakati wa safari ya kilomita 19,300 kutoka kwenye maji ya barafu ya Aktiki hadi kwenye maji ya joto ya Baja California Sur ili kujamiiana na kuzaa.

Ingawa eneo hili sasa maji yake ni salama kwa kuzaliana, huko nyuma nyangumi wa kijivu waliwindwa katika eneo hili. Hata hivyo, inaonekana wanyama hao sasa wamejifunza kuwaamini wanadamu.

Kwa hakika, wakati wa safari yangu ya hivi karibuni ya kutazama nyangumi na kampuni ya utalii wa mazingira ya Pure Baja Travels, tulishuhudia nyangumi mama wakileta watoto wao kwenye boti.

Pia unaweza kusoma

Tabia ya nyangumi hao

Kwa zaidi ya miaka 50, nyangumi wa kijivu huko Baja wameonyesha kuwa na udadisi kama sisi wenyewe. Wanabiolojia wa baharini wanaamini hali hii ina sababu.

"Katika rasi hiyo kwa sasa, hakuna vitisho," anasema Dk Steven Swartz, mtafiti ambaye amewasoma nyangumi wa kijivu huko Laguna San Ignacio kwa miaka 45.

Nyangumi hawa ni maarufu kwa kuwakaribia wanadamu, na kulingana na Swartz, hapa ndipo mahali pekee ambapo hufanya hivyo mara kwa mara, na huinuka mara nyingi zaidi kutoka majini ili kuruhusu wanadamu kuwagusa.

Sheria za eneo hilo

Kuangalia nyangumi kunaruhusiwa tu katika eneo maalum la hifadhi ya nyangumi, na kuna sheria kali: Boti zote lazima zizime moto wakati nyangumi wanapokaribia. Na muhimu zaidi, waendeshaji mashua hawawafukuzi au kuwafuata nyangumi.

"Manahodha wanakupeleka katika eneo hilo, na wanawaacha nyangumi waamue kama watakuja, na kusema hello au la," anasema Swartz.

“Mamalia wana hamu ya kutaka kujua; wana hisia za kutaka kujifunza kuhusu mazingira yao, na wanajifunza kwa kuchunguza," anaeleza Swartz, akiongeza kuwa akina mama hupitisha udadisi huu wa kuzunguka boti na watu kwa watoto wao. "Na [Nyangumi] wana uwezo wa kukumbuka."

“Nyangumi, kwa ujumla, wanapenda kusugua na kugusa; hivyo ndivyo wanavyowasiliana, Swartz anasema. Nyangumi wa kijivu wa Pasifiki hawaji hapa kutafuta chakula, bali hutafuta wakiwa Aktiki.”

“Ingawa hatuwezi kujua hasa kwa nini nyangumi hufanya kile wanachofanya,” anasema Swartz na wanabiolojia wengine wa baharini wote wanakubali nyangumi hao hukaribia boti kwa hiari.

Chanzo cha matukio ya sasa

Nyangumi wa kijivu waliwindwa na kukaribia kutoweka wakati wa Karne ya 18 na 19, na kwa sababu hiyo, wanyama hawa wakawa na tabia ya ukali kwa wanadamu - kiasi kwamba wavuvi wa eneo hilo waliwaita "samaki wa shetani" na kuwakwepa.

Lakini katika 1972, mwanaume aitwaye Francisco (Pachico) Meya alikuwa akitoka kuvua samaki huko Baja wakati nyangumi alipotokea na kukaa karibu na mashua yake. Udadisi ukamfanya auweka mkono ndani ya maji. Nyangumi alimsugua Meya na kukaa na kukaa kwa muda.

Habari kuhusu tukio la Meya zilienea, na wenyeji, bila woga, walingoja kwa subira ili kukutana na nyangumi. "Nyangumi wa kijivu hawajawahi kuogopa kukaribia vitu vinavyoelea ndani ya maji. Nyangumi wa kijivu wakaanza kuzoea mwingiliano huo," Sanchez ananiambia.

"Baada ya mawasiliano ya kwanza [ya Meya] yaliyokwenda kwa amani, wanadamu walianza kutambua nyangumi wa kijivu sio wanyama wa kutisha kama tulivyofikiri.”

Sanchez alikuwa mwanasayansi wa kwanza wa Meksiko kuongoza ziara za kutazama nyangumi katika rasi hii katika miaka ya 1990, na kampuni yake ya utalii wa mazingira sasa ina kambi huko San Ignacio Lagoon.

Mwaka 1972, serikali ya Mexico iliunda hifadhi ya asili ya San Ignacio Lagoon, na 1988, rasi hiyo pia ilitangazwa kuwa hifadhi ya nyangumi. Miaka mitano baadaye, iliteuliwa kama Eneo la Urithi wa Dunia na UNESCO. Nyangumi wa kijivu waliondolewa kwenye orodha ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka mwaka 1994.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah