Jinsi China inavyotumia wapelelezi kufuatilia na kuwachafua wapinzani wanaoishi Marekani

Kama mpinzani mkongwe wa jimbo la California na mwanaharakati dhidi ya serikali ya China, Arthur Liu, ambaye ni baba wa kiongozi wa Olimpiki, Skater Alyssa Liu, hakushangazwa hasa kupokea simu kutoka shirika la Upelelezi la Marekani (FBI).

"Niliambiwa kwamba serikali ya China imetuma wapelelezi kwenye eneo la San Francisco Bay kupata taarifa za pasipoti ya binti yangu", aliiambia BBC.

"Siwezi kusema kuwa nilishtuka, lakini nilifikiri, ole wao wanalichukulia jambo hili kwa uzito mkubwa".

Wito wa mashaka

Mara ya kwanza, Liu hakuelewa baada ya kupokea simu ya "mashaka" kutoka kwa mtu anayedai kuwa ametokea kwenye Kamati ya Olimpiki ya Marekani na Paralympic, akidai kuwa alikuwa akifanya "mapitio ya maandalizi" kwa ajili ya safari ya Olimpiki ya Winter mwezi Februari mwaka huu.

"Sikufahamu kabisa kuwa alikuwa ni mtu ambaye hakuwa ametokea kwenye kamati ya Olimpiki", Liu alikumbuka. "Niliamua kufanya kitu sahihi na sitoi taarifa yoyote. Hiyo siyo tu namna tunavyowasilisha pasipoti ".Sauti ya upande mwingine, mamlaka za Marekani zinaamini, alikuwa Anthony Ziburis, mlinzi wa zamani wa gereza na mpambe wa jimbo la Florida.

Ujumbe wake ulikuwa ni kuwapeleleza na kuwachafua wapinzani wa Kichina kwa ajili ya huduma za upelelezi za Beijing. Wapinzani hao waliripotiwa kuwa ni pamoja na raia wawili wa Marekani, Liu na Yan Xiong, kasisi wa jeshi la Marekani na mgombea wa ubunge ambaye alihusika katika maandamano ya 1989 kwenye viwanja vya Tiananmen.

Mwezi Machi Ziburis alishtakiwa na Idara ya Sheria ya Marekani kwa upelelezi wa serikali ya China. Mpaka sasa, mawakala wa Marekani wameshtaki watu wasiopungua 12, wakiwemo raia kadhaa wa Marekani, kwa kuwabughudhi na kuwanyanyasa wakazi wa Marekani nchini China.

Pia unaweza kusoma:

Onyo kutoka kwa MI5 na FBI

Mashtaka pia yalifunguliwa mnamo Julai 8 dhidi ya watu wengine wawili ambao walikuwa sehemu ya mpango huo kama wale waliokuwa wanamlenga Liu.

Kesi ya Liu inakuja wakati wa mvutano, Marekani na Uingereza, kutokana na kuongezeka kwa shughuli za upelelezi wa Kichina duniani kote.

Katika tukio lisilo la kawaida lililofanywa na umma wiki iliyopita kwenye kiwanja cha MI5 jijini London, viongozi wa huduma za usalama za Marekani na Uingereza walionya kuhusu mtandao mkubwa wa upelelezi na programu ya uvamizi - ambao ni mkubwa kuliko wote katika nchi nyingine kubwa za dunia - inaoendeshwa na China.

Programu hii inaaminika kuwa ni sehemu ya juhudi kubwa, zinazokua na zenye sura tofauti ili kuifaidisha China dhidi ya washindani wake na kunyamazisha au kukandamiza vitisho vilivyoonekana dhidi ya serikali ya Chama cha Kikomunisti cha China.

Mkakati huo unahusisha kila aina ya juhudi, kuanzia uvamizi hadi upelelezi kwenye milango.

"Sumu tano" za China

Maajenti wa zamani wa upelelezi nchini Marekani wanasema kuwa watu wanaolengwa zaidi ni wale wanaoaminika kuwa na uhusiano na kile ambacho serikali ya China imekitambua kama "sumu tano" zinazoitishia.

Nao ni: Watu wa Kitibeti na Uyghur wanaotaka kujitenga, wanaharakati za kiroho wa kundi la Falung Gong, wanaharakati wanaojitegemea wa nchini Taiwan kama ilivyo kwa Liu, wanachama wa harakati za kudai demokrasia nchini China.

Kwa bahati mbaya, juhudi hizi zinatarajiwa kuongezeka huku kukiwa na uhusiano mbaya wa Sino na Marekani, na hata raia wa Marekani hawajaachwa. Kwa Liu, ambaye alitoroka China kupitia Hong Kong baada ya maandamano ya mwaka 1989 ya kudai demokrasia katika viwanja vya Tiananmen, mawazo ya kupelelezwa yaliwahi kutokea.

Jaribio la awali lilimalizika wakati alipokuwa na urafiki bila kujua na wakala wake, mwanafunzi aliyetambulishwa kwake kupitia mawasiliano ya mtandao wa China wa wakazi wa nje ya nchi hiyo ambaye alimsaidia kupata makazi nchini Marekani.

"Mmoja au miaka miwili baadaye aliniambia kwamba ameombwa kunipeleleza. Ilikuwa ni sharti aje (Marekani)", Liu alisema. "Lakini baadaye hakutaka kufanya hivyo".

Kompyuta na upelelezi wa binadamu

Upelelezi dhidi ya raia wa China wanaoishi nje ya nchi unakuja kwa namna nyingi: Kutoka majaribio ya uvamizi katika barua pepe zao na vifaa, kwa uwekaji wa mawakala binadamu ndani ya jamii zinazowazunguka au mashirika ya kigeni.

Njia za kielektroniki hutumiwa mara nyingi "kuwezesha" upelelezi wa binadamu.

"Unaweza kupeleleza mtu mtandaoni na kupata wazo la mawasiliano yao", alisema Christopher Johnson, mchambuzi mkuu wa zamani wa China katika CIA. "Basi labda unaweza kuwa karibu na watu hao na kitu kimoja kikachochea kingine".

Beijing inawashambulia wapinzani kama Liu kwa sababu inaamini kuwa ni sehemu ya "vita vya masimulizi ya kimataifa" kati ya China na nchi za Magharibi, Johnson aliongeza.

Wale wanaopaza sauti zao hadharani dhidi ya utawala wa nchi hiyo huenda wakakwamisha juhudi za China za kujiwasilisha katika mtazamo chanya.

Hii imechukua "umuhimu mpya katika miaka miwili iliyopita", alisema.

Upande wa simulizi yako

"Wanatumia msemo wa kitambo wa Waumaksi wa 'nguvu ya hotuba'. Ni wazo ambalo wao wenyewe wanapaswa kusimulia habari za China kupitia propaganda zao wenyewe ".

Serikali ya China haikujibu ombi la kutoa maoni yake kuhusiana na suala hili. Wakati Ziburis aliposhtakiwa mwezi Machi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Beijing Zhao Lijian aliituhumu Marekani kwa "udhalilishaji usio na msingi na kuichafulia sifa China.

Hata hivyo, maafisa wa upelelezi wa sasa na wa zamani wa Marekani wamekuwa wakionya juu ya kampeni kubwa ya upelelezi wa Kichina nchini Marekani.

Katika hotuba yake mapema mwaka huu, Mkurugenzi wa FBI John Wray alisema upelelezi wa Kichina nchini Marekani ni "ujasiri usio na aibu" kwa namna ambayo haijawahi kutokea.

Hii inamaanisha kuwa, uongozi wa Biden unaweka wazi ushindani uliopo kati ya Marekani na China katika mapambano ya kimataifa kati ya nchi za kidemokrasia na yenye mamlaka ya mtu mmoja,Johnson alisema.

Kesi moja kila baada ya masaa 12

Kwa mujibu wa shirika la ujasusi la Marekani (FBI), ofisi hiyo inafungua kesi mpya inayohusiana na ujasusi nchini China kila baada ya saa 12. Hadi Februari, zaidi ya kesi 2,000 zilikuwa zimefunguliwa.

Pamoja na hili, Johnson aliziita juhudi za Marekani kuzuia upelelezi wa Kichina "kutokomezwa".

"Wako tayari kuweka juhudi za kuing 'oa zaidi ya hapa tulipo ili kujaribu kuizuia", alisema.

Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) linakadiria kwamba kuna "mamia" ya wapinzani nchini Marekani ambao China inatarajia kuwalenga kama sehemu ya kampeni inayozidi kuwa ya fujo ya kulipiza kisasi cha kibinafsi na kisiasa.

"Malengo mengi ni wakazi wa kudumu au raia wa asili. Watu wenye haki na ulinzi muhimu chini ya sheria ya Marekani", alisema Mkurugenzi Wray.

"Sijali"

Kwa upande wake, Liu, alisema hafikirii jitihada za kumpeleleza zitakoma. Jaribio la hivi karibuni zaidi, hata hivyo, lilikuwa na utata wa zaidi.

Wakati wa wito wa FBI, Alyssa Liu, ambaye alikuwa ameweka maudhui kuhusu kitendo cha China dhidi ya kabila la Uyghur la watu wachache kwenye mitandao ya kijamii, alikuwa na uhakika wa kusafiri kuelekea Beijing.

Liu alikiri kwamba alikuwa na "wasiwasi mkubwa" kwa usalama wake, lakini alichagua kutokumwambia wakati huo. "Sikutaka aende China na mzigo mzito begani mwake", alisema.

"Nilitaka kwenda kufurahia uzoefu wa Olimpiki". Mwaka mmoja baadaye, alisema kuwa hatashangazwa kama FBI ingewasiliana naye tena, ingawa ana matumaini kuwa "hatakiwi kufanya hivyo tena".

"Nilijifunza tabia kama mtu wa kawaida. Wao (serikali ya China) wanaweza kufanya chochote wanachotaka, siwezi kuwazuia. Sijali ", alisema.

"Nitaendelea kuzungumza juu ya baadhi ya tabia na aina yoyote ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Na hapana yeyote awezae kunizuia.