Miaka 10 tangu ajali ya ndege ya Malaysia, familia bado ziko kwenye fumbo

    • Author, Jonathan Head
    • Nafasi, BBC

Tarehe 8 Machi 2014, saa moja baada ya safari ya usiku kutoka Kuala Lumpur kwenda Beijing kuanza, rubani alisema usiku mwema kwa wasimamizi wa anga wa Malaysia.

Ndege hiyo aina ya Boeing 777, iliyokuwa na abiria 227 na wafanyakazi 12, ilikuwa karibu kuingia anga ya Vietnam.

Kisha ilibadilisha mwelekeo ghafla, na mawasiliano yote ya kielektroniki yalikatika. Ilirudi nyuma, kurudi Malaysia, na kisha ikaelekea kusini mwa Bahari ya Hindi mbali hadi ikadhaniwa kuwa imeishiwa na mafuta.

Ushahidi pekee wa ndege hiyo kurudi nyuma ni kutoka kwa rada ya kijeshi ya Malaysia na Thailand, ambazo ziliiona ndege hiyo ikiruka magharibi katika peninsula ya Malay.

Kampuni ya Uingereza, Inmarsat, iligundua eneo ndege ilipo kila baada ya saa moja kwa mara tano kupitia satelaiti wakati MH370 ilipokuwa ikielekea kusini. Masiliano mengine yote kwenye ndege yalikuwa yamezimwa.

Operesheni kubwa na ya gharama kubwa zaidi ya utafutaji kuwahi kufanyika ilidumu kwa miaka minne lakini haikuweza kupata mtu yoyote aliyekuwemo kwenye ndege hiyo.

Maelfu ya wataalamu wa masuala ya bahari, wahandisi wa anga na mafundi walitumia taarifa za mwisho za ndege hiyo, wakijaribu kukokotoa mahali ilipoishia safari yake.

Pia unaweza kusoma

Familia ya Eryou, China

Kwa familia za wale waliokuwemo hii imekuwa miaka 10 ya huzuni isiyoweza kuepukika, ikipambana ili kuendeleza msako, ili kujua ni nini hasa kilitokea kwa MH370, na kwa nini.

Ndege ya Malaysia Airlines MH370 ilipotea na mtoto wa Li Eryou, aitwaye Yanlin akiwa na abiria wengine mwongo mmoja uliopita.

Yeye na mke wake, Liu Shuangfeng – ni wakulima kutoka kijiji kusini mwa Beijing, China – wanapata tabu kuelewa moja ya siri kubwa katika historia ya usafiri wa anga.

Li amezunguka dunia nzima kuunga mkono kampeni hiyo. Anasema ametumia akiba yake kusafiri hadi Ulaya na Asia, na kwenye fukwe za Madagascar, ambapo baadhi ya mabaki ya ndege iliyotoweka yamepatikana.

Anakumbuka alipiga kelele kwenye Bahari ya Hindi, akimwambia Yanlin, yupo pale ili kumrudisha nyumbani: “Nitaendelea kusafiri hadi mwisho wa dunia kumtafuta mwanangu,” anasema.

Wanandoa hao, ambao sasa wana umri wa zaidi ya miaka 60, wanaishi katika sehemu ya mashambani ya mkoa wa Hebei nchini China. Sehemu kubwa ya mapato yao yalilipia masomo ya watoto, na hawakuwahi kuwa na pesa za kusafiri.

Yanlin alikuwa mtu wa kwanza katika kijiji chao kwenda chuo kikuu, na wa kwanza kupata kazi nje ya nchi, akifanya kazi nchini Malaysia katika kampuni ya mawasiliano.

Alikuwa akirejea China ili kupata viza wakati ndege hiyo ilipotoweka. "Kabla ya tukio hili kutokea, hatukuwahi hata kufika katika mji wa karibu wa Handan," Li anasema.

Sasa ni wasafiri wenye uzoefu, wamekwenda tena Malaysia kuadhimisha mwaka wa 10 pamoja na familia nyingine.

Yanlin alikuwa mmoja wa abiria 153 raia wa China kwenye ndege hiyo. Wazazi wake ni miongoni mwa familia zipatazo 40 za China ambazo zimekataa fidia kutoka serikali ya Malaysia.

Badala yake wamefungua kesi za kisheria nchini China dhidi ya shirika la ndege, watengenezaji wa ndege na wahusika wengine.

Familia ya Anne, Uingereza

Grace Nathan alikuwa akifanya mitihani yake ya mwisho katika fani ya sheria nchini Uingereza wakati MH370 ilipotoweka.

Mama yake Anne alikuwa kwenye ndege. Nathan sasa ni wakili na anafanya kazi nchini Malaysia, na mama wa watoto wawili wadogo.

Katika tukio la kumbukumbu huko Kuala Lumpur, akiwa ameshika picha ya mamake akitembea siku ya harusi yake, anakumbuka kuukosa ushauri wa Mama yake alipokuwa akipitia vipindi viwili vizito vya mimba zake mbili.

Msako wa Ndege

Kwenye tukio hilo kulikuwa na vipande vichache vya ndege, ushahidi pekee kuwahi kupatikana kutoka ndege hiyo. Kulikuwa na sehemu za bawa la ndege, zenye kutu kutokana na kuzama kwa muda mrefu baharini.

Katika umati huo alikuwepo Blaine Gibson, ambaye alipata vipande vingi vya MH370 kuliko mtu mwingine yeyote.

"Nilipohudhuria hafla ya kuadhimisha mwaka mmoja nilijifunza kwamba hapakuwa na msako uliopangwa kwenye fukwe. Walikuwa wakitumia mamilioni ya dola kutafuta chini ya maji.

Kwa kuwa hakuna mtu aliyekuwa akifanya hivyo, nilisema mimi nitatafuta kwenye fukwe."

Alitafuta kwa muda wa mwaka mmoja, kwenye fukwe za Myanmar hadi Maldives, kabla ya kupata kipande chake cha kwanza, kwenye fukwe za Msumbiji.

Wakati huo kipande kingine kikubwa, kilikuwa tayari kimepatikana kwenye Kisiwa cha Reunion, na kuthibitisha kwamba MH370 ilianguka katika Bahari ya Hindi.

Sehemu ambazo zilipatikana zote ziliokotwa miezi 16 au zaidi baada ya MH370 kutoweka, vipande vilisombwa hadi katika fukwe mbalimbali za Afrika Mashariki.

Msako huo uliohusisha meli 60 na ndege 50 kutoka nchi 26 ulianza Machi 2014 hadi Januari 2017. Ulianza tena mapema 2018 kwa miezi mitano na kampuni ya kibinafsi ya Marekani iitwayo Ocean Infinity, ikitumia ndege zisizo na rubani za chini ya maji kukagua eneo la bahari.

Ocean Infinity ilichunguza eneo la kilomita 112,000, mwaka 2018. Ilijumuisha maeneo yenye changamoto nyingi, kama vile korongo zenye kina kirefu cha maji.

Uvumi juu ya kilichotokea

Data ya rada na satelaiti na wataalamu wengi wanakubali kwamba ndege hiyo iliendelea kuruka kusini, na maelezo yanayokubalika ni kwamba mtu aliirusha huko makusudi.

Katika makala mpya ya BBC, "Why Planes Vanish", wataalam wawili wa masuala ya anga wa Ufaransa, kwa kuzingatia ndege hiyo kugeuza ghafla - wamehitimisha kuwa hilo lingeweza tu kufanywa na rubani mwenye ujuzi na uzoefu.

Kuna nadharia zingine - kwamba kila mtu kwenye ndege alizimia kutokana na ukosefu wa oksijeni, baada ya mfadhaiko usiojulikana, au janga la moto au mlipuko wa ghafla ulikata mawasiliano na kuwalazimisha marubani kurudi nyuma.

Lakini uwezo wa ndege hiyo kuendelea na safari, kuelekea kusini kwa saa saba, kunafanya nadharia hiyo isiwe rahisi kutokea.

Hata hivyo wazo kwamba mmoja wa marubani alirusha ndege hiyo kimakusudi na abiria wake wote kwenda baharini pia ni gumu kukubalika. Hakuna rubani mwenye historia inayoweza kueleza kitendo kama hicho.

Tangu mwanzo serikali ya Malaysia ilikosolewa na familia. Kwanza kushindwa kuchukua hatua za haraka kwenye ufuatiliaji wa rada ya kijeshi. Na baadaye, kwa kusita kwake kuidhinisha utafutaji zaidi, baada ya operesheni ya mwisho na Ocean Infinity kumalizika katikati ya 2018.

Kampuni hiyo imejitolea kuendelea na utafutaji bila malipo, lakini inahitaji idhini ya serikali.

Familia hizo zinasema zimetiwa moyo na ahadi za hivi karibuni zilizotolewa na waziri wa uchukuzi wa Malaysia aliyeahidi kuisaka ndege hiyo. Lakini wanabaki kuwa waangalifu. Kwani wamepewa matumaini makubwa hapo awali bila utekelezaji.

Katika tukio hilo la kumbukumbu ubao mkubwa ulikuwa umewekwa, watu wameandika jumbe za matumaini, za huruma, au za huzuni.

Li alipiga magoti kumwandikia Yanlin ujumbe kwa herufi kubwa za Kichina, kisha akaketi huku akilia, akiutazama.

"Mwanangu, ni miaka 10. Mama na baba yako wako hapa kukurudisha nyumbani. Machi 3, 2024."

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah