Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kombora la Iran la Fattah 'linalopenya' mifumo ya Ulinzi wa anga Israel
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi nchini Iran IRGC lilitangaza jana usiku kuwa limetumia kombora la "Fatah hypersonic" katika shambulio la kombora dhidi ya Israeli.
Hii inaonekana kuwa mara ya kwanza kwa IRGC kutumia makombora ya Fatah tangu kuanza kwa vita vya Israel na Iran siku ya Ijumaa, Juni 13.
Walinzi wa Mapinduzi waliielezea Fatah kama kombora "lisiloweza kudhibitiwa" ambalo lilimepenya ngao ya ulinzi wa makombora ya Israeli.
Jeshi la Israel pia limethibitisha kuwa makombora ya Iran yaligonga maegesho ya magari mjini Tel Aviv.
IRGC ilikuwa imeshambulia Israel kwa makombora ya Fatah-1 pekee wakati wa Operesheni "Odeh Sadeq II" mnamo Oktoba 1, 1403.
IRGC ilisema wakati huo kwamba kombora hili liliweza "kuharibu rada za ngao za ulinzi za kombora la Paykan 2 na 3 za Israeli."
Je! tunajua nini kuhusu kombora la Fatah, ambalo Walinzi wa Mapinduzi wanasema lina teknolojia ya "hypersonic" au "supersonic" na ambalo kuna mazungumzo mengi na uvumi juu yake?
Fatah, jina lililochaguliwa na Kiongozi mkuu wa kidini nchini Iran
"Fattah", ambalo ilipewa jina na Ali Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu, lilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1402 kama kombora la hypersonic katika makundi mawili: Balestiki na cruise.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi linasema kuwa kombora la Fatah linaweza kwenda umbali wa kilomita 1,400 na lina uwezo wa kupita katika mifumo yote ya ngao ya makombora na kuiharibu pia.
Iran inayaita makombora ya umbali wa zaidi ya kilomita 1,300 "Israeli -killing au muuaji wa Israel" , hivyo baada ya kufichuliwa kwa kombora la balestiki la Fatah-1, bango lenye kauli mbiu "sekunde 400 kufika Tel Aviv" liliwekwa katika uwanja wa Fasaltin mjini Tehran ili kutishia Israel.
Fatah-1 ina kichwa kigumu cha injini ya duara chenye mafuta na IRGC inasema kina "uwezo wa kuelekea upande wowote."
Fatah ni kombora la mafuta ambalo toleo lake la balestiki hufikia kasi ya Mach 13 hadi 15 kabla ya kugonga shabaha yake. Mach 15 ni sawa na kilomita 5 kwa sekunde.
Vyombo vya habari vya Iran, ikiwa ni pamoja na Tasnim, viliandika kwamba Fatah-2 "ina uwezo wa kuruka chini chini sana na pia inaweza kubadilisha mkondo wake mara kadhaa wakati wa safari."
Kombora la kusafiri la Fatah-2 lilizinduliwa wakati wa ziara ya Kiongozi Mkuu Ali Khamenei katika Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga na Teknolojia cha Ashura chenye uhusiano na Walinzi wa Mapinduzi, lakini hakuna taarifa sahihi inayopatikana kuhusu masafa ya kombora hilo.
Ingawa Iran ilianzisha makombora ya Fatah kutishia Israeli, haikutumia katika shambulio lake la kwanza dhidi ya Israeli mwezi Aprili 13, 2024.
Je, kombora la Fatah lina teknolojia ya "hypersonic"?
Wakati Walinzi wa Mapinduzi wakisisitiza kwamba wamepata kizazi cha makombora ya hypersonic, baadhi ya wataalam hawakuchukulia kombora la Fatah kuwa kombora la hypersonic na wana shaka juu yake.
Fabian Heinz, mtafiti wa masuala ya ulinzi na uchambuzi wa kijeshi na mtaalamu wa makombora ya balestiki katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, aliiambia BBC kwamba teknolojia ya makombora ya balistiki ilianza tangu Vita vya Pili vya Dunia na kwamba makombora hayo yanafikia kasi ya hypersonic, mara tano ya kasi ya sauti, wakati fulani kwenye njia yao.
Lakini hypersonic katika muktadha wa makombora haimaanishi kasi tu, anasema Bw. Haynes: "Tunapozungumza juu ya silaha za hypersonic, tunazungumza juu ya silaha zinazosafiri mara tano ya kasi ya sauti na bado zinapita kwenye angahewa ya Dunia, na kuzifanya kuwa ngumu sana kuzilenga. Hiyo ndiyo tunayomaanisha kwa silaha za hypersonic."
Bw. Haynes anasema kwa aina hii ya kombora, inaweza kuwa bora kutumia neno "ujanja wa hypersonic."
Mtaalamu huyo wa makombora aliiambia BBC kwamba Iran bado haina silaha zinazojulikana katika nchi za Magharibi kama vile silaha za hypersonic, kama vile vichwa vya makombora ya balestiki au makombora ya hypersonic cruise, lakini kuna uwezekano kwamba inafanyia kazi teknolojia hizi.
Taasisi ya Huduma ya Kifalme ya Uingereza (RUSI) pia ilibainisha katika ripoti iliyochunguza shambulio la kombora la Iran dhidi ya Israel mwaka jana kwamba kombora la Fatah-1 linapaswa "kuainishwa vyema kama kombora la balistiki badala ya kombora la hypersonic."
Hata hivyo, Amir Ali Hajizadeh, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Wanaanga wa IRGC, alisema katika hafla ya kuzindua kombora la Fatah, "Kombora hili lina kasi kubwa na linaweza kuruka ndani na nje ya anga," na "haliwezi kuharibiwa na kombora lolote."
Hata baadhi ya vyombo vya habari vya Iran, kama vile Khabar Online, vikinukuu maneno ya Amir Ali Hajizadeh, kamanda wa Kikosi cha Wanaanga wa Mapinduzi, vilidai kuwa ni Urusi, China na Iran pekee ndizo zinazoweza kutumia makombora ya hypersonic na kwamba Marekani haina teknolojia hii, wakati Marekani ina makombora ya juu zaidi ya hypersonic.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Galant alisema katika kujibu uundaji wa makombora ya nyuklia ya Iran: "Nimesikia kwamba maadui zetu wanajisifu kuhusu silaha wanazozitengeneza. Tuna jibu bora kwa maendeleo yoyote, iwe ya ardhini, angani au baharini."
Miezi minne baada ya kuzindua Fatah-1, IRGC ilizindua kombora la Fatah-2. Fatah-2 inasemekana kuwa kizazi cha makombora ya kusafiri kwa umbali wa kilomita 1,500.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla