Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kesi ya kumuondoa Gachagua inasikilizwa Seneti
- Author, Basillioh Rukanga
- Nafasi, BBC News, Nairobi
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Bunge la Seneti nchini Kenya limeanza hatua ya mwisho ya kumuondoa mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Wiki iliyopita wabunge walipiga kura katika Bunge la Kitaifa kuidhinisha kuondolewa kwake madarakani, na hivyo kuweka mazingira ya kusikilizwa kwa kesi ya siku mbili katika Seneti ambayo itaamua iwapo atamtimua au la.
Naibu Rais anakabiliwa na mashtaka 11 yakiwemo ufisadi, kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu serikali - yote anayakanusha.
Mchakato huo unafuatia mzozo wake wa hivi majuzi na Rais William Ruto, ambaye amekuwa kimya kuhusu suala hilo.
Kesi ya Gachagua inaendeshwa mbele ya bunge zima la Seneti baada ya kuachana na mchakato wa kuunda kamati ya watu 11 kuchunguza mashtaka hayo.
Kesi hiyo ilianza asubuhi na baada ya vikao vya awali, mashtaka yalisomwa kwa naibu rais ambaye alisimama kabla ya 12:00 saa za ndani (09:00 GMT).
Ameendelea kusimama huku akisomewa mashtaka hayo, huku akikana mashitaka hayo
Wachambuzi wanatarajia kuondolewa kwa Naibu rais kutazingatiwa kwani maseneta wa chama tawala huenda wakaungwa mkono na wale wa upinzani kama ilivyofanyika wakati Bunge la Kitaifa lilipopiga kura kuhusu kesi hiyo.
Ushahidi wa Bunge la Kitaifa dhidi ya Gachagua, wakiwemo mashahidi wowote, utawasilishwa baadaye na kuchunguzwa kwa saa tatu na kufuatiwa na mahojiano mengine ya saa mbili.
Siku ya Alhamisi, kesi itaendelea kushughulikia ushahidi na mashahidi kutoka upande wa Gachagua hadi alasiri.
Mwishoni mwa mchakato huo jioni, maseneta watajadili hoja hiyo kwa takriban saa mbili na kisha kupiga kura - iliyopangwa kufanyika Alhamisi usiku kutoka 20:30 saa za ndani.
Seneti inaweza kuamua kurefusha mchakato hadi Ijumaa, siku ya mwisho ambayo inaweza kuongeza suala hilo kisheria.
Thuluthi mbili ya wajumbe 67 wa Seneti lazima waidhinishe hoja ya Gachagua kuondolewa afisini.
Iwapo hilo litatokea na kuondolewa kwake madarakani kupitishwa na seneti, atazuiwa kushika wadhifa wa umma.
Anatarajiwa kupinga mashtaka hayo katika mahakama iwapo yatapitishwa.
Naibu rais amefanya majaribio kadhaa bila kufanikiwa kusitisha mchakato wa kumshtaki, huku takriban kesi 26 zikiwasilishwa mahakamani kufikia sasa.
Siku ya Jumanne, jaji aliamua kwamba mahakama haitaingilia kati na kusema kuwa Seneti inapaswa kuendelea na mamlaka yake ya kikatiba.
Na kabla ya mchakato huo kuanza Jumatano, majaji watatu pia ilikataa ombi kama hilo.
Baadhi ya sababu za kushtakiwa kwa Gachagua ni pamoja na shutuma kwamba alipata mali ya thamani ya shilingi bilioni 5.2 za Kenya ($40m; £31m) katika kipindi cha miaka miwili tangu awe naibu wa rais - inayodaiwa kupatikana kwa njia za ufisadi.
Ameeleza, ikiwa ni pamoja na wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake Bungeni, kuwa mali nyingi zinazozungumziwa ni mali ya marehemu kaka yake.
Naibu rais ni mfanyabiashara tajiri kutoka eneo la Mlima Kenya lenye idadi kubwa ya wapiga kura.
Katika muda wa miaka mitano pekee, alipanda kutoka kuwa mbunge kwa mara ya kwanza na kuwa wa pili katika uongozi wa Kenya, baada ya Ruto kumteua kama mgombea mwenza wake katika uchaguzi wa Agosti 2022.
Wakati huo, alikuwa akipambana na madai ya ufisadi mahakamani ambayo yalitupiliwa mbali baada ya kuwa naibu wa rais.
Kesi yake ya kuondolewa madarakani imetawala mijadala ya Wakenya wengi na vyombo vya habari katika wiki za hivi majuzi.
Baadhi wanahisi suala hilo ni la kisiasa na limeondoa macho ya Wakenya kutoka kwa masuala ya kiuchumi ya Wakenya walio wengi wanaotatizika kutokana na gharama ya juu ya maisha.
Mnamo Juni Wakenya waliokuwa na kinyongo walifanya maandamano makubwa kupinga nyongeza ya ushuru katika hatua ambayo ilifichua mpasuko mkubwa kati ya Ruto na Gachagua.
Gachagua sasa anadaiwa kuhujumu utendakazi wa mashirika ya usalama kufuatia matamshi aliyotoa wakati huo akilaumu shirika la kijasusi.
Pia unaweza kusoma:
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Yusuf Jumah