Mimi sio mjinga, nimeamua kuzungumza-mwanamke aliyelaghaiwa kimapenzi kwa miaka tisa

Muda wa kusoma: Dakika 4

Amber Sandhu na Manish Pandey

BBC Asian Network News

th

Chanzo cha picha, NETFLIX

Maelezo ya picha, Kirat Assi alilaghaiwa kimapenzi kwa karibu miaka tisa

Yote ilianza na ombi la urafiki.

Kirat Assi alifikiri amepata 'dhahabu' wakati Bobby, daktari mtanashati wa magonjwa ya moyo, alipowasiliana naye mwaka wa 2009.

Hakuwa mgeni kabisa. Wawili hao wote walitoka jamii ya Sikh ya London magharibi na walikuwa na marafiki sawa.

Kwa hivyo, Kirat alikubali, na mazungumzo yake ya mtandaoni yalikua mazungumzo ya kina kabla ya kugeuka na kuwa hadithi ya mapenzi.

Wawili hao waliingiana zaidi katika maisha ya kila mmoja wao lakini hawakuwahi kukutana, hata baada ya miaka mingi ya mawasiliano.

Bobby alitoa visingizio vya ajabu zaidi. Alikuwa na kiharusi. Alikuwa amepigwa risasi. Alikuwa ameingia kwenye mpango ulinzi wa mashahidi.

Hadithi ndefu, ingawa, ziliungwa mkono na mtu wa karibu wa Bobby - au hivyo ndivyo Kirat alivyofikiria.

Kwa kweli, alikuwa mwathirika wa mpango kabambe sana na wa kutisha wa kulaghaiwa kimapenzi katika mtandao au Catfishing kwa Kiingereza .

Baada ya miaka tisa, visingizio vilipopungua, hatimaye Kirat alikutana uso kwa uso na Bobby.

Lakini hakumtambua mtu aliyekuwa mbele yake.

Mtu ambaye alikuwa akimtumia ujumbe alikuwa binamu yake wa kike, Simran, ambaye ndiye alikuwa mhusika wa kila kitu nyuma ya pazia.

Akikumbuka sasa, Kirat anajiuliza: "Niliwezaje kuwa mjinga sana?"

Unaweza Pia Kusoma

Hadithi ya kushtua ya Kirat ilikuwa maarufu kwa podcast 'Tortoise' mnamo 2021. Unaweza kusikiliza hiyo kwenye BBC Sounds hapa . Sasa, miaka mitatu baadaye, Netflix hivi karibuni imetoa makala inayosimulia alichokipitia

Anasema kwamba kusimulia hadithi yake kumewasukuma wengine kuuliza swali lile lile: "Mtu anawezaje kulghaiwa na jambo kama hilo?"

Pia imechochea matusi kutoka kwa baadhi ya watu mtandaoni.

"Kwa watu ambao bado wanaweza kudhani mimi ni mjinga. Hiyo ni sawa, unaruhusiwa maoni kutoa yako," anaiambia BBC Asian Network News.

Lakini Kirat anasema watu hawapaswi kushikilia dhana fulani - na kupinga dhana hizo ndiyo sehemu iliyomsukuma kusimulia hadithi yake.

“Mimi sio mjinga, si bubu, mimi ndiye niliyeamua kuongea.

"Mimi ndiye niliyejiweka kwenye mstari wa mbele natumai wengine watajitokeza," anasema.

Swali jingine ni: Kwa nini mtu ambaye amedanganywa kwa njia hii ajiweke hadharani?

th

Chanzo cha picha, NETFLIX

"Tuna majukumu kwa jamii yetu"

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kirat, ambaye anatoka asili ya Kipunjabi, anasema kuzungumza wazi ilikuwa muhimu kwa sababu alitaka kupinga unyanyapaa katika jamii ya watu wa Asia Kusini.

"Tunaogopa sana kufunguka kuhusu masuala haya," anasema.

"Kwa sababu ya jinsi jamii itakavyoonekana na jamii pana, waathiriwa katika jamii zetu wanaendelea kuteseka."

Kirat anasema jibu la baba yake kwa hadithi yake ni mfano mzuri wa kile anachomaanisha.

"Hataki kujua kilichotokea," anasema.

"Kwa sababu kukabiliana na kile kilichotokea, na jinsi ilivyokuwa hali ya kutisha, litakuwa jambo chungu.

"Ninampenda baba yangu na najua baba ananipenda," anasema, na kuongeza: "Ni aina tofauti ya maadili ambayo amelelewa nayo."

Kirat anasema hajazungumza moja kwa moja na "Bobby halisi" kuhusu kile kilichotokea, na analaumu kusita huku kwa kile anachosema ni woga wa jamii kuwa na mazungumzo magumu.

Anashangaa kama masaibu yake yangekuwa sawa ikiwa angetoka kwenye historia nyingine.

"Ningekuwa nikifanya maamuzi tofauti," anasema.

"Kwa sababu tuna majukumu kwa jamii yetu. Una shinikizo la familia."

TH

Chanzo cha picha, NETFLIX

Maelezo ya picha, Kirat anahisi kuna hofu katika jamii ya Asia Kusini kuzungumza kuhusu masuala hatarishi

'Sibebi mawazo ya mwathirika'

Licha ya athari mbaya kwa kusimuliwa tena kwa Sweet Bobby, Kirat anasema afadhali apambane na maswali wazi wazi.

"Ikiwa utaniona, usiogope kunikaribia," anasema.

"Na ikiwa unataka kusema jambo ambalo linaweza kuwa na utata kwangu, ni sawa.

"Hebu tufanye majadiliano juu yake," anasema.

Kirat alipoulizwa ikiwa kuzungumza na podcast au watayarishaji wa filamu kumempa hisia ya kufunga awamu kuhusu masaibu yake, hana uhakika wa hilo.

Simran alikataa ofa za kushirikishwa katika filamu hiyo, ambapo inachezwa na mwigizaji.

Kirat alifaulu hatua za kishria dhidi ya binamu yake, akipokea fidia na kuombwa msamaha mwishoni mwa kesi.

Taarifa kutoka kwa Simran iliyojumuishwa kwenye onyesho hilo inasema: "Suala hili linahusisha matukio ambayo yalianza alipokuwa msichana wa shule. Analichukulia kuwa suala la faragha na anapinga vikali kile anachoeleza kuwa tuhuma nyingi zisizo na msingi na zenye madhara."

Kirat anasema Simran hajakabiliwa na mashtaka yoyote ya jinai, na anataka awajibike.

"Siko sawa na mtu huyo kuwa huko nje," anasema Kirat.

Kuna swali lingine ambalo hajajibu: Kwa nini?

Kirat hafikirii kuwa atawahi kujua ni nini kilichochea kampeni dhidi yake.

"Nadhani nimekata tamaa kwa muda mrefu," anasema.

"Kiwango ambacho mtu huyo alienda, huwezi kuhalalisha alichofanya.

"Sielewi kwa nini hukuacha ... ni nini kilikupa raha ya kusikia mtu akiwa na maumivu."

Lakini kutokuwa na majibu hakumzuii kuendelea na maisha, ikiwa ni pamoja na kuchumbiana tena.

"Ninafanya kazi kwa bidii, zaidi kuliko ninavyopaswa kufanya hivi sasa ili kujenga upya maisha yangu na kazi yangu," anasema.

"Sibebi mawazo ya mwathiriwa karibu nami. Sitaki kuwa mtu huyo.

"Nitaendelea kufanya kazi kufikia malengo na ndoto zangu."

Sweet Bobby: My Catfish Nightmare inapatikana Netflix.

Unaweza Pia Kusoma

Imetafsiriwa na Yusuf Jumah