Waridi wa BBC: Mazungumzo binafsi yalivyogeuka mazungumzo kwa wengi

M

Chanzo cha picha, BMK

Maelezo ya picha, Brenda Msangi, Mkurugenzi mtendaji mkuu hospitali ya CCBRT
    • Author, Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC Dar es Salaam

Nilikuwa mdogo mdogo sana hata shuleni walikataa kuniandikisha wakati umri wangu wa kwenda shule ulikuwa umewadia, mpaka mama yangu aliposisitiza sana kuwa waniache tu niende shule na wataniandikisha watakapoona muda unafaa, maana hata nilikuwa siwezi kukaa vizuri katika madawati kwa sababu ya kimo changu.

Ila baada ya kufanya vizuri katika masomo yangu, niliandikishwa baada ya miezi sita.

Na kwa bahati iliyoje nilianza kuwa kiongozi tangu nikiwa shule ya msingi.

Nilipenda masomo ya sayansi ingawa sikuwahi kuwa na ndoto ya kuwa daktari au kutamani kuwa daktari.

Nilipata ufadhili wa kusoma Uingereza na niliibuka kuwa mwanafunzi kinara katika mwaka niliosoma.

Wakati nasoma, ndiyo ule wakati ambao kama nasomeshwa na kijiji.

'Dear Girl Child' Brenda Msangi Kinemo

Wakati ninasoma Shahada yangu ya pili, nilikuwa nina majukumu tayari tofauti na ile ya kwanza.

Nilikuwa mama, mke na mkurugenzi. Siku nilipomaliza kazi yangu ya shule, ‘course work’ nilipotuma tu kwenye barua pepe majira ya saa sita usiku, nilijitathmini jinsi nilivyokuwa nimechoka sana na kuhisi kushindwa kuendelea yaani nilihisi kukata tamaa.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini kulikuwa kama kuna sauti ilikuwa ikiniambia kuwa kuna mtu anajisikia kama ninavyojisikia, ni vyema ukaongea naye. Nikachukua simu yangu na kwenda kwenye mtandao wa Instagram na kuanza kuongea na huyu binti. Yalikuwa mazungumzo yangu binafsi mimi kama binti.

Nilikuwa najiongelesha na kujijibu mimi mwenyewe.

Niliandika ‘Najua unapitia mambo mengi lakini kila kitu kinawezekana …

Ilipofika asubuhi nilikuta ujumbe mwingi sana, wa watu wengi kuona naongea nao. Mpaka mume wangu alishangaa simu yangu kupata ujumbe mwingi alfajiri.

Wengi waliandika dada Brenda ulikuwa unaongea na mimi kabisa….Hapo ndipo safari ya ‘Dear Girl Child’ ilipoanza.

Nikafungua kurasa maalumu kwa ajili ya mazungumzo ya namna hiyo na kuita chapisho hilo 'Dear Girl Child BMK'

Kila mtu alikuwa anaona mazungumzo ni yake, wakati yalikuwa mazungumzo yangu binafsi na nilidhani niko peke yangu katika hali ya kukata tamaa, lakini kumbe tuko wengi tunaopitia changamoto kama zangu. Niliona kuwa sehemu ya kumkumbusha mtu na kumpa ujasiri.

Niliona ninaweza kutoa muongozo kwa wengine kwa namna hiyo na hata kuna wakati ilinibidi niwe mkali ili niweze kueleweka. Na sasa ninawafikia karibu mabinti elfu kumi ingawa vijana wa kiume pia wanafuatilia machapisho yangu.

Mimi na maongezi ya nafsi yangu nimeweza kuhamasisha wengine na kuwavutia kusonga mbele.

mm

Chanzo cha picha, BMK

Malezi yanasaidia kukuza ujasiri

Nimelelewa na wazazi ambao walitueleza kuwa vitu au mali unazoziona hapa, si zetu na zitabaki nyumbani lazima utafute za kwako kwa kusoma.

Nyumba nyingine ni kawaida kuona mama akichapwa vibao, au baba akifoka jambo ambalo sikushuhudia nikiwa nakua, lakini kwa wengine ni jambo ambalo wanakutana nalo.

Mfano, mtoto wa kiume anakuwa katika mazingira ambayo akila chakula hatoi sahani yake mezani, lakini unamkuta ameoa mke ambaye amelelewa kwa misingi ya kuwa mtu akila, lazima atoe chombo chake haijalishi ni wa kiume au wa kike.

Kiongozi anaanzia nyumbani, malezi yana nafasi kubwa sana katika jamii.

Binafsi nimelelewa katika mazingira ya maombi na kumtumaini Mungu ni muhimu.

Huwezi kujijenga bila kupitia changamoto

Kupitia nyakati ngumu au changamoto ni hali ya kawaida. Tunajengwa na nyakati ngumu, ninaamini kuwa huwezi kuwa na misuli bila changamoto na hatua hii niliyofika ni changamoto ndio zimenifikisha hapa katika safari yangu.

Ukitaka kupita hali fulani bila changamoto, utafika au utaendelea vizuri tu lakini swali ni je unataka kufika wapi?

Ni vyema kutoka katika mazingira uliyoyazoea na kama haupo tayari basi ngumu kusogea, na furaha yako itategemea kiwango hicho ulichokubaliana nacho. Ni vyema kuwa na uthubutu wa kutaka kufika sehemu fulani.

Ni vyema kupambana maana mpaka leo mimi ni mkurugenzi na changamoto ninazo lakini huwa ninajiuliza Brenda ni jambo gani unataka kujifunza?

Tuzo nyingi ulizopokea zina maana gani?

m

Chanzo cha picha, BMK

Ninamshukuru Mungu kupata tuzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Tuzo zina maana kuu mbili katika maisha yangu:

Mosi inanionesha jambo ambalo nimelifanya kuonekana kuwa limepokewa katika jamii na kutokana na hiyo, ninapata moyo na nguvu wa kuendelea na safari yangu ya kutaka kufika ninapotaka kufika.

Pili, si kama ninapata tuzo kwa juhudi zangu binafsi ninaamini kuwa kuna neema ya Mungu.

Hivyo katika kujitafakari ninarudisha nini kwa jamii, kwa hii neema ndiyo inakuja machapisho haya ya 'Dear Girl Child'

Sio jambo ambalo ni lazima kulifanya, licha ya kuwa linachukua muda wangu mwingi

Lakini naona nimepewa nafasi hii muhimu ili niwavute wengine. Huu ujuzi ambao ninao, nina wajibu wa kuwshirikisha wengine.

Kwa asili wanawake tumeumbwa kuwa viongozi, kiongozi wa kwanza kumfahamu ni mama yangu. Hata kama jina la uongozi linaweza kuwa halipo lakini majukumu tuliyonayo ni uongozi.

Uongozi ni ushawishi

Kama unaamini una ushawishi basi ujue wewe ni kiongozi.

Sisi kama wanawake kuna vitu ambavyo tumezaliwa navyo na vinatufanya tuwe viongozi , ila vitu hivyo kuna wakati vinahitaji kupaliliwa

Mtoto wa kike ana kofia nyingi

“Binti anavaa kofia nyingi kwa wakati mmoja, una nguvu ya kutengeneza mabadiliko chanya, anza kuwa bora kwa kuwavutia wengine.”

Hii ni moja ya machapisho katika kurasa ya Instagram ya 'Dear Girl Child'.

Kwa kila mwanamke ambaye amefanikiwa ujue kuwa mume wake yuko nyuma yake.

Nina mume ambaye si ‘pasua kichwa’ anapenda mafanikio yangu, anapenda kuniunga mkono na ninamshukuru Mungu sana kwa kunipa Patrick Kinemo.

Muhimu ni kuwa na watu wanaokuamini na kukushika mkono na kutengeneza mfumo wa kukusaidia ni muhimu.

m

Chanzo cha picha, Bmk

Kujiamini ndiyo nguzo ya kila mwanamke

Inawezekana kwa kila kijana kujiamini. Ni muhimu kujaribu kuwa na ndoto hata kama unaona ndoto yako haiwezekani. Ni vyema kuwa na ndoto ambayo inakupa dira, usiwe unafiriki leo tu.

Hakikisha kuwa unaongeza thamani ya kwako binafsi, kwa kusoma vitabu, vitu unavyoangalia kwenye mitandao ya kijamii viwe na thamani katika maisha yako ya kila siku.

`Kila kitu unachosoma na kukisikia hakikisha kuwa kinaakisi maisha yako halisi.

Wanawake tuache kufuatilia mitandao ya udaku pekee, tujiongezee thamani kwasababu watu watakulipa kutokana na thamani uliyokuwa nayo. Kumbuka kuwa maisha si rahisi, usidhani kuwa ukimuona mtandaoni Brenda akiwa ameng’aa basi maisha yake ni mepesi, huo si uhalisia. Hakuna maisha ya mteremko au ya kudondoshwa tu, safari ni ngumu.

Simulizi za ‘wamama’ wanaokabiliana na fistula zinaniliza kila wakati

M

Chanzo cha picha, BMK

Katika kazi ninayoifanya, ninaangazia masuala ya fistula ambapo mama anapata tatizo la haja ndogo au kubwa bila kujizuia baada ya kujifungua. Habari njema ni kuwa ugonjwa huu unatibika bila malipo.

Ukikutana na hawa wanawake na wakikusimulia maisha yao, lazima ulie nao. Nimekutana na maelfu ya akina mama wa aina hii, nguvu yetu huwa inakuja kwa kuimba na kusali pamoja.

Kila mwaka, tarehe 23 Mei, tunaadhimisha siku ya fistula, wanawake walikuwa wanateseka na tatizo hili huku jamii ikihusisha ushirikina au wanawake kutokuwa waaminifu, wakati tatizo lipo kwenye sekta ya afya na si kosa la mama.

Miaka 20 iliyopita tulikuwa tunapata wanawake 40 wakati taasisi yetu pekee ndiyo ilikuwa inatoa huduma hiyo, huku takwimu za Umoja wa Mataifa zilionesha kuwepo wanawake 3000 waliokuwa wakiugua fistula Tanzania. Hivyo elimu ni jambo muhimu utafiti ulitusaidia kufikia wanawake wengi zaidi.

Imehaririwa na Florian Kaijage