Prince Harry atoa madai ya kusisimua katika kitabu chake 'Spare'

Msururu wa madai na shutuma za kushangaza kutoka kwa Prince Harry, Spare, umevuja.

Kitabu hicho kinaelezea malalamiko na maumivu katika Familia ya Kifalme, mfano kuna madai kwamba yeye na Prince William walimsihi baba yao asimuoe Camilla.

Lakini moja ya madai yanayojulikana kutoka kwa Harry, yaliyoripotiwa kwanza na gazeti la Guardian, ni jinsi alivyogombana na kaka yake.

 Kasri ya Kensington na Buckingham, zote zimesema hazitatoa maoni.

BBC News imepata nakala ya Spare nchini Uhispania na inaitafsiri.

 Gazeti la The Guardian lilipata nakala ya kitabu hicho na kuchapisha dondoo mapema Alhamisi.

Gazeti la The Sun na mengine pia yalipata toleo la Kihispania baada ya kuchapishwa nchini Uhispania kabla ya tarehe yake rasmi ya kutolewa - ambayo ni tarehe 10 Januari.

 Madai zaidi kutoka katika kitabu hicho yamewekwa hadharani tangu makala ya kwanza ya Guardian.

 Miongoni mwa madai hayo ya Harry ni kwamba William na Catherine, ambaye sasa ni Mwana Mfalme na Binti wa Mfalme wa Wales, walimcheka baada ya kumuona akiwa amevalia sare za Nazi kwenye sherehe.

Pia kuna taarifa za Harry kutumia dawa za kulevya na uzoefu wa Harry kama rubani wa helikopta ya Jeshi katika mgogoro wa Afghanistan.

 Maridhiano na maelewano hayako kwenye ajenda, angalau kulingana na dondoo zilizovuja. Kufikia sasa kuna sauti ya huzuni isiyotatuliwa, malalamiko na shutuma za madai ya Harry.

Ni ya kibinafsi pia, inahusu familia yake ya karibu, kaka, mama wa kambo, dada-mkwe, baba yake.

Kuna wingu la hasira juu ya madai haya na haitawezekana kwa hilo kupuuzwa kwa wakati ujao Harry atakapoonekana na Familia ya Kifalme.

 Sherehe za kumvika taji Mfalme zimebaki miezi michache tu na hazitaangalia simulizi kuhusu Harry.

Harry na William walimsihi baba yao asimuoe Camilla

Harry anaandika kwamba yeye na William walimsihi baba yao asioane na Camilla, ambaye sasa ni Malkia wa Consort, kwa kuhofia angekuwa mama yao wa kambo mbaya, The Sun limeripoti.

The Sun, ambalo lilipata nakala ya Kihispania ya kitabu hicho baada ya kuchapishwa kwa bahati mbaya kabla ya tarehe rasmi ya kutolewa, inaripoti kwamba Harry anadai yeye na kaka yake walikuwa na mikutano tofauti na Camilla kabla ya kujiunga rasmi na familia.

Harry anadai kwamba alitafakari ikiwa siku moja angekuwa "mama yake wa kambo mwenye roho mbaya", lakini kwamba yeye na kaka yake walikuwa tayari kumsamehe "mioyoni mwao" ikiwa angeweza kumfurahisha Mfalme Charles.

Hakuna maelezo yaliyotolewa kuhusu wakati ambao mkutano huo ulipofanyika au Harry alikuwa na umri gani wakati huo.

Mwanamke mwenye ujumbe kutoka kwa Diana

 Harry anaelezea huzuni yake juu ya kifo cha mama yake, Diana, Princess wa Wales, ilisababisha kutafuta msaada kutoka kwa mwanamke ambaye "alidai kuwa na 'nguvu".

"Mama yako anasema unaishi maisha ambayo hangeweza kuishi," Harry anasema mwanamke huyo alimwambia. "Unaishi maisha ambayo alitaka kwako."

Diana aliuawa katika ajali ya gari huko Paris mnamo 1997 wakati Harry alipokuwa na umri wa miaka 12.

Maelezo ya Harry kuhusu mazungumzo ambayo anasema alikuwa nayo na marehemu mama yake ni mafupi, gazeti la The Guardian linasema. Pia hakuna maelezo juu ya wapi au lini mkutano na mwanamke huyo ulifanyika.

William 'alimpiga na kuanguka chini'

Harry anadai kaka yake alishika kola yake, akararua mkufu wake na kumwangusha sakafuni kwenye jumba lake la kifahari la mjini London.

Kitabu hiki kinaweka mabishano kati ya ndugu hao, ambapo Harry anadai yalichochewa na maoni yaliyotolewa na William kuhusu Meghan.

Harry anaandika kwamba kaka yake alikuwa akimkosoa Meghan na William akimtaja kama "mtu mgumu" na "mkali".

Duke wa Sussex alisema kwamba kaka yake "alikuwa akiongea na waandishi wa habari" wakati mzozo ulipokuwa ukiongezeka, kulingana na Guardian.

Harry anasemekana kuelezea kile kilichofuata, ikiwa ni pamoja na madai ya ugomvi wa kupigana.

"Aliweka chini glasi ya maji, akaniita jina lingine, kisha akaja kwangu. Yote yalitokea haraka sana. Kwa haraka sana.

"Alinishika kwenye shingo, akararua mkufu wangu na kuniangusha chini.

"Niliangukia kwenye bakuli la mbwa, ambalo lilipasuka chini ya mgongo wangu, vipande vipande ndani yangu. Nilijilaza hapo kwa muda, nikiwa nimepigwa na butwaa, kisha nikasimama na kumwambia atoke nje."

William na Catherine walimcheka Harry alipovaa mavazi ya Nazi

Maelezo hayo pia yanadai William na Catherine wakati Harry alirudi nyumbani akiwa amevaa mavazi ya Nazi kabla ya sherehe ya mavazi ya kifahari mnamo 2005.

Harry anasema alikuwa akijadili mavazi kwa ajili ya tukio hilo na kuwataka wawili hao kutoa maoni yao, kati ya sare ya marubani na vazi la Nazi ili aweze kuchagua. Anafafanua juu ya kumbukumbu hiyo:

"Nilimpigia simu Will na Kate na kuwauliza wanafikiria nini"

"Sare ya Nazi, walisema"

"Niliikodisha, pamoja na sharubu za kubandika, na kurudi nyumbani"

"Willy na Kate walikuwa wakicheka. Ilikuwa mbaya zaidi kuwa vazi la chuichui la Willy. Ni baya zaidi."

Harry alikuwa na umri wa miaka 20 wakati Sun ilipochapisha picha ya ukurasa wa mbele akiwa amevalia sare kwenye karamu ya mavazi yenye mandhari ya "Alama za Ukoloni".

Kutumia Cocaine akiwa na miaka 17 na kuvuta bangi huko Eton

Harry anasema alipewa cocaine kwenye nyumba ya mtu alipokuwa na umri wa miaka 17 na anakiri kutumia dawa za kulevya mara kadhaa, ingawa hakuifuraia.

Anaandika: “Haikuwa ya kufurahisha sana na haikunifanya nijisikie mwenye furaha hasa kama ilivyoonekana kuwafanya watu wengine wote, lakini ilinifanya nijisikie tofauti, na hilo ndilo lilikuwa lengo langu kuu.

"Nilikuwa mvulana wa umri wa miaka 17 tayari kujaribu chochote ambacho kilibadilisha agizo lililowekwa hapo awali."

Pia anasimulia uvutaji wa bangi bafuni katika Chuo cha Eton wakati mwanafunzi, huku maafisa wa Polisi wa Thames Valley wakihudumu kama walinzi wake waliokuwa wanalinda nje ya jengo hilo.

William alikuwa hapendi kuwa na Harry huko Eton

 "Hunijui Harold. Na mimi sikujui," ndivyo Harry anadai William alimwambia alipokuwa karibu kuanza shule katika Chuo cha Eton.

Harry anasema kaka yake alimweleza "kwamba katika miaka yake miwili ya kwanza huko, Eton alikuwa patulivu,".

"Hiyo ilikuwa bila mzigo wa kaka mdogo ambaye angemsumbua kwa maswali kwenye mzunguko wake wa kijamii," Harry anasema.

Anasema alimwambia William "usijali". "Nitasahau nakufahamu", ndivyo anadai kumwambia kaka yake.

Wapiganaji 25 wa Taliban waliuawa nchini Afghanistan

Akiwa rubani wa helikopta nchini Afghanistan mwaka 2012-13, Harry anasema alishiriki katika operesheni sita, ambazo zote zilihusisha vifo, lakini aliona kuwa ni halali.

"Haikuwa takwimu iliyonijaza kiburi lakini wala haikuniacha aibu," anaandika. "Nilipojikuta nimeingia kwenye joto na mkanganyiko wa mapigano sikuwafikiria wale 25 kama watu. Walikuwa vipande vya mchezo wa chess vilivyoondolewa kwenye ubao, watu wabaya waliondolewa kabla ya kuua watu wema."

William alipendekeza kanisa la kijijini kwa ajili ya harusi ya Harry na Meghan

Harry anadai kuwa familia ya kifalme ilitaka kupanga tarehe na mahali pa harusi yake na Meghan.

Anasema aliposhauriana na kaka yake kuhusu uwezekano wa kufunga ndoa katika kanisa la Westminster Abbey au Kanisa Kuu la St Paul, William alisema haiwezekani kwa sababu palikuwa ndio sehemu za harusi za Charles na Diana na William na Catherine.

William badala yake alipendekeza kanisa la kijiji karibu na nyumba ya baba yao ya Highgrove House huko Cotswolds, anasema Harry.

Harry na Meghan walifunga ndoa katika St George's Chapel, Windsor Castle, Mei 2018.

Hofu kubwa kabla ya kuonekana kwa umma

"Mwishoni mwa majira ya joto ya mwaka 2013, nilikuwa nikipitia wakati mbaya, nikibadilishana kati ya vipindi vya kudhoofika na mashambulizi ya kutisha ya hofu," Harry anaandika katika kumbukumbu yake.

Akielezea majukumu yake wakati huo, kutoka katika kutoa hotuba hadi kufanya mahojiano, Harry anasema alijikuta "hawezi kufanya kazi hizi za msingi".

Muda mfupi kabla ya hotuba, mwili wake ulikuwa ukitokwa na jasho na kuvaa suti ndio chanzo cha hofu ilipoanza, anasema.

"Nilipovaa koti na kufunga viatu, jasho lilikuwa likinitoka mashavuni na mgongoni".