Uchaguzi wa Chadema: Mambo matano muhimu vita vya Mbowe na Lissu

    • Author, Na Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Tanzania
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Huenda historia ikaandikwa leo kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambacho ndio chama kikuu cha upinzani Tanzania, kupata Mwenyekiti mpya baada ya miaka takribani 20 ya uongozi wa Freeman Aikaeli Mbowe, au Mbowe kuendelea na uenyekiti.

Chadema inafanya uchaguzi wa viongozi wake wa ngazi ya taifa huku nafasi ya Mwenyekiti wa chama ikigombaniwa na watu watatu; Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Odero Charles Odero. Hata hivyo mchuano umekuwa mkali zaidi kati ya Lissu na Mbowe.

Mchuano huo wa Mbowe na Tundu Lissu, aliyewahi kuwa Mbunge wa Chadema katika jimbo la Singida Mashariki, pia akapata kuwa Rais wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), umeibua mambo mengi.

Wababe hawa wawili katika siasa za chama hicho wanaitaka nafasi ya uenyekiti. Katika mbio hizo mambo mengine yamezuka kwa faida ya chama na mengine yanaonekana kukiumiza chama.

Pia unaweza kusoma

Chadema bado ina ushawishi

Kuanzia 2010 Chadema ndipo ilianza kuwa chama kikuu cha upinzani, ikivipiku vyama vingine vya upinzani kama Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.

Tangu wakati huo nguvu zake za kisiasa bado ni kubwa, licha ya matokeo mabaya kwa vyama vyote vya upinzani katika uchaguzi wa 2020, ambayo bila shaka yalichangiwa pakubwa na kile ambacho wengine wanachoamini ni 'udhalimu wa kisiasa' uliotokea.

Cheche za chaguzi huu wa ndani zimedhihirisha Chadema bado kina wafuasi na kina ushawishi katika siasa za Tanzania, hasa kutokana na ukubwa wa mijadala inayoendelea kuelekea uchaguzi wao, kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

Kumeguka kwa chama

Uzito wa mijadala na hisia zilizoibuka zimeonesha kuwa ndani ya Chadema kwa sasa kuna makundi mawili makubwa yanayovutana, kundi la Mbowe na la pili ni lile linalomuunga mkono Lissu. Kupitia mitandao ya kijamii makundi haya yameshambuliana na kudhihirisha upinzani kati yao, na hata wakati mwengine kutumia maneno ya kejeli.

Lakini kumeguka huku ni tatizo kubwa zaidi kwa ustawi wa chama kuliko mtu mmoja moja. Ustawi wa chama chochote hautegemei umoja wa chama. Kwa kuzingantia hilo, swali ambalo litabaki hadi uchaguzi huu uishe, ni lile linalohusu mustakabali wa makundi haya mawili ndani ya Chadema. Je, yatarudi kuwa pamoja au ndio utakuwa mwanzo wa Chadema kumeguka?

Demokrasia ya kuvuana nguo

Uchaguzi huu umeshuhudia Lissu akimshutumu Mbowe kwa kubadilika na kulegeza misimamo yake dhidi ya chama tawala, akidai mabadiliko ya Mbowe yalianza kuonekana mara tu baada ya kutoka gerezani.

"Mwenyekiti aliyeenda gerezani, si mwenyekiti aliyetoka gerezani miezi minane baadae. Yule aliyetoka gerezani alikuwa tofauti, akiimba maridhiano anaimba mapendano" amesema Lissu.

Pili kambi ya Lissu imetuhumu uwepo wa rushwa ndani ya chama hicho chini ya uenyekiti wa Mbowe.

Januari 17 mwaka huu wakati akizungumza katika mdahalo wa kisiasa, Tundu Lissu alisema, "mimi ndiye niliyekuwa wa kwanza, kupuliza filimbi kwamba kuna rushwa kwenye chaguzi zetu (Chadema). Tuna tatizo. Muda huu tunapozungumza, kuna wajumbe wanasafirishwa, wanawekwa kwenye mahoteli, makambi, wanapewa pesa, wanalishwa na wagombea. Kuna uchafuzi wa aina hiyo, unoafanywa na wagombea na wapambe wao."

Hata hivyo Mbowe ametupilia mbali shutuma zinazoelekezwa dhidi yake na chama pia akisema hazina ushahidi wowote ule.

"Hakuna shutuma hata moja anayoileza hadharani dhidi yangu ambayo ni ya kweli, na tumeshamtaka kama una shutuma au lawama yoyote dhidi ya mwenyekiti, ilete kwenye vikao vya chama vizungumzwe" alisema Mbowe alipokuwa akizungumza na Crown Media.

Akizungunza na BBC Mbowe pia alisema wakati mwengine anajiuliza kama huyu wa kwenye uchaguzi ndiye Lissu wa kila siku anayemfahamu.

Mbowe ameelezea utoaji wa kashfa na matusi vinavyoendelea katika uchaguzi wa chama chao kama utovu wa nidhamu akiongeza kuwa anatumaini uongozi mpya utakao ingia madarakani baada ya uchaguzi utashughulikia hali hiyo kwa nguvu kubwa.

Lissu alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na Mbowe kwa sasa alijibu kwa kusema. "Tukikutana hivi, hatupigani ngumi. Lakini uhusiano haupo kama mwanzoni."

Hatima ya wagombea

Changamoto nyingine iliyopo mbele ya Chadema ni mustakabali wa wagombea wao. Ukirejelea mashambulizi waliyotupiana, ikiwa Lissu atashindwa, swali; ataendelea kubaki na kufanya kazi na Mbowe? Mbowe ambaye amebadilika na kiongozi imara kama alivyokuwa kwabla kukaa kizuizini gerezani?

Na ikiwa Mbowe atashindwa, atabaki Chadema na kuendelea kufanya kazi na Lissu? Lissu ambaye wafuasi wa Mbowe wanasema hana sifa na uwezo wa kuwa mwenyekiti wa Chadema?

Haya ni maswali ambayo yanahitaji muda kupata jawabu sahihi.

Pia muundo wa uchaguzi wa Chadema kila mgombea anajitegemea, ikiwa na maana kura za mwenyekiti na makamo mwenyekiti, zinajitegemea. Kuna uwezekano wa Mwenyekiti wa kambi moja akalazimika kufanya kazi na makamu mwenyekiti wa kambi nyingine, kulingana na namna ushindi utakavyo kuja.

Chadema itameguka ama kusalia moja? Ipi hatima ya atakayeshindwa? Mvutano huu ni kukuwa kwa demokrasia ya chama au ndio mwanzo wa mpasuko wa chama? Maswali haya na mfano wa haya, yatapata majibu baada ya uchaguzi huo kukamilika.

Wapinzani wa Chadema wamepata hoja

Huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini Tanzania, na tayari dalili zinzonesha kipyenga kimeshapulizwa kuelekea mwezi Oktoba.

Baada ya kuraruana wenyewe kwa wenyewe ndani ya Chadema, ni Dhahiri kuwa yeyote atakayeshinda uchaguzi huu ataachwa na dosari pamoja na chama kwa ujumla. Dosari hizo zitatumiwa na wapinzani wa Chadema hususani chama tawala CCM katika kuwarushia makombora katika mbio za uchaguzi.

Profesa Kitila Mkumbo, Mbunge wa Ubungo (CCM) na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, kupitia Wasafi Fm hivi karibuni alitumia mvutano wa Chadema kukishambulia chama hicho, akisema: "Hakuna Chama chenye akili duniani kitaruhusu mwenyekiti na makamu wake, wakaingia kwenye ushindani, hata kama kuna Demokrasia."

Huu ni mwanzo tu, wengine wataungana na Kitila katika kuishambulia Chadema kwa kutumia silaha zao wenyewe.