Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Shambulio la mbwa Afrika Kusini: 'Hatuwezi kuishi katika ulimwengu ambao mbwa hula watoto'
Onyo: Baadhi ya wasomaji wanaweza kupata maelezo katika hadithi hii ya kuhuzunisha.
Wakazi wa kitongoji cha Phomolong nchini Afrika Kusini waliamka kwa mayowe ya kutisha Jumapili iliyopita asubuhi.
Walitoka kwenye eneo ambalo mtoto wa miaka mitatu alipokuwa akishambuliwa na kisha kuuawa na mbwa wawili wa Marekani wanaoitwa pit bull.
Mtoto huyo alikuwa ametoka nje na marafiki zake kwenye ua wa mbele wa lango la jirani, ambapo mbwa hao wawili kwa kawaida walikuwa wamefungwa kwenye banda lao.
Lakini asubuhi hiyo walikuwa huru na wakizurura. Watoto walipokuwa wakicheza ndipo mbwa walimrukia Keketso Saule. Familia yake iliyo na huzuni inasema shambulio hilo la kinyama lilidumu kwa dakika kadhaa.
"Kama mtu asingemvuta mbwa wangemaliza [kumla]," shangazi yake aliyefadhaika, Nthabeleng Saule, aliiambia BBC.
"Upande mmoja uso wake ulikuwa umeliwa na unaweza kuona ubongo wake." Video iliyochukuliwa wakati wa shambulio hilo inaonesha jamaa na majirani waliojawa na hofu wakipiga kelele kwa mshtuko na kuwatazama mbwa hao wakali bila kujua la kufanya na jinsi ya kuingilia kati.
Ni pale tu mtu alipowamwagia mbwa maji ya moto ndipo watu waliweza kuuvuta mwili wa Keketso usio na uhai.
Kwa hasira, umati wa watu waliokimbilia eneo la tukio, waliwageukia mbwa hao na kuanza kuwarushia vitu. Waliweza kumshika mmoja, na kumchoma moto.
Polisi kisha walifika huku jamii ikilipiza kisasi, na mmiliki wa mbwa hao, Lebohang Pali, mwenye umri wa miaka 21, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kufuga mbwa hatari na anaweza kukabiliwa na faini au kifungo cha jela cha hadi miaka miwili au vyote kwa pamoja.
Mbwa wa pili alichukuliwa na kuuawa na kikundi cha ustawi wa wanyama SPCA. Bw Pali tangu wakati huo amepewa dhamana - iliyowekwa ya randi 300 ($18, £15).
Haijulikani ikiwa atarudi kwenye nyumba aliyokuwa amepanga.
Tulipotembelea mtaa katika jimbo la Free State, takriban kilomita 250 (maili 155) kusini-magharibi mwa Johannesburg, mabaki yaliyoungua barabarani nje ya nyumba ya familia ya Saule yalitoa picha ya matukio ya wikiendi ya kutisha.
Mawe, fimbo na gurudumu lililoungua vilitapakaa eneo ambalo mbwa huyo alikuwa amechomwa.
Wakazi walijitokeza kuzungumzia mshtuko na hasira zao kuhusu kile walichokishuhudia Jumapili. "Tukio hili limetuumiza mioyo yetu," alisema Emily Moerane, mama mdogo aliyembeba mtoto wake mchanga.
"Hatutaki Pit Bull tena," alisema, akiongeza kuwa ikiwa mmiliki wa mbwa hatapata anachostahili "tutachukua sheria mikononi mwetu".
Ndani ya nyumba ya Saule, shangazi yake Kekesto alituonesha picha ya mvulana mdogo mwenye macho ya tabasamu kwenye simu yake. Akiwa anapambana kuzuia machozi, alizungumza kuhusu mshtuko wa familia hiyo.
"Mambo si sawa kabisa, hata mama wa mtoto, bibi na babu walishuhudia kilichotokea," alisema. "Itachukua muda kwao kuelewa ni kwa nini [mbwa] walimla mtoto."
Kuwasalimisha mbwa aina ya 'Pit Bull'
Mmoja wa watazamaji nje aliniambia kuwa kulikuwa na mbwa mwingine barabarani, akielekeza kwenye nyumba moja kwa moja mkabala wa nyumba ya Saule.
Mmiliki wa mbwa huyo, Mokete Selebano, alinikaribisha na kunipeleka nje ya uwanja wake wa nyuma, mbwa wake wa rangi ya kahawia akimrukia yeye na mkewe.
"Huyu ni Junior - ni kama mwanangu," alisema. Lakini akihofia chuki ya jamii dhidi ya Pit Bull, Bw Selebano alisema, "Hatuwezi kuishi hivi katika ulimwengu ambao mbwa hula watoto.
Ikiwa jamii ina hasira basi hakuna ninachoweza kufanya. Lakini kumuona akienda kunaniuma sana mimi na mke wangu." Kufuatia msururu wa mashambulizi mabaya ya hivi karibuni, watu wengi kama Bw Selebano wamekuwa wakiwasalimisha mbwa wao kwa hiari.
Siku tatu baada ya kifo cha Kekeswa aina hiyo ya mbwa ilikabidhiwa kwa SPCA baada ya mtoto wa miaka minane Olebogeng Mosime kuuawa na mmoja wiki moja kabla.
Siku hiyo hiyo Kekesto alikufa, msichana alivamiwa na mbwa watatu huko Cape Town. Alijeruhiwa na kukimbizwa hospitalini, na jamii ikawachoma wanyama hao kuwateketeza. Mbwa waliokabidhiwa kwa SPCA wote watathaminishwa mmoja mmoja na shirika hilo limeomba msaada kwa serikali kukabiliana na wimbi hilo.
Kundi lisilo la faida la Animals 24-7 lina kumbukumbu ya mashambulizi mabaya ya mbwa yaliyoripotiwa katika vyombo vya habari vya Afrika Kusini tangu 2004.
Kwa vifo hivyo viwili wiki hii, ambavyo bado havijajumuishwa katika orodha yake, italeta jumla ya vifo hadi 37 katika kipindi cha miaka 18 iliyopita.
Kumi na wanane kati ya waathiriwa walikuwa watoto - watano kati yao wameuawa mwaka huu, na kufanya kuwa matukio mabaya zaidi katika rekodi ya vifo vya watoto.
Vifo vya watoto wanne viliripotiwa mnamo 2017, mwaka mbaya zaidi kurekodiwa tangu 2004 na vifo vinane kwa jumla - na tangu 2016 takribani kifo kimoja kilichosababishwa na mbwa kimeripotiwa kila mwaka.
Kwa mujibu wa kampuni ya mawakili ya DSC Attorneys, inayoshughulikia kesi za majeraha ya binafsi, visa vinavyohusisha mbwa vinaongezeka.
"Tumekuwa na zaidi ya maswali 70 yanayohusiana na kuumwa na mbwa mwaka huu hadi sasa - hivyo wastani wa sita kwa mwezi - na Oktoba pekee tulikuwa na matukio 50% zaidi ya mwezi uliopita,"
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Kirstie Halsam aliiambia BBC.
Kuuawa kwa Storm Nuku mwenye umri wa miaka 10 na mbwa wawili wa familia yake mnamo Septemba kulifanya wakfu wa Sizwe Kupelo kuanzisha ombi la kutaka mbwa hao kupigwa marufuku nchini Afrika Kusini.
"Utetezi wa wapenda Pit Bull ulisema kwamba ni jinsi unavyomlea mbwa. Hivyo watu wengi, wakiwemo wakimbiaji wameshambuliwa na kuuawa na mbwa," linasema ombi hilo ambalo lina saini zaidi ya 129,000 hadi sasa.
"Ni wakati ambapo serikali ya Afrika Kusini inapaswa kuchukua hatua madhubuti na kuweka marufuku kamili ya umiliki wa Pit Bull kama wanyama wa kufugwa."
Vizimba vya mapigano ya Mbwa
Hofu ya uhalifu inahisiwa kuwa sababu kuu katika kuwafunza wanyama kama vile mbwa kuwa walinzi.
Bw Selebano, ambaye alimpata Junior kama ulinzi kwa mke wake alipokuwa peke yake nyumbani, anasema kuna mbwa wengi katika kitongoji cha Phomolong.
Kuongezeka kwa umiliki wa Pit Bulls, haswa katika vitongoji, sio tu kwa ulinzi, lakini kwa mapigano haramu ya mbwa.
Wanyama hao hufunzwa kuwa wakali, huwekwa kwenye vizimba vikali kwenye minyororo kwa madhumuni ya kupigana na kuuana.
Mara nyingi hupangwa na mashirika, watu hulipa kutazama na kucheza kamari kwenye mapigano.
Mwezi Julai, SPCA ilivamia kizimba cha mbwa katika bustani ya Grassy Park, Cape Town, ikiwaokoa mbwa saba, wakiwemo watoto watatu wa mbwa aina ya pit bull, baada ya mamlaka kufahamu kuhusu video ya mbwa wakihimizwa kupigana.
Mapigano ya mbwa hubeba adhabu ya faini ya $4,700 au kifungo cha hadi miaka miwili au vyote kwa pamoja.
"Ufugaji wa nyuma wa nyumba" pia umekuwa tatizo - na wamiliki wa mbwa wa kuzaliana na mifugo mingine kama Boerboels kwa ajili ya mapigano haramu ya mbwa.
Hii ina maana kwamba mbwa hao wanaweza kuonekana kama mbwa wa Marekani lakini ni wakali zaidi na wana uwezekano mkubwa wa kuuma watu, hasa watoto.
Wakosoaji wa marufuku ya moja kwa moja ya Pit Bull wanasema haitamaliza shida ya umiliki usiowajibika. "Mauaji haya ni ya kusikitisha," Lins Rautenbach, msemaji wa Shirikisho la Pitbull la Afrika Kusini, aliiambia BBC.
Lakini aliweka lawama kwa wamiliki wa mbwa hao - akisema sheria zinahitaji kuwekwa ili kukabiliana nao. "Kupiga marufuku kuzaliana kunamaanisha watu nchini Afrika Kusini ambao wanataka kujisikia salama watahama kutoka kwa aina hii ya mbwa hadi kuzalisha aina nyingine. "Kwa hivyo labda tutaona kupungua kwa Pit Bulls , lakini tutaona ongezeko la aina nyingine kama Rottweiler au German Shepherd maulings," alisema.