Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Familia inayojitolea kuchimba makaburi kwa miongo mitano
- Author, Mansur Abubakar
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Kwa zaidi ya miaka 50, familia moja imejitolea kutunza mava makubwa zaidi katika jiji la kaskazini mwa Nigeria la Kaduna – kazi ambayo wakazi wengine hawapendi.
Hadi wiki chache zilizopita, walikuwa wakifanya kazi hiyo bila malipo rasmi - kuchimba makaburi, kuosha maiti na kutunza makaburi, wakipokea michango kidogo tu kutoka kwa waombolezaji.
Mava ya Tudun Wada ilitengwa kwa ajili ya wakazi Waislamu wa jiji hilo na mamlaka karne moja iliyopita.
Familia ya Abdullahi ilianza kujihusisha na kazi hiyo miaka ya 1970 kupitia ndugu wawili - Ibrahim na Adamu. Ndugu hao sasa wamelala chini ya udongo kwenye mava hiyo, na watoto wao wamekuwa walinzi wakuu wa makaburi hayo.
"Mafundisho yao kwetu sisi, watoto wao, yalikuwa 'Mungu anaipenda kazi hiyo na atatupa thawabu hata kama hatupati manufaa yoyote ya kidunia," anasema Magaji, mtoto mkubwa wa Ibrahim Abdullahi (58).
Kazi ya siku saba za wiki
Yeye na binamu zake wawili wadogo - Abdullahi, 50, na Aliyu, 40, (watoto wa Adamu Abdullahi) - ndio wafanyakazi watatu wa kudumu, wote wanaripoti saa 01:00 asubuhi kwa zamu ya saa 12, siku saba kwa wiki.
Magaji hupigiwa simu yake ya mkononi, moja kwa moja kutoka kwa jamaa au imamu - viongozi wote wa kidini jijini wana nambari yake.
"Watu wengi wana namba zetu na mara mtu anapofariki tunapigiwa simu na nasi tunaingia kazini," anasema.
Mmoja wa watatu hao huenda kuiandaa maiti, shughuli inayojumuisha kuiosha na kuifunika kwa sanda. Mwili hupimwa na maelezo yanatumwa kwa walio makaburini ili kaburi lichimbwe.
Mchakato wa kuchimba kaburi unaweza kuchukua karibu saa moja - watu wawili huchimba kwa zamu kaburi la futi 6 (1.8m) - wakati mwingine zaidi ya saa, ikiwa kaburi litakuwa na mawe.
Huchimba makaburi zaidi ya moja kwa siku katika baadhi ya siku - kazi ngumu katika joto la Kaduna.
"Leo pekee tumechimba makaburi manane na haijafika hata mchana, baadhi ya siku hali huwa hivyo," anasema Abdullahi, aliyeanza kazi ya kuchimba makaburi akiwa na umri wa miaka 20.
Nyakati za machafuko
Binamu hao wamekumbwa na nyakati za mfadhaiko - haswa pale ghasia za kidini zinapotokea kati ya wakazi wa jiji Wakristo na Waislamu. Jamii hizi mbili zinaishi pande tofauti za Mto Kaduna.
"Tumekuwa na mizozo kadhaa ya kidini huku Kaduna lakini mzozo mkubwa zaidi ni ule wa mwanzoni mwa miaka ya 1990. Watu wengi waliuawa," anasema Magaji.
"Tulizunguka na kukusanya maiti na kuziondoa mitaani."
Waislamu walipelekwa Tudun Wada kaskazini mwa mji huo na Wakristo kwenye makaburi ya vitongoji vya kusini.
"Ulikuwa wakati wa shida sana kwangu na sikuwa na muda mrefu katika kazi hii, lakini hilo lilinisaidia kuimarisha dhamira yangu ya kuendelea na kazi hii," anasema Magaji.
Kawaida, timu inapochimba kaburi, kwenye msikiti imamu hutangaza wakati wa moja ya sala tano za kila siku kuwa mazishi yatafanyika.
Waumini kisha huenda katika nyumba ambayo mwili unatayarishwa kwa ajili ya swala – na baadaye husafirishwa hadi makaburini kwa maziko, mara nyingi watu wanakuwa wengi makaburini. Na hapo ndipo mwili uliofunikwa hushushwa kaburini.
Ombi la michango
Baada ya ibada kukamilika na kabla ya waombolezaji kuondoka, walinzi wa makaburi huomba michango.
Ombi hilo kwa kawaida hutolewa na Inuwa Mohammed mwenye umri wa miaka 72, ambaye hueleza umuhimu wa familia ya Abdullahi kwa jamii.
Alikuwa akifanya kazi na baba za binamu hao: "Walikuwa na tabia njema na walipenda wanachofanya na wame warithisha watoto wao kazi hii ya kujitolea."
Pesa kidogo zinazokusanywa wakati mwingine zitanunua chakula cha mchana kwa wafanyakazi hao - lakini hazitoshi kwa kitu kingine chochote. Ili kuishi, familia hiyo pia ina shamba ndogo ambapo wanalima mazao ya chakula.
Makaburi hayo yanatumika tena baada ya miaka 40, ikimaanisha kupata ardhi ya kuzika sio suala gumu - lakini ushughulikiaji wa mava ndio muhimu.
"Kuna mengi ambayo yanakosekana kwa sasa - hatuna vifaa vya kutosha vya kufanya kazi, au ulinzi mzuri," anasema Aliyu, ambaye amefanya kazi kwa miaka 10.
Anaeleza jinsi sehemu ya ukuta ilivyoporomoka, hivyo kuwaruhusu wale waliokuwa wakitafuta vyuma chakavu kuiba alama za makaburi.
Baadhi ya makaburi yana vibao vya chuma vilivyoandikwa jina na tarehe ya kuzaliwa na kifo - ingawa wengi hawafanyi hivyo, maulama wa Kiislamu hawawa hamasishi kufanya hivyo. Makaburi mengi huekwa alama kwa mawe na matofali au kwa fimbo.
Kwa vyovyote vile, binamu hao wanakumbuka eneo la kila mtu aliyezikwa kwenye makaburi na wanaweza kuwaelekeza watu ikiwa wamesahau eneo la kaburi la jamaa zao.
Baada ya ziara ya BBC
Kufuatia ziara ya hivi karibuni ya BBC kwenye makaburi hayo, wamepata mabadiliko makubwa.
Mwenyekiti mpya wa halmashauri ya mji, ambaye ofisi yake inasimamia eneo hilo, ameamua kuwaweka kwenye orodha ya malipo.
"Wanastahili, kutokana na kazi kubwa wanayofanya kila siku," anasema Rayyan Hussain kuiambia BBC.
"Makaburi ni nyumba za mwisho kwetu sote na watu wanaofanya kazi ngumu kama hii wanastahili kulipwa, hivyo ofisi yangu itawalipa mradi mimi ni mwenyekiti."
Magaji anathibitisha kuwa wameanza kupokea posho ya mwezi kwa mara ya kwanza: Watano ambao ni wakubwa zaidi, akiwemo yeye mwenyewe, wanapata naira 43,000 (dola za kimarekani 28). Wengine, akiwemo Abdullahi na Aliyu, wanapokea naira 20,000 (dola 13; £10.50).
Hiki ni kima cha chini sana cha mshahara wa kitaifa cha dola $45 kwa mwezi, lakini Hussain anasema anatumai kuwaongezea posho "baada ya muda."
Anasema inasikitisha kwamba mava hiyo ilitelekezwa kwa miaka mingi na wakuu waliopita wa halmashauri za jiji.
Ana mipango ya kukarabati sehemu ya uzio, kuweka taa za umeme wa jua na kuongeza usalama, amesema mwenyekiti.
"Pia najenga chumba makaburini ambapo maiti zinaweza kuoshwa na kutayarishwa kwa maziko, mambo ambayo kwa sasa yote yanafanywa majumbani."
Kwa familia ya Abdullahi, haya yote yanakaribishwa - na Magaji anatumai mmoja wa watoto wake 23 siku moja atakuwa mtunzaji wa makaburi.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah