Hezbollah laonya kueneza vita baada ya wanachama wa kundi hilo kuuawa na Marekani

Kufuatia mauaji ya wanachama kadhaa wa kundi la wanamgambo wa Iraq wa Kataib Hezbollah katika shambulio la ndege za Marekani, kundi hilo limeonya kuwa litapanua wigo wa operesheni zake iwapo mashambulizi ya Marekani yataendelea.

Afisi kuu ya operesheni za wanajeshi wa Marekani iliyoko Khawamiyane, Centcom, ilitangaza mapema kwamba Jumatano asubuhi (Novemba 22) ilifanya mashambulizi dhidi ya maeneo mawili nchini Iraq ili kukabiliana na mashambulizi ya makundi yanayoungwa mkono na Iran.

Shirika la habari la Associated Press lilinukuu maafisa wawili wa ulinzi wa Marekani - ambao hawakutajwa - kwamba ndege za kivita za Marekani zililenga kituo cha operesheni cha Kataib Hezbollah na kituo cha amri na udhibiti.

Maafisa wa wanamgambo nchini Iraq walisema kuwa wanachama wanane wa Kataib Hezbollah waliuawa katika shambulio la Marekani huko Jarf al-Sakhr, kusini mwa Baghdad.

Serikali ya Iraq ililaani shambulizi hilo la Marekani, ikisema ni "uchochezi hatari" ambao haukuratibiwa na mamlaka ya nchi hiyo.

Mapema Jumatatu jioni, Marekani ililenga kundi la wapiganaji kwa kutumia ndege aina ya AC-130 ambayo ilisema ilishambulia kambi ya Assad kwa makombora ya masafa mafupi. Marekani ilisema wapiganaji watatu waliuawa katika shambulio hilo, lakini Kataib Hezbollah ilisema mwanachama mmoja aliuawa.

Pentagon pia ilisema kuwa vikosi "vinane" vya Marekani na muungano vilijeruhiwa katika shambulio la wapiganaji hao dhidi ya al-Assad kwa makombora ya masafa mafupi, na kambi hiyo iliharibiwa kidogo.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press, Kataib Hezbollah lilisema katika taarifa yake kwamba ikiwa jeshi la Marekani litaendelea na mashambulizi yake, litapanua wigo wa mashambulizi yake, na kuongeza kuwa mashambulizi haya "hayatapita bila kulipa kisasi."

Mashambulizi ya makundi yanayojiita "Islamic Resistance" huko Iraq na Syria dhidi ya Marekani yalianza tarehe 17 Oktoba, ambayo yaliambatana na kurushwa kwa makombora 66 katika vituo vya Marekani na kuwajeruhi wanajeshi wasiopungua 62.

Kataib Hezbollah ni sehemu ya vikosi vinavyojulikana kama Hashd al-Shaabi au Uhamasishaji Maarufu na ilishiriki katika kuingia madarakani kwa Waziri Mkuu Mohammad Shia Sudani yapata mwaka mmoja uliopita.

Mashambulizi ya Jumatatu ya wapiganaji hao yalikuwa ya kipekee kwa kuwa walitumia makombora ya masafa mafupi ya balestiki, na majibu ya Marekani dhidi yake ndani ya Iraq yalikuwa ya haraka.

Kutokana na halii ya kisiasa nchini Iraq, Marekani haijawa na hamu ya kulipiza kisasi dhidi ya wapiganaji wa nchi hiyo, wakati hapo awali ilipiga shabaha mara tatu kujibu mashambulizi hayo nchini Syria.

Katika taarifa yake, serikali ya Iraq iliyataja mashambulio hayo ya Marekani kuwa ni "ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya taifa na jaribio la kuvuruga hali tulivu ya ndani" na wakati huo huo ilizingatia mashambulizi ya makundi yenye silaha dhidi ya maslahi ya taifa.

Baghdad pia ilizingatia mashambulizi dhidi ya jukumu la ushauri la vikosi vya kimataifa nchini Iraq vinavyopigana na kundi la Islamic State (ISIS).

Katika hatua nyingine, afisi kuu ya usimamizi wa operesheni za kijeshi za Marekani, CENTCOM, imetangaza kuwa, meli ya kivita aina ya Thomas Hodner imezitungua ndege kadhaa zisizo na rubani ambazo zilirushwa kutoka eneo lililo chini ya udhibiti wa waasi wa Houthi wa Yemen Alhamisi asubuhi (Novemba 23, saa za Yemen).

Kulingana na taarifa hii, ndege hizi zisizo na rubani zilidunguliwa wakati meli ya Marekani ilipokuwa ikishika doria katika Bahari Nyekundu.

Centcom ilisema chombo hicho au wafanyakazi wake hawakujeruhiwa.

Haya yanajiri siku moja baada ya msemaji wa usalama wa taifa wa White House John Kirby kusema utawala wa Joe Biden unazingatia "ainisho linalowezekana" la Houthis kama shirika la kigaidi.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla