Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, dunia inaelekea kwenye mdororo wa kiuchumi?
Ushuru wa Rais wa Marekani Donald Trump umewasha moto katika masoko ya hisa ya kimataifa. Je, hilo linamaanisha tunaelekea kwenye mdororo wa kiuchumi?
Jambo la kwanza la kusisitiza ni kwamba kinachotokea katika soko la hisa - sio lazima wakati wote kiathiri uchumi - kushuka kwa thamani ya hisa haimaanishi kutatokea matatizo ya kiuchumi mbeleni. Lakini wakati mwingine hilo linaweza kuathiri.
Kuporomoka kwa thamani katika soko la hisa, kunamaanisha kuwa kuna tathmini ya msingi ya faida za siku zijazo kwa kampuni yanayounda soko la hisa la ulimwengu.
Kwa kiasi kikubwa, kile kinachotarajiwa katika masoko; ni kwamba ongezeko la ushuru litamaanisha gharama zitapanda na faida zitashuka.
Hilo halimaanishi mdororo wa uchumi utatokea, lakini nafasi ya mdororo kutokea ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya Trump kutangaza ushuru mpya na mpana.
Uchumi huelezwa kuwa uko katika mdororo, pale jumla ya vitu ambavyo sisi na serikali tunatumia au kuuza nje vitapungua kwa vipindi viwili mfululizo vya miezi mitatu.
Kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana, uchumi wa Uingereza ulikua kwa 0.1%, na ripoti ya hivi karibuni ya kila mwezi inaonyesha umepungua kwa kiwango sawa na hicho mwezi Januari.
Makadirio ya kwanza ya jinsi uchumi wa Uingereza ulivyokuwa mwezi Februari, yatatolewa Ijumaa ijayo. Kwa hivyo, bado tuko mbali sana kuweza kusema tumefika katika mdororo.
Hata hivyo, katika ajali ya kuanguka kwa soko la hisa, kuna baadhi ya majeruhi wa kutisha na wanaotia wasiwasi.
Majeruhi wanaotisha
Benki mara nyingi huonekana kama wakala wa uchumi. Mfuatiliaji mmoja anayeheshimika wa soko la hisa, amenambia: "Kitu ambacho kimenitia hofu ni kuanguka kwa benki."
Benki za HSBC na Standard Chartered - ambazo zinafanya kazi katika biashara ya kimataifa kati ya mashariki na magharibi - zote zilishuka thamani kwa zaidi ya 10% usiku mmoja kabla ya kupata nafuu.
Ishara zingine mbaya haziko kwenye soko la hisa bali kwenye ubadilishaji wa bidhaa.
Bei ya shaba na mafuta zinachukuliwa kuwa kipimo cha afya ya uchumi duniani. Zote mbili zilishuka kwa zaidi ya 15% tangu Trump alipue bomu lake la ushuru.
Miaka ya 1930, athari ya Mgogoro Mkubwa wa Kifedha na hofu wakati wa janga la Uviko 19, ni mifano mitatu iliyotuonesha kudorora kwa uchumi katika nchi kubwa.
Inaaminika kuwa hatuwezi kushuhudia kushuka uchumi kwa kiwango cha kama wakati huo katika kipindi hiki, lakini kudorora kwa uchumi nchini Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya kunatarajiwa kwa kiasi kikubwa na wachambuzi wengi wa kiuchumi.
Kansela wa Uingereza Rachel Reeves, anasema gharama za kukopa za serikali huenda zikashuka kwa takriban pauni bilioni 5 hadi bilioni 6 kwa mwaka, huku wawekezaji wakimiminika kwenye usalama wa dhamana za serikali.
Lakini wana hatari ya kukabiliwa na migongano ya risiti za ushuru za serikali ikiwa na uchumi kwa ujumla utakwenda vibaya.