Je, Vinicius Jr atashinda tuzo ya Ballon D'or?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Dakika chache baada ya mashabiki wa Real Madrid kumuimbia Vinicius Jr ili ashinde Ballon d'Or, mshambiliaji huyo wa Brazil alisisitiza kwamba anataka "kusalia klabuni humo milele".

Vinicius Jr alifunga hat-trick ya kuvutia dhidi ya Borussia Dortmund kwenye Ligi ya Mabingwa siku ya Jumanne na kusaidia timu yake kutoka 2-0 na kushinda 5-2 Santiago Bernabeu.

Hangeweza kupanga muda wake bora zaidi wa kutwaa tuzo ya Ballon d'Or, ambayo inachukuliwa kuwa kombe la hadhi kubwa zaidi katika kandanda, inayotarajiwa kutolewa Jumatatu, 28 Oktoba.

Baada ya mechi, meneja wa Real Carlo Ancelotti alimwita Vinicius Jr "mhusika wa ajabu" na kusisitiza "atashinda Ballon d'Or" kutokana na mchezo wake msimu uliopita.

Mazungumzo yanayoendelea ni kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kushinda tuzo hiyo ya kifahari baada ya kuiongoza Real kutwaa ubingwa wa La Liga msimu uliopita, akifunga katika fainali ya Ligi ya Mabingwa na pia baadaye kutajwa kuwa mchezaji bora wa mashindano hayo.

Nje ya uwanja Vinicius Jr alishinda tuzo ya pili ya Socrates mwaka jana, iliyotolewa kwa mwanasoka ambaye amefanya kazi bora zaidi ya kibinadamu kote duniani.

Wengi kwenye mitandao ya kijamii wanahisi mbio za kuwania tuzo ya Ballon d'Or tayari zimekamilika baada ya tetesi kuibuka kuwa Nike wanataka kutoa viatu maalum vya Mercurial Vinicius Jr, siku mbili baada ya sherehe hiyo.

Vyovyote vile, uchezaji wa Vinicius Jr dhidi ya Dortmund katika awamu ya Ligi ya Mabingwa unaweza tu kusaidia kazi yake.

Pia unaweza kusoma

Vinicius Jr alifunga vipi hat-trick yake dhidi ya Dortmund?

Baada ya kuanza kwa kusawazisha mabao, mabao mawili ya mwisho ya Vinicius Jr dhidi ya Dortmund yalikuwa ya kipekee.

Wakiwa 3-2, huku tishio la bao la kusawazisha la Dortmund likiwa limening'inia juu ya Real Madrid, aliuchukua mpira ndani ya nusu yake, akashuka chini upande wa kushoto akimpita Emre Can kwa kasi safi na kupiga shuti kwenye kona ya chini kutoka pembeni mwa lango.

Alikamilisha hat-trick yake dakika za lala salama, safari hii akikimbia kutoka yadi 40 nje, akiwashinda walinzi watatu, na kupiga shuti kwenye paa la wavu.

Kisha alisherehekea kwa kuvua shati lake, akikimbilia kwa mashabiki wa nyumbani ambao waliimba "Ballon D'or - Vinicius Ballon D'or".

Baada ya mechi, Vinicius Jr aliambia chombo cha habari cha Uhispania Movistar: "Ni ndoto iliyotimizwa wakati mashabiki wetu wanaimba jina langu, nataka kuendelea kuwazawadia kwa mabao zaidi na zaidi.

"Nina umri wa miaka 24 na ninataka kubaki na Madrid milele. Nataka kurudisha kila kitu kwa klabu ambayo imenipa mengi sana."

Nani anaweza kushindana na Vinicius Jr kwa Ballon d'Or?

Kuna majina 30 kwenye orodha ya wanaowania tuzo ya Ballon d'Or, wakiwemo Waingereza Harry Kane, Jude Bellingham, Phil Foden, Declan Rice, Bukayo Saka na Cole Palmer.

Mpinzani wake wa karibu anaonekana kuwa kiungo mkabaji Rodri ambaye aliisaidia Manchester City kushinda taji la Ligi ya Premia na Uhispania kubeba Ubingwa wa Uropa msimu uliopita.

Lakini, kulingana na waandishi wachanganuzi wa Uingereza, Vinicius Jr ndiye anayependelewa zaidi.

Alifunga mabao 26 na kutoa asisti 12 katika mechi 51 alizocheza kwa klabu na nchi msimu uliopita, na angekuwa mtu wa tatu ambaye hana jina la Lionel Messi au Cristiano Ronaldo kushinda Ballon d'Or tangu 2007.

Wengine ni mchezaji mwenza Luka Modric mnamo 2018 na Karim Benzema mnamo 2022.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla