Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kutoweka kwa maafisa wa ngazi ya juu kutamletea matatizo Rais Xi Jinping?
Kutoweka kwa maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa China katika miezi ya hivi karibuni, kumezua uvumi kuhusu iwapo Rais Xi Jinping anaanza zoezi la kuwasafisha, hasa wale wanaohusishwa na jeshi.
Mtu wa hivi karibuni ni waziri wa ulinzi Li Shangfu - hajaonekana hadharani kwa wiki kadhaa sasa. Awali, kutoonekana kwake lilionekana ni jambo la kawaida. Lakini maswali yalizidi pale mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani alipobainisha hilo.
Ripoti ya Reuters baadaye ilisema Jenerali Li, aliyekuwa akisimamia ununuzi wa silaha kwa Jeshi la Ukombozi wa Watu wa China (PLA), anachunguzwa kuhusu ununuzi wa vifaa vya kijeshi.
Kutoweka kwake kunakuja wiki kadhaa baada ya maafisa wawili wakuu wa kitengo cha kijeshi kinachosimamia makombora ya nyuklia - na jaji wa mahakama ya kijeshi kutumbuliwa.
Hakuna maelezo mengi kuhusu kutumbuliwa huko, mbali na kuelezwa kuwa ni "sababu za kiafya." Wengi wanasema kwamba mamlaka inadhibiti ufisadi katika jeshi.
Uvumi pia unaenea kwamba baadhi ya makada wa Chama cha Kikomunisti cha China (CCP), kutoka kamatai ya kijeshi inayodhibiti vikosi vya jeshi pia wanachunguzwa.
Jeshi limekuwa katika hali ya tahadhari - mwezi Julai lilitoa wito usio wa kawaida kuwataka wananchi kutoa taarifa kuhusu rushwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Rais Xi pia alizindua ziara ya ukaguzi, alitembelea kambi tano za kijeshi kuanzia Aprili, kulingana na uchunguzi wa BBC Monitoring.
Ufisadi umekuwa tatizo la muda mrefu jeshini hasa tangu China ianze kufanya uchumi huria miaka ya 1970, anabainisha James Char, mtafiti katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nanyang cha Singapore ambaye ametafiti uhusiano kati ya CCP na jeshi.
Kila mwaka China inatumia zaidi ya yuan trilioni moja kwa jeshi huku nyingine zikielekezwa kwenye shughuli za ununuzi, ambazo kwa sababu za usalama wa taifa haziwezi kuwekwa wazi. Ukosefu huu wa uwazi unachangiwa zaidi na mfumo wa China wa chama kimoja.
‘Wakati Xi amepata ushindi fulani katika kupunguza rushwa ndani ya jeshi na kurejesha sifa yake kwa kiasi fulani; kung'oa rushwa ni jambo la kutisha ama jambo lisilowezekana kwani itahitaji mabadiliko ya kimfumo ambayo ninaogopa kusema kuwa serikali ya China haitokuwa tayari nayo," anasema Dk Char aliongeza.
"Hadi serikali ya CCP itakapo kuwa tayari kuweka mfumo sahihi ambao haujisimamii wenyewe."
China na Washindani wake
Mwezi Julai, sheria iliyoboreshwa ya kukabiliana na ujasusi ilianza kutumika nchini Uchina, ikiipa serikali nguvu zaidi za kufanya uchunguzi. Muda mfupi baadaye, wizara ya usalama ya serikali ya China iliwahimiza hadharani raia kuwasaidia kupambana na shughuli za kijasusi.
Kutoweka kwa Jenerali Li kunalingana na kutoweka kwa waziri wa mambo ya nje Qin Gang, ambaye kuondolewa kwake mwezi Julai pia kulisababisha uvumi mkubwa.
Wiki hii, jarida la Wall Street Journal liliripoti kuwa Qin alikuwa akichunguzwa kuhusu madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi nje ya ndoa ambayo yalisababisha mtoto kuzaliwa nchini Marekani.
"Kuwa na uhusiano wa kimapenzi sio jambo baya kwa makada wa chama hicho - lakini kuwa na mtu ambaye anaweza kushukiwa kuwa ni jasusi wa kigeni na kuzaa naye mtoto - akiwa na pasipoti ya mpinzani wako mkuu wa kijiografia, hilo linaweza kuleta shida, "anabainisha mchambuzi wa China, Bill Bishop.
Pia kuna uvumi kwamba Xi yuko chini ya shinikizo la ndani la chama ili kusafisha uchafu, wakati China inapambana na uchumi unaodorora baada ya Uviko 19 na kuongezeka kwa ukosefu wa ajira kwa vijana.
Chini ya mfumo wa kisiasa wa China, Xi sio tu rais wa China bali pia kiongozi mkuu wa jeshi.
Mduara wa Rais Xi
Kufikia 2017 Xi alikuwa amewaondoa maafisa wakuu zaidi ya 100. Wakati huo shirika la habari la serikali Xinhua lilisema katika makala kwamba idadi hiyo ilizidi idadi ya majenerali waliouawa katika vita ili kuunda China mpya.
Miaka mingi ya kuwaondoa wale ambao wameacha kuwa upande wake na kuwaweka katika nyadhifa za juu wafuasi wake inaweza kumaanisha kuwa Xi amejizungushia watu wa 'ndio mzee.'
Kutoweka kwa maafisa kumetokea zaidi wakati wa mvutano kati ya China na Taiwan, na China ilituma meli za kivita na ndege za kijeshi wiki za hivi karibuni.
Wengine hata hivyo wanasema kuwa uongozi wa kijeshi wa China uko imara vya kutosha kuhimili uwekwaji wa baadhi ya maafisa wakuu wapya, na kueleza kuwa imekuwa makini katika nyakati za misukosuko.
‘Wengine wanaamini kutoweka kunaweza kuleta athari za muda mrefu kwa utulivu wa uongozi wa Bw Xi. Hakuna hata mmoja miongoni mwa makada ambao wameondolewa hadi ambaye ni sehemu ya mduara wake wa ndani,’’ anasema Neil Thomas, mtaalamu wa siasa za China katika Taasisi ya Sera ya Jumuiya ya Asia.
Jambo ambalo wachambuzi wengi wanaweza kukubaliana nalo ni kwamba matukio haya yanaashiria kukosekana kwa uwazi katika mfumo wa kiutawala wa China.